Home Habari za michezo GAMONDI AFURUGWA NA WASHAMBULIAJI WA YANGA, AWAPA NENO HILI

GAMONDI AFURUGWA NA WASHAMBULIAJI WA YANGA, AWAPA NENO HILI

Habari za Yanga SC

Kocha Mkuu wa Yanga SC, Miguel Gamondi amewataka washambuliaji wa timu yake kuhakikisha wanatengeneza rekodi kubwa ya kufunga magoli ya kutosha kutoka kwa kila nafasi wanayoitengeneza tofauti na msimu uliopita ambao walizidiwa na Simba kwa kufunga magoli.

Ikumbukwe msimu uliopita Ligi Kuu Bara, Simba chini ya Robertinho Oliveira, ilihitimisha ligi hiyo ikiwa imefunga jumla ya mabao 75 ikimaliza katika nafasi ya pili wakati wapinzani wao, Yanga licha ya kuwa mabingwa walifunga jumla ya mabao 61 tu, jambo ambalo limemfanya Gamondi kuwatolea macho washambuliaji wa timu hiyo.

Akizungumza na Nipashe, Gamondi amesema moja ya mkakati wake mkubwa ni kuhakikisha washambuliaji wa timu hiyo wanaweza kufunga mabao mengi zaidi ili kuvunja rekodi ya wapinzani wao, Simba ya msimu ulioisha katika Ligi Kuu Bara licha ya wao kufanikiwa kuchukua ubingwa.

Amesema jambo muhimu ni kupata bao katika kila mchezo wa ligi ambao watacheza kwa sababu itawasaidia kupunguza presha kubwa kutoka kwa wapinzani.

“Jukumu la kwanza la kufunga lipo kwa washambuliaji halafu na kwa timu nzima katika kila nafasi ambayo itakuwa imepatikana kufanya hivyo, kuna kila sababu hasa upande wa safu ya ushambuliaji kuongeza kasi na umakini wa kutosha katika kutimiza majukumu yake.

“Nataka kuona wakifunga mabao mengi zaidi, angalia msimu ulioisha licha ya kushinda ubingwa, timu ilizidiwa mabao mengi na wapinzani jambo ambalo sihitaji kuona likijirudia kwa sasa, msimu ujao unaelekea utakuwa wa ushindani kwa kila timu kujipanga vizuri,” amesema Gamondi.

Ameongeza kuwa maelekezo hayo kila mchezaji anayajua li cha ya kuendelea kutengeneza muunganiko wa kikosi chake pamoja na kuwataka wachezaji kutumia kila nafasi watakazozipata kufunga mabao.

Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka leo kuelekea Tanga kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, utakaopigwa keshokutwa, Jumatano kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

SOMA NA HII  TAIFA STRAS YATENGEWA BILIONI 1.6 KUFUZU KOMBE LA DUNIA QATAR...MAJALIWA ATOA AGIZO...