Home Habari za michezo KANOUTE, MZAMIRU MTEGONI SIMBA NGOMA ATAJWA ISHU IKO HIVI

KANOUTE, MZAMIRU MTEGONI SIMBA NGOMA ATAJWA ISHU IKO HIVI

Kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Fabrice Ngoma ni wazi amewaweka mtegoni viungo Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin katika vita ya kuwania nafasi katika kikosi hicho msimu ujao.

Simba SC imemnasa Ngoma mwenye umri wa miaka 29 kutoka Al Hilal ya Sudan, anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji kuimarisha kikosi chake kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali msimu ujao.

Ujio wa nyota huyo aliyewahi kukipiga AS Vita ya DRC na Raja Casablanca ya Morocco, kuna uwezekano utaleta vita ya aina yake kugombea nafasi katika kikosi cha kwanza.

Kocha wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, msimu uliopita alikuwa akiwatumia mara kwa mara Kanoute na Mzamiru katika kiungo wa ulinzi na wakati akimpa mwingine nafasi Nassor Kapama katika eneo hilo.

Hata hivyo, msimu uliopita kocha huyo mara chache alikuwa akiwapa nafasi Victor Akpan, Erasto Nyoni na Jonas Mkude ambao wameshatimka katika kikosi hicho.

Kama Robertinho ataamua kutumia mfumo wa viungo wawili msimu ujao, Ngoma ambaye alikuwa na kikosi hicho katika kambi ya Uturuki, ana nafasi kubwa ya kuanza na mmoja kati ya Kanoute na Mzamiru.

Ikiwa Mbrazili huyo ataamua kutumia kiungo mkabaji mmoja, hatua hiyo inaweza kuongeza ushindani kwa kuwa nyota wote watatu watawania nafasi moja.

Mfumo huo unaweza ukawapa ugumu zaidi Kanoute na Mzamiru katika kikosi cha kwanza huku Ngoma akitabiriwa kuwa na nafasi kubwa ya kuanza.

Kocha na mchambuzi wa soka nchini, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’, amesema anaamini usajili wa Ngoma katika kikosi hicho utaongeza ushindani katika eneo la kiungo na ubora wa kikosi.

“Ni usajili mzuri kwa kuwa utaongeza ushindani wa wachezaji katika kikosi kwani kila mmoja atahitaji kupata nafasi ya kucheza katika timu, lakini Robertinho atamtumia zaidi mchezaji anayefanya vizuri katika mazoezi,”amesema.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Zamoyoni Mogella, amesema usajili huo utaiimarisha Simba.

“Ni usajili mzuri utakaokwenda kuwaamsha Kanoute na Mzamiru. Simba SC inahitaji kufanya makubwa msimu ujao;” amesema.

SOMA NA HII  THE CRANE YA UGANDA YAKANUSHA TAARIFA YA YANGA KUHUSU BEKI WAO HUYU