Home Habari za michezo BAADA YA SIMBA NA YANGA KUSMHINDWA…WAARABU WA MAFUTA KUMNG’OA BRUNO SINGIDA…

BAADA YA SIMBA NA YANGA KUSMHINDWA…WAARABU WA MAFUTA KUMNG’OA BRUNO SINGIDA…

Tetesi za Usajili

ACHANA na ushindi wa bao 1-0 ambao Singida Big Stars iliupata dhidi ya Future FC ya Misri katika mchezo wa awali wa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kubwa zaidi ni baada ya mechi iliyopigwa Azam Complex – Chamazi kumalizika, mchezaji wa timu hiyo, Bruno Gomes alionekana lulu, huku uongozi ukisema unasikilizia ofa.

Baada ya mchezo huo kumalizika baadhi ya wachezaji wa Future FC walimfuata Bruno na kuonekana wakizungumza naye huku wakionyesha kama vile kuna jambo ambalo wanahitaji kujua kutoka kwa nyota huyo wa Kibrazili.

Wakati huohuo, viongozi wa Future FC walionyesha nia ya kuhitaji kuzungumza na nyota huyo, lakini kutokana na muda kuwa mfupi walionekana wakichukua namba yake ya simu kwa ajili ya mazungumzo naye ya kina baadaye.

Licha ya namba ya Bruno kuchukuliwa, bado wachezaji wawili wa Future FC walitoka na kwenda kukaa mlangoni katika vyumba vya kubadilishia nguo walivyotumia Singida wakionekana kana kwamba wanamsubiri Bruno, lakini baada ya kuona wapinzani wao wanachelewa kutoka ndani waliamua kuondoka sehemu hiyo.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo kama kuna ishu ya staa huyo kutimkia Misri, ofisa habari wa Singida Big Stars, Hussein Masanza alikiri ubora wa Bruno hivyo ni kitu cha kawaida kwa timu zingine kuhitaji huduma yake.

Masanza alisema tukio hilo kama uongozi hawakuliona kwa sababu tayari walikuwa vyumbani, lakini hawezi kulizungumzia sana kwa sababu mchezaji hajasema lolote na hata viongozi wa Future hawajasilisha ombi lolote kwa uongozi kumtaka nyota huyo.

“Kwanza Bruno sisi ni mchezaji wetu hadi 2025. Kwa hiyo hatuna wasiwasi wowote ule kwa sasa. Kuhitajika kwake sio jambo baya kwa sababu ni mchezaji mzuri na timu nyingine zinapenda kupata huduma yake,” alisema.

“Bado (Future) hawajaja ofisini kwetu kwa sasa, lakini wakija uongozi utaangalia ofa yao na ndipo majibu yatatoka. Kwa sasa ni ngumu sana kusema lolote maana hakuna ofa rasmi mezani kwetu.”

Bruno amekuwa na kiwango bora katika kikosi cha Singida tangu ajiunge nayo msimu uliopita na tayari timu kadhaa zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake baada ya kuonyesha kiwango bora katika Ligi Kuu zikiwemo Simba na Yanga kwa nyakati tofauti.

SOMA NA HII  KAMATI:- MWAMUZI ALIINYONGA SINGIDA FG ...KONA HAIKUWA SAHIHI ....