Home Habari za michezo PAMOJA NA KUFUZU AFCON MWAKANI…KILICHOIBEBA TAIFA STARS MBELE WA WAARABU HIKI HAPA…

PAMOJA NA KUFUZU AFCON MWAKANI…KILICHOIBEBA TAIFA STARS MBELE WA WAARABU HIKI HAPA…

Taifa Stars

Kujitoa ni miongoni mwa siri ambazo zimeelezwa na wachezaji wa Taifa Stars baada ya timu hiyo kuweka historia ya kututinga kwa mara ya tatu kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), huku Uganda ikibaki midomo wazi kwa vijana wa Adel Amrouche kuilazimisha Algeria suluhu.

Ni Tanzania na Uganda, ambazo zilikuwa zikipigania nafasi hiyo, huku Taifa Stars ikionekana kuwa na kibarua kizito zaidi ugenini dhidi ya kinara wa Kundi F, Algeria, ambayo tayari ilishafuzu kwa fainali hizo za mwakani nchini Ivory Coast.

Akiwa kwenye ardhi ambayo atakuwa akicheza soka la kulipwa nchini humo, Simon Msuva ambaye siku chache zilizopita alijiunga na JS Kabylie, alisema iliwabidi kila mchezaji kujitoa kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Ninafuraha sana kulisaidia Taifa langu kwa mara nyingine kufuzu Afcon, hii ni nafasi ambayo mataifa mengi yaliitaka, kiukweli kazi ilikuwa kubwa na ngumu na hatukuwa na budi zaidi ya kuamua kila mchezaji kujitoa kwa ajili ya timu, sote tunajua ubora wa Algeria lakini tuliingia na mpango,” alisema Msuva.

Miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa nguzo kwenye kujilinda, Haji Mnoga, ambaye anacheza soka la kulipwa England akiwa na kwa mkopo Aldershot Town, alisema: “Kila ambapo niliwajibika kulinda sikuwa nikihisi kuchoka, nilijiona fiti kucheza zaidi na zaidi kwa ajili ya kufanikisha hili.”

Taifa Stars imetinga Afcon baada ya kuvuna pointi nane, huku Uganda ikichemka ikiwa na pointi saba kwenye nafasi ya tatu, kinara wa kundi hilo ni Algeria, ambayo imekusanya pointi 16, haijapoteza mchezo wowote.

AKicheza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Taifa Stas, kiungo wa Azam FC, Sospeter Banyana alisema: “Mungu ni mwema sana jana (juzi) nimecheza mchezo wangu wa kwanza nikiwa na timu ya Taifa na kufuzu Afcon, kazi imekamilishwa

Wachezaji wengine ambao wameweka historia ya kuisaidia timu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza ni pamoja na Beno Kakolanya (Singida BS), Erick Johora (Geita Gold), Ibrahim Hamad (Yanga), Clement Mzize (Yanga), Abdulmalik Zakaria (Namungo), Lameck Lawi (Coastal Union), Morice Abraham (Sparkat Subotica), Haji Mnoga (Aldershot Town), Ben Sharkie (Basford Utd) na Abdi Banda Richards Bay).

Aliyekuwa winga wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Dua Said alisema mbali na watu kuona Stars itafungwa ugenini, lakini aliaamini kikosi na mpango wa kocha Amrouche uliisaidia timu hiyo.

Dua alisema kuwa mpango alioingia nao kocha Amrouche umeisaidia Taifa Stars, kwani iliihitaji sare au ushindi pekee ndiyo ifuzu.

“Ukicheza na timu kama Algeria nyumbani kwao unatakiwa uingie na mpango kama ule wa kukaba na kuziba lango kwa kuwa ukijifanya unakwenda kuwashambulia wale jamaa wanakuadhibu, kwahiyo pongezi kwa makocha na wachezaji, walijituma na kufanya kazi kubwa,” alisema Dua.

Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Juma Pondamali alisema anaamini kujitoa kwa wachezaji kumeifanya miamba hiyo kufuzu kwa mara ya tatu Afcon.

Pondamali alisema kikubwa alichokiona ni kuwa namna wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi kusaidia kwa uzoefu wao, akiamini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikisaidiana na klabu nchini kuwauza vijana kupata uzoefu nje itaisaidia zaidi kizazi kijacho.

“Mpango wa Kocha umeenda vizuri, lakini kingine nilichokiona ni namna vijana wanaocheza nje wanavyojiamini wakiwa uwanjani, kwakuwa tayari wana uzoefu kidogo na timu zao, naamini wakitolewa wengi itasaidia kutoa unyonge wa kufungwa kila siku,” alisema Pondamali.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Boniface Mkwasa alisema mechi ilikuwa ngumu, lakini uwezo wa vijana na kufuata maelekezo ya kocha uliisaidia timu kupata matokeo.

Mkwasa alisema: “Naamini maandalizi mazuri kujituma na kusikiliza kocha nini anataka ndiyo iliisaidia Stars kupata matokeo.”

Pongezi zilikuwa kila mahali baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo kwenye Uwanja wa May 19, mjini Annaba, Algeria, wakati Taifa Stars ikifuzu kwa mara ya tatu kucheza mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Miongoni mwa waliotoa pongezi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kupitia akaunti zake za mitandao ya Twitter na Instagram, aliandika: “Hongereni vijana wetu wa Taifa Stars kwa kufuzu michuano ya kuwania kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (2023 Africa Cup of Nations). Mmeandika historia kwani hii ni mara yetu ya 3 kufuzu tangu kuanzishwa kwa mashindano haya. Nawatakia kila la kheri.”

Mwanaspoti.

SOMA NA HII  SIMBA YAWEKA WAZI ISHU YA KUACHANA NA BANDA....... ISHU IKO HIVI