Home Habari za michezo GAMONDI WA YANGA NAE ATAMBA, AWATAJA MASTAA HAWA KATIKA USAJILI WA MSIMU...

GAMONDI WA YANGA NAE ATAMBA, AWATAJA MASTAA HAWA KATIKA USAJILI WA MSIMU HUU

Habari za Yanga SC

KATIKA kuhakikisha timu yake inapata ushindi wa mabao mengi, Kocha Mkuu wa Yanga Muargentina Miguel Gamondi ameanza mazoezi ya kimbinu kwa wachezaji wake akitaka mabao kupatikana kupitia pembeni kwa kuwatumia mawinga.

Yanga inaendelea na kambi yake ya pamoja kujiandaa na msimu ujao huko Kijiji cha Avic Town, Kigamboni ambako wapo kwa ajili ya Pre Season chini ya kocha huyo Muargentina.

Safu ya mawinga wa Yanga inatarajiwa kuongozwa na nyota wapya waliotambulishwa wikiendi iliyopita juzi Maxi Nzengeli , Skudu Makudubele, Nickson Kibabage, Jesus Moloko, Denis Nkane na Farid Mussa.

Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Jumatano kuwa, Kocha Gamondi mazoezini kwake ameonekana kuanza kuisuka safu ya ushambuliaji ambayo ina maingizo mapya katika usajili wa msimu ujao huku wakitarajiwa kumuuza mshambuliaji wao tegemeo, Fiston Mayele.

Kocha huyo ndani ya wakati mmoja anawafanyisha program ya gym asubuhi na jioni anahamia mazoezi ya kiufundi kwa kuwataka wachezaji wake kufanya mashambulizi kutokea pembeni ya uwanja.

Aliongeza kuwa, kocha huyo katika mazoezi hayo ya kimbinu ameonekana kuwapa mbinu mawinga wake Maxi, Skudu, Moloko, Kibabage na Nkane kuhakikisha wanapiga krosi safi zote zikifika kwa washambuliaji wa kati Kennedy Musonda, Clement Mzize na Chrispin Ngushi.

Aliongeza kuwa program hiyo pia iliwahusisha mabeki wa pembeni akiwemo mpya kutoka Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast, Attahoula Yao, Kibwana Shomari, Joyce Lomalisa ambao mara kadhaa kocha huyo ameonekana kuwapa maelekezo jinsi ya kupiga krosi safi zitakazozaa mabao zitakazofika kwa washambuliaji wake.

“Kocha hana tatizo na safu ya ulinzi, kwani hakuna mchezaji aliyeondoka zaidi ya aliyeingia ambaye ni Gift (Fred), hivyo hofu kubwa katika safu ya ushambuliaji ambayo wachezaji wengi wameondoka akiwemo Mayele, Kisinda (Tuisila), hivyo yanahitajika maboresho.

“Na hiyo imetokana na maingizo mapya ya wachezaji katika safu ya ushambuliaji aliyebakia ambaye alikuwa katika kikosi cha kwanza ni Musonda pekee ambaye yeye ataongezewa wachezaji wengine huko mbele.
“Hiyo ameanza kutengeneza muunganiko utakaocheza vizuri na kuelewana, ameanza kuwapa mbinu za jinsi ya kutengeneza mashambulizi na kufunga mabao katika kuelekea msimu ujao.

“Amewataka mawinga kupiga krosi safi zitakazofika kwa washambuliaji wake na kufunga mabao, pia mabeki wa pembeni nao wametakiwa kuanzisha mashambulizi kupitia pembeni kwa kupiga krosi zitakazozaa mabao,” alisema bosi huyo.

Gamondi juzi mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini alisema kuwa: “Naitengeneza timu kwa sasa itakayoleta ushindani, kwa kuboresha baadhi ya sehemu, na nitatumia kipindi hichi cha pre season kuwaandaa wachezaji wangu kwa kuwapa mbinu zaidi za ushindi.”

SOMA NA HII  HAYO MAPOKEZI YA MAYELE HUKO MISRI, SIO POA UNAAMBIWA KAMA MFALME