Home Habari za michezo MAYELE,CHAMA PASUA KICHWA SIMBA, JAMBO JIPYA LAIBUKA UARABUNI

MAYELE,CHAMA PASUA KICHWA SIMBA, JAMBO JIPYA LAIBUKA UARABUNI

Habari za Simba na Yanga

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikikubali yaishe kwa mshambuliaji wake, Fiston Mayele kwenda kujaribu changamoto nyingine Pyramids FC ,mgogoro mpya umeibuka kwa kiungo fundi, Clatous Chama na Simba.

Mayele sasa hatakuwa na Yanga msimu ujao, lakini mioyo ya mashabiki wa timu hiyo haijafurahi kutokana na ubora mkubwa aliouonyesha ndani ya kikosi hicho kwa misimu miwili aliyocheza.

Mashabiki wengi wa Yanga wanahofu kama watapata mbadala sahihi wa Mayele katika miaka ya hivi karibuni na misimu yake miwili aliyocheza Yanga amefunga jumla ya mabao 33 kwenye Ligi Kuu.

Mwanachi linajua kuwa Yanga imepanga kumuaga Mayele kwa heshima, Jumamosi, kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi, sherehe zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Mayele, Chama ameshindwa kujiunga na kambi ya Simba iliyopo Uturuki, kutokana na mvutano uliopo wa kimaslahi, huku kundi la mwisho la wachezaji likiondoka jana.

Beki mpya, Che Malone Fondoh, washambuliaji Jean Baleke na Willy Onana na winga Aubin Kramo waliondoka nchini jana bila kuongozana na Chama kama ilivyoelezwa awali, kutokana na raia huyo wa Zambia kuwa na kikao cha mwisho na viongozi.

Kiungo huyo alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili na nusu akitokea RS Berkane ameugomea uongozi wake kurudi kambini akitaka kuongezewa kitita cha fedha ili kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Hali ilivyo
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwananchi kuwa jeuri ya sasa ya Chama inatokana na mabadiliko ya kimkataba yanayodaiwa kufanywa baada ya kumalizika kwa msimu wa 2012/22, ambayo uongozi wa Simba unadaiwa kupunguza mwaka mmoja.

Sababu za kupunguzwa kwa mwaka mmoja ni kuonekana kuwa na majeraha ya mara kwa mara kwa nyota huyo, huku pia suala la kocha Robert Oliviera ‘Robertinho’ kutokuwa na mpango wa kumtumia zaidi msimu ujao.

Suala la mkataba ambalo linadaiwa kumpa nguvu Chama, ni kipengele cha mkataba kinachodaiwa kubadilishwa na kusomeka mwisho ni 2023, badala ya Juni 2024, kama ambao ulipelekwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, ambaye alikiri kuwa ni kweli Baleke, Onana, Che Malone na Kramo waliondoka nchini jana alfajiri kwenda kambini Uturuki bila kuwepo kwa Chama.

“Kundi la pili limeondoka alfajiri ya leo (jana) na Chama hajaondoka kwenda Uturuki, suala lake lipo katika uongozi wa juu wakijaribu kulishughulikia litakapoamriwa basi tutawajulisha,” alisema Ahmed.

Inaelezwa kuwa kiungo huyo mshambuliaji amewaandaa wanasheria wake kwa ajili ya kumtetea katika upande huo wa mkataba, kwani alionao unatarajiwa kumalizika 2023, wakati uliopo TFF ukisomeka mwisho ni 2024.

Kinachoonekana ni kwamb Simba inaamini kuwa inaweza kubaki katika mkataba uliopo TFF ili kukwepa kumlipa Chama upya fedha ya usajili kama inavyodaiwa kuwa anataka kiasi kikubwa.

Awali, ilielezwa kuwa madai ya Chama ni ya kawaida kutokana na kukubaliana tangu 2021, kuwa watakuwa wakimpa fedha kila msimu unapoanza, japo haikujulikana ni kiais gani.

Taarifa za kumpa hela zilithibitishwa na mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, aliyekiri kuwa walikubaliana kama kumpa kiasi fulani cha fedha kila mwanzo wa msimu, lakini mwaka huu mambo yamekuwa tofauti, kwani mchezaji huyo ameona fedha hizo ni kidogo.

SOMA NA HII  KISA KUIFUNGA ARGENTINA...MFALME SAUDI ARABIA ATANGAZA SIKU YA MAPUMZIKO NCHI NZIMA...