Home Habari za michezo WAKATI BODI YA LIGI WAKIIKATALIA SIMBA KUCHEZA NA COSTAL…MBRAZILI KAAMUA KUJA NA...

WAKATI BODI YA LIGI WAKIIKATALIA SIMBA KUCHEZA NA COSTAL…MBRAZILI KAAMUA KUJA NA GIA HII…

Habari za Simba SC

KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ mjanja sana, baada ya kugundua kuwa timu hiyo itakaa nje ya uwanjani karibu mwezi mzima kabla ya kurudi kwenye mechi ya mashindano, fasta akaamua kufanya jambo ili kuwaweka mastaa wa timu hiyo katika moto ule ule walioanza nao Ligi Kuu.

Robertinho amesema anaandaa namna bora ya kuhakikisha vipaji vya mastaa wa timu hiyo havishuki kutokana na kutokuwa na mechi yoyote ya kiushindani tangu ilipocheza mchezo wa mwisho na Dodoma Jiji kwa kuomba timu ipate mechi za kirafiki zisizopungua tatu kipindi ligi ikisimama.

Kauli ya kocha huyo raia wa Brazili, imekuja baada ya kuahirishwa kwa mchezo wa timu hiyo dhidi ya Coastal Union ambao awali haukupangiwa tarehe ila kutokana na kutokuwa na mechi yoyote baina yao na Simba iliomba upigwe jana Ijumaa ambako nako ilishindikana kupigwa.

Robertinho alisema hakuna kitu kinachomuumiza kichwa kama jinsi ya kuwaweka wachezaji katika mazingira mazuri ya kiushindani kwa muda uliopo kutokana na kuanza kuelewana na kuingia kwenye mfumo.

“Kila mchezaji ameonyesha ari ya kuipambania timu ili kufikia malengo tuliyojiwekea hivyo kutokana na kutokuwa na mechi ya hivi karibuni inatupaswa kukaa na benchi langu la ufundi ili kuona namna nzuri ya kulinda viwango vyao, na kubwa ni kuomba mechi za kirafiki,” alisema kocha huyo.

Robertinho aliongeza licha ya wachezaji wote kutopata nafasi sawa ya kucheza ila haina maana wanaoanza ni bora zaidi ya wengine isipokuwa kila mmoja wao atacheza ingawa itategemea na aina ya mpinzani anayekutana naye siku husika.

“Nafahamu presha iliyopo kutoka sehemu mbalimbali lakini kwangu najivunia kufanya kazi na wimbi kubwa la wachezaji bora hapa nilipo, kwangu ni nafasi ya kuendelea kuonyesha kila mmoja wao ana umuhimu sawa na wengine bila kujali ni nani.”

Robertinho tangu ateuliwa kukiongoza kikosi hicho Januari 3, mwaka huu ameiongoza timu hiyo katika michezo 13 ya Ligi Kuu kuanzia msimu uliopita na huu ambapo kati yake hajapoteza yoyote kwani ameshinda 11 na kulazimishwa sare miwili tu.

Msimu huu tayari ameshinda michezo miwili ambapo alianza na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar na kisha kuifunga Dodoma Jiji 2-0 na kuifanya timu hiyo ikae kileleni ikiwa na pointi sita na mabao sita, ikifuatiwa na Mashujaa, Geita Gold zenye pointi nne kila moja na Yanga yenye pointi tatu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUGOTESHWA KWENYE MAPINDUZI CUP....GAMONDI AAPA KUFA NA HILI NDANI YA YANGA...