Home Uncategorized KIGOGO AFUNGUKIA USAJILI WA NIYONZIMA YANGA

KIGOGO AFUNGUKIA USAJILI WA NIYONZIMA YANGA


UONGOZI wa Yanga umekanusha tetesi za kiungo wao wa zamani Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kuwa anaweza kujiunga tena na timu hiyo.

Taarifa hizo zilianza kuzagaa juzi mitandaoni wakati tamasha lao kubwa la ‘Kubwa Kuliko’ likiwa linaendelea kwenye Ukumbi wa Dimaond Jubilee, Upanga jijini Dar es Salaam.

Niyonzima ni kati ya wachezaji waliomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara akiwemo pia Mganda, Emmanuel Okwi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa timu hiyo, Mshindo Msolla alisema kuwa haitawezekana kwa kiungo huyo kurejea Yanga hivi sasa. Msolla alisema, mchezaji huyo hayupo kwenye mipango ya kocha, hivyo ni ngumu kusaini kwao na wao wanafanya usajili kwa mujibu wa ripoti ya Mwinyi Zahera.

Aliongeza kuwa, wanaheshimu uwezo wa kiungo huyo, lakini kwa hivi sasa hana nafasi na badala yake wanaendelea kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya ligi kuu bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Wachezaji wapo wengi wa kusajili nje na ndani ya nchi tofauti na huyo Niyonzima, hivyo Niyonzima kuichezea tena Yanga haitawezekana.

“Usajili wetu Tunaufanya kiufundi zaidi kwa kusajili wachezaji wale wote kocha aliowatolea mapendekezo ya usajili na huyo Niyonzima hayupo,”alisema Msolla.

SOMA NA HII  MATUSI YA AMUNIKE VYUMBANI KWA WACHEZAJI, YONDANI AMWAGA MACHOZI - VIDEO