Home Habari za michezo KISA AL AHLY….MBRAZILI SIMBA AWAPA MAJUKUMU HAYA CHAMA NA PHIRI….

KISA AL AHLY….MBRAZILI SIMBA AWAPA MAJUKUMU HAYA CHAMA NA PHIRI….

Habari za Simba

Saa chache baada ya kufanyika kwa droo ya michuano mipya ya African Football League (CAF Super League) na Simba kujikuta ikipangwa kuvaana na Al Ahly ya Misri, kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliamua kukaa na nyota wawili wa kimataifa kutoka Zambia, Clatous Chama na Moses Phiri.

Wazambia hao waliteta na Robertinho kwa ajili ya kutaka kujua uimara na udhaifu wa Power Dynamos ambayo watakutana nayo kwenye mechi za raundi ya pili za Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Septemba 16 na Oktoba Mosi kuwania tiketi ya kutinga makundi ya michuano hiyo kwa msimu huu.

Mwanaspoti limepenyezewa, kocha Robertinho alikaa mezani na mastaa hao akitaka wampe mkanda mzima kuhusu Dynamos ambao licha ya kucheza nao kwenye mechi ya kilele cha Tamasha la Simba Day ikiifunga mabao 2-0, lakini kwa sasa wanakutana kwenye mechi ngumu ya kuamua hatma yao kimataifa msimu huu.

Taarifa hizo zinasema, Phiri na Chama walimfichulia kila kitu juu ya timu hiyo waliyowahi kuvaana nayo wakati wakicheza nchini humo na kumwambia awaachie msala wao kwani kazi iakuwa nyepesi tofauti na presha aliyokuwa nayo kocha huyo.

Mastaa hao walimueleza Robertinho mambo mengi kuanzia aina ya maisha ya Zambia, wakamchambua mchezaji mmoja mmoja wa Dynamos na kisha wakamaliza kwa kumuomba awape nafasi kwenye mchezo huo kwani wana uchu wa kuonyesha ubora wao wakiwa kwenye ardhi ya kwao jambo ambalo kocha aliafiki.

Pia kocha huyo hakuishia kuchukua madini kwa Chama na Phiri tu, ila aliamua kuiangalia mikanda ya video ya mechi za Dynamos za hivi karibuni akiwa sambamba na wataaalamu wengine wa benchi wakiongozwa na ‘video analyst’ wa timu hiyo, Mzimbambwe Culvin Mavunga na kubaini mambo mengi ya kiufundi.

Robertinho aliithibitishia Mwanaspoti kufanyika kwa mambo hayo kambini na kusisitiza ni wakati wa Simba kuonyesha ukubwa wake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kugeukia michuano mipya ya Supa Ligi.

“Tunajiandaa na mechi zijazo lakini kwa sasa tunaangalia zaidi mechi na Dynamos, tumepata muda wa kutosha kufanya utafiti kuhusu timu hiyo, kwa kutumia wataalamu na vyanzo vyetu mbalimbali. Tumebaini ni timu nzuri na yenye ushindani zaidi hususani inapocheza nyumbani, lakini Simba ni timu kubwa na nadhani huu ndio muda wa kuonyesha ukubwa wa timu hii uwanjani,” alisema Robertinho.

Chama alipoulizwa na Mwanaspoti, alikiri Dynamos ni timu yenye msuli mkubwa na ushawishi nchini Zambia, ila yeye na wenzake wamejipanga vyema kwa ajili ya mechi ya kwanza itakayopigwa Septemba 16 kabla ya kurudiana nao Oktoba Mosi, jijini Dar es Salaam.

“Dynamos ni timu niliyoipenda sana, mwaka 2009 hadi 2011 ilikuwa moto kama Barcelona ya enzi hizo na niliwahi kucheza kama miezi sita kabla sijatua Zesco. Ni timu nzuri ndio mabingwa wa Zambia.

“Tumewahi kucheza nao lakini wakati huu itakuwa kwenye mtoano hivyo naamini itakuwa mechi nzuri na tutawapiga,” alisema Chama aliyejiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos kisha mwaka 2021 kuuzwa kwa RS Berkane ya Morocco lakini mwaka jana alirejea katika dirisha dogo na kukutana na Phiri aliyejiunga msimu uliopita akitokea Zanaco pia ya Zambia.

SOMA NA HII  BAADA YA YANGA KUTOBOA CAF...KAZE AIBUKA NA 'KICHAMBO' KWA MASHABIKI...