Home news HII SASA SIFA, UNAJUA KWANINI? SIMBA KAMA INATAKA KUKOMOA

HII SASA SIFA, UNAJUA KWANINI? SIMBA KAMA INATAKA KUKOMOA

Tetesi za Usajili Simba

HII sasa sifa. Simba ni kama inataka kukomoa. Unajua kwa nini? Baada ya kukosa taji lolote katika misimu miwili mfululizo, safari hii mabosi wa Simba ni kama wanakomoa kutokana na kushusha vyuma vitupu tangu dirisha la usajili lifunguliwe Julai Mosi.

Ilianza na kumsanisha Willy Onana kutoka Rayon Sports ya Rwanda akiwa ni Mfungaji na Mchezaji Bora wa Ligi ya nchi hiyo. Wakati mashabiki wa Simba wakiendelea kuchekea tumboni, wanamleta tena winga teleza, Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Kuna watu walidhani kazi imeisha, kumbe wapi! Juzi kati si ikamshusha tena beki kitasa kutoka Cameroon, Che Fondoh Malone aliyekuwa CotonSport, kisha mabosi wakaweza pozi kidogo.

Walipoona watu wameanza kujiuliza, ikamtambulisha beki wa kumwaga maji, David Kameta ‘Duchu’ aliyerejeshwa kikosini na mashabiki walionekana kama wamevurugwa kwani akili zao zilikuwa mbali. Walipotangaziwa kuna chuma kinarudi Msimbazi, wengi waliamini ni lazima atakuwa Luis Miquissone kama sio Shiza Kichuya.

Hata hivyo, kumbe mabosi wa Simba walikuwa wanawapima imani tu kwa Duchu, lakini ukweli ni kwamba mipango yao ni kumshusha Luis, aliyeuzwa na klabu hiyo kwa Al Ahly ya Misri.

Taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba mshambuliaji huyo mwenye kasi na aliyeondoka huku mashabiki wakiendelea kuliimba jina lake, yupo hatua nzuri kurudi Simba ili kuungana na kina Onana, Jean Baleke, Moses Phiri na Saido Ntibazonkiza ili kuwavuruga mabeki wa timu pinzani.

Akili za mabosi wa Simba na benchi la ufundi ni kutaka kuwavuruga mabeki wa timu pinzani wasijui wamkabe nani kati ya mashine hizo za mbele ya Simba. Na hapo hajatajwa Pape Osmane Sakho ambaye inaelezwa analazimisha kusepa barani Ulaya kucheza soka la kulipwa.

Msimu uliopita, Simba ilimaliza msimu ikifunga jumla ya mabao 75 ikiwa ndio kinara, huku safu yake ya mbele ikifunga zaidi ya mabao 50, hivyo kuongezwa kwa Kramo, Onana na sasa kuletwa kwa Luis kunaweza kuwa balaa zaidi kwa timu zitakazokutana na Simba.

Kazi ya mashine hizo zitaanza kuonekana kwenye mechi za Ngao ya Jamii zitakazopigwa jijini Tanga, Simba ikianza na Singida Fountain Gate itakayovaana nao Agosti 10 kisha kama itapenya hapo itaumana na mshindi kati ya Yanga na Azam zitakazocheza siku moja kabla jijini humo.

Chanzo makini kimelidokeza Mwanaspoti kuwa, winga huyo kutoka Msumbiji kupitia klabu ya Al Ahly wameafikiana na zinahesabiwa siku kabla ya kuja nchini kwa mkopo ili kuliamsha tena kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.

“Mazungumzo baina ya Simba na Al Ahly juu ya Luis Miquissone yamefuikia pazuri na lolote linaweza kutokea kwa mchezaji huyo kuja nchini, ile ishu ya fedha za mshahara limepata muafaka, ila kwa sasa inafanywa siri kwa vile uongozi umepanga kufanya sapraizi,” kilisema chanzo hicho.

Inaelezwa kwa sasa Simba inasikilizia ishu za Peter Banda na Sakho, ili kupata nafasi ya kumuingiza jamaa (Luis), kwani kwa idadi ya nyota wa kigeni imevuka ile ya 12, hivyo ni lazima mmoja atemwe au kuondoka klabu kutoa kwa nafasi ya mashine mpya zinazosubiriwa akiwamo beki wa kushoto.

“Hadi sasa kuna zaidi ya wachezaji 12 kwa waliosalia msimu uliopita na waliosajiliwa, lakini ishu ya Luis ni suala la muda tu, kwani viongozi wameamua wakitaka kurejesha heshima kwa msimu ujao,” kilisisitiza chanzo hicho.

Hakuna kiongozi yeyote wa Simba aliyepatikana kuzungumzia suala hilo, lakini inaelezwa baadhi yao walikuwa bize kukamilisha taratibu za kundi la mwisho la wachezaji wa timu hiyo kwenda kambini Uturuki akiwamo Jean Baleke aliyekuwa kwao DR Congo kufuatilia viza.

Simba imeanza rasmi mazoezi juzi kwenye kambi hiyo ya msimu mpya, huku ikielezwa mzuka umepanda baada ya kukutana na sapraizi ya mashabiki wa Kitanzania waishio huko sambamba na hali ya hewa ambayo imemfurahisha Kocha Robertinho.

SOMA NA HII  KAPOMBE KUIKOSA DODOMA JIJI LEO JAMHURI