Home Habari za michezo YANGA YABAKISHA SIKU NNE KUWASHANGAZA MASHABIKI NA WADAU

YANGA YABAKISHA SIKU NNE KUWASHANGAZA MASHABIKI NA WADAU

Habari za Yanga leo

ZIMEBAKI siku nne kuanzia leo mashabiki wa Yanga kushuhudia tamasha kubwa la kilele cha Wiki ya Mwananchi ambalo wanalitumia kutambulisha wachezaji wapya na wa zamani watakaowatumia msimu mpya, kuna sapraizi nne.

Kuna mambo manne ya moto ambayo miongoni mwayo yatakuwa ni sapraizi kutokana na uongozi kutoweka wazi hadi sasa.

SAJILI ZA MWISHO

Yanga inaendelea kusajili ni baada ya kinara wa ufungaji Fiston Mayele kuondoka kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo.

Mayele ameuzwa Pyramids ya Misri na uongozi wa timu hiyo upo kwenye mchakato wa kusaka mbadala wake na inasemekana kuwa mbali na usajili eneo hilo pia wana mpango wa kusajili winga na kiungo.

Yanga hadi sasa imetambulisha wachezaji watano kiungo, Jonas Mkude, Nickson Kibabage, Gift Fred, Kouassi Attohoula (wote mabeki) na winga Maxi Mpia Nzengeli.

DIARRA, AUCHO, AZIZ KI

Kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra viungo Khalid Aucho na Stephan Aziz KI hawajarudi tangu walipopata mapumziko.

Mastaa wanaanza kurejea kambini kuanzia leo kwa ajili ya kuwahi wiki ya Mwananchi ambayo kilele chake ni Jumamosi kwa Yanga kukipiga na Kaizer Chief.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ameliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji hao walichelewa kambini kwa ruhusa maalumu na wataanza kurejea leo.

“Walikuwa na ruhusa maalumu wataanza kurejea kila mchezaji ambaye ana mkataba na Yanga ataonekana wiki ya Mwananchi hakutakuwa na mchezaji ambaye hatakuwepo hivyo mashabiki waondoe hofu.”

KOCHA KUONYESHA MBINU

Baada ya kuondoka kwa Nasreddine Nabi, Yanga imemtangaza Miguel Gamondi akitokea timu ya Ittihad Tanger ya Morocco.

Kocha huyu mwenye uraia wa Argentina na Italia ana umri wa miaka 56, mechi yake dhidi ya Kaizer Chief itawafanya wadau wa soka kutambua mbinu zake na ni mfumo gani atakuwa anatumia japo itakuwa ni mapema sana kumjaji.

Kocha huyo ambaye amekuja na wasaidizi wake siku hiyo ndio itatoa mwanga namna gani kikosi kitakuwa cha ushindani kabla ya kuvaana na Azam FC kwenye Ngao ya Jamii.

THANK YOU NYINGINE

Yanga imeachana na mastaa Benard Morisson, Dickson Ambundo, Tuisila Kisinda, Abdallah Shaibu na Erick Johora. Wakati ikitoa wawili tu wa kigeni imeshusha vyuma vinne hivyo inatarajiwa kupunguzwa wengine kutokana na idadi kuwa kubwa.

Mbali na nyota wa kigeni pia kuna nafasi kubwa ya kutoa wengine wazawa kwa mkopo ili kwenda kuboresha viwango huku kuna baadhi kama David Bryson tayari kaenda kujaribu changamoto nyingine JKT Tanzania.

SOMA NA HII  WAKATI JAHAZI LA SIMBA LIKIZIDI KWENDA KOMBO...PABLO AIBUKA NA HILI JIPYA...AFUNGUKA KUHUSU CHAMA...