Home Habari za michezo KARIA AIBWAGA SIMBA KAMA MASIHARA

KARIA AIBWAGA SIMBA KAMA MASIHARA

Unahitaji muda sana kuuelewa mpira wetu. Una njia zake. Unajiendesha kivyake vyake. Nigumu sana kumpata Mtanzania ambaye sio shabiki wa Yanga wala Simba. Ni vigumu sana.

Wapo wachache sana ambao ni Cosmopolitan piga ua. Hawajawahi kubadilika miaka nenda, miaka rudi. Wapo wachache sana ambao pia ni mashabiki wa Coastal Union. Wapo kabisa lakini, ni wachache. Wapo mashabiki wa African Sports. Wapo.

Waliobaki wote ni ama atakuwa Simba au Yanga. Ndiyo utamaduni wa mpira wetu ulivyo. Misimu miwili kurudi nyuma Rais wa TFF, Wallace Karia ametukanwa sana na baadhi ya mashabiki na wapenzi wa Yanga, huku akituhumiwa kuibeba Simba kwa sababu yeye pia ananasibishwa na klabu hiyo.

Amesemwa sana kuipendelea Simba. Kipindi hicho Simba ilikuwa ya moto kwelikweli. Karia na TFF wamesemwa sana juu ya kuikandamiza Yanga ambayo kimsingi ilikuwa inasajili wachezaji wengi wenye uwezo mdogo. Yanga ilikuwa inaungaunga tu. Haikuwa na mbele wala nyuma. Siku zikapita. Jua likazama. Ufalme wa Simba ukapotea. Baadaye Hersi Said, rais wa Klabu ya Yanga akageuza kibao. Akashusha wanaume sita kutoka DR Congo.

Akamshusha Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Yannick Bangala, Djuma Shaban na Simba la masimba – Dangote, Fiston Mayele. Hatimaye Yanga wakatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo. Kelele juu ya rais wa TFF kuibeba Simba zikaisha. Kelele juu ya TFF kuipendelea Simba zikatoweka.

Baada ya Simba kutwaa ubingwa wa Bara mara nne mfululizo na ikionekana kama watu wanaobebwa zaidi na Karia, walimuuza Luis Miquissone, Clatous Chama, Rally Bwalya na wengine kushuka kiwango. Simba haijawahi kutengemaa tangu kuondoka kwa hao wachezaji.

Baadaye ikaja kuachana na Pascal Wawa, Meddie Kagere, Chris Mugalu na wengine. Simba haijawahi kurudi kwenye ubora wake. Tayari kelele kwa TFF ziliibuka kuwa wanaipendelea Yanga. Tayari Karia alianza kutusiwa kuwa anawabeba Yanga. Ndiyo mpira wetu ulivyo.

Simba walifika mahali mpaka wanatishia kuhama ligi. Simba walitaka kwenda kushiriki ligi ya Zambia kwa sababu wanaona hapa ndani Yanga wanapendelewa. Unahitaji muda sana kuujua mpira wetu. Unahitaji utimamu wa akili kuwaelewa viongozi na mashabiki wa Simba na Yanga.

Wao kila mwenye timu bora anapendelewa na TFF. Wao kila anayekosa ubingwa lawama zote ni kwa rais wa TFF. Hakuna anayekubali kushindwa kwa sababu ya makosa yake. Hakuna anayekubali kupoteza ubingwa kirahisi. Hakuna anayetaka kuwaeleza ukweli mashabiki wake.

Kila mtu anasingizia kuonewa na shirikisho. Kila mtu ananyoosha kidole kwa rais wa TFF. Simba ikifanikiwa zaidi Karia anakuwa ni shabiki wa Simba. Yanga ikifanikiwa zaidi Karia anakuwa ni shabiki wa Yanga. Huu ndiyo mpira wetu na watu wake. Huu ndiyo utamaduni wetu ambao ni lazima uuelewe vizuri. Tangu Yanga wamejua namna ya kusajili wachezaji bora, lawama kwa Karia na TFF zimepungua. Hawapigi sana kelele. Siku hizi wana jeuri ya mpaka kwenda uwanjani wamechomekea.

Tangu Simba wamepoteza ubingwa, ni kama hawaelewielewi. Msimu huu wamefanya bonge la usajili. Kama wakikosa tena ubingwa kelele kwa Karia kuipendelea Yanga haziepukiki. Kama wakishindwa kupata chochote cha kuwapooza mashabiki wao, kuna hatua lawama nzito zitapelekwa tu kwa TFF. Ndiyo timu zetu zilivyo.

Hazijawahi kukubali kushindwa Kwa sababu za kitaalamu. Timu zetu hazijawahi kukubali udhaifu wao. Siku zote zinatafuta kichaka cha kujificha. Baada ya kumrudisha Chama na Miquissone, baada ya kuwaongeza Willy Onana, Fabrice Ngoma na Che Malone, Simba inataka ubingwa.

Simba inataka kupiga hatua kubwa kimataifa. Walau ikifanikiwa eneo moja kelele kwa TFF zitapungua. Ukiwatazama Yanga nawaona wakiwa kwenye moto. Bado wanautaka Ubingwa wa ndani. Bado wanataka historia mpya kimataifa. Ni ngumu wote wawili kila mtu kutimiza malengo yake yote. Ni ama wagawane au mmoja ashinde kila kitu.

Tegemea lawama nyingine nyingi sana mwishoni mwa msimu. Ama za kwenda moja kwa moja kwa Karia au TFF. Timu zetu hazijawahi kukiri udhaifu wao. Wao siku zote wanasaka mchawi nje ya klabu zao.

Yanga ukitazama usajili wao msimu huu wameanzia walipoishia msimu uliopita. Moto ni uleule. Msako unapigwa kwelikweli. Ukitazama usajili wa Simba matumaini ni makubwa sana. Simba imeshusha wanaume wa kazi. Watu wakali kwelikweli. Lazima kitapigwa sana msimu huu. Baada ya mechi tatu za ligi, kila mmoja kaondoka na alama tisa. Sio jambo dogo. Unahitaji kukaza sana.

Ligi yetu inazidi kukua. Timu nyingi zinasajili wachezaji bora na kuwalipa vizuri. Kuna pesa nyingi kwenye mpira wetu. Ushindani unapoongezeka, uteja wa timu nyingi kwa Simba na Yanga unafutika.

Msimu huu kitapigwa kweliKweli. Simba inataka ubingwa. Yanga inataka ubingwa. Lawama kwa Karia na TFF ni suala la muda tu. Yanga waliwahi kutaka kufanya maandamano waende kwa Rais Ikulu kulalamika. Hizi timu hazijawahi kuacha vibweka.

Hizi timu ni mwendo wa kulialia tu zikishachemsha. Nakusubiri kwa hamu kujua kama Karia msimu huu atakuwa shabiki wa Simba au Yanga. Ni suala la muda tu. Timu yotote inayotwaa ubingwa hugeuka timu yake. Timu yoyote inayokosa ubingwa hugeuka kuwa adui. Mpira wetu ukiujua sana haukuumizi kichwa. Una njia zake. Una watu wake.

SOMA NA HII  UBABE WA YANGA WAIHAMISHA GEITA GOLD