Home Habari za michezo MASTAA HAWA WA YANGA WAMCHANGANYA KOCHA WA AL MAREIKH

MASTAA HAWA WA YANGA WAMCHANGANYA KOCHA WA AL MAREIKH

Habari za Yanga

Mastaa wa Yanga wapo kambini wakiwa wamevaa sura ya kazi, akili zikiwa kwenye dakika 90 za mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merreikh, lakini kuna habari itakayomfanya kocha Miguel Gamondi achore ramani vizuri ili kutibua hesabu za Wasudani hao.

Al Merrikh waliopasuka mabao 2-0 katika mechi ya nyumbani ilipoavaana na Yanga kwenye Uwanja wa Kigali Pele (zamani Nyamirambo), jijini Kigali, lakini kumbe benchi la ufundi la timu hiyo lililoondoka na majina ya nyota wa Yanga akiwamo Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI ili kuwasoma.

Kocha wa Al Merrikh, Osama Nabieh aliliambia Mwanaspoti kuwa, wakati wamebakiza siku chache kabla ya kutua nchini kurudiana na Yanga, kwa sasa wanaumiza kichwa ni jinsi gani waje kupindua matokeo ya kipigo cha awali na kwamba hawatapaki basi, ila wamepanga kushambulia na kuwakabili mastaa wa Yanga kibabe.

Nabieh alisema katika maandalizi yao ya mwisho kabla ya kutua nchini kucheza na Yanga wanajipanga kupindua matokeo hayo lakini haoni kama kupaki basi itakuwa ni njia sahihi kwao na kwamba watajiandaa kucheza kwa nidhamu kubwa eneo la ulinzi kutokana na ukali wa mastaa wa Yanga walioweka rekodi Kigali.

Yanga ilikuwa haijawahi kupata ushindi mbele ya Al Merrikh katika michuano ya CAF tangu 1973 na hyata kwenye michuano ya Klabu Bingwa kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup), hivyo ushindi wa Kigali ni wa kwanza na kukaribia kuvunja unyonge wa miaka 25 iliyopita bila kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanya mara ya mwisho mwaka 1998.

Al Merrikh itakutana na Yanga Jumamosi ya Septemba 30 kwenye Uwanja wa Azam Complex ina mlima wa kutakiwa kushinda kwa 3-0 ili ipindue matokeo hayo ya awali, lakini kikwazo ni kasi ya nyota wa Yanga wakiongozwa na Maxi, Pacome, Aziz KI, Clement Mzize na wengineo kitu kinachomchanganya Nabieh.

“Sidhani kama kukaa nyuma itakuwa ni kitu sahihi kwetu, tunahitaji ushindi tukisema tukae nyuma itakuwa ni kama tunaulinda ushindi wa wapinzani wetu, tutakuja na akili ya kutafuta ushindi kwa vile hatuna cha kupoteza,” alisema Nabieh na kuongeza;

“Kitu muhimu kwetu tunatakiwa kuwa makini na kucheza kwa nidhamu kubwa eneo la ulinzi, kwani Yanga ina wachezaji wenye kasi na wajanja, hii ni mechi iliyoshikilia hatma yetu kubaki au kwenda, najua wapinzani wetu wanakuwa bora sana wanapocheza nyumbani lakini huu ni mchezo wa soka lolote linaweza kutokea.”

Kocha huyo raia wa Misri aliongeza endapo vijana wake watafanikiwa kupata bao moja la mapema litakuwa na mchango mkubwa kwao kwa kuwapa presha wapinzani wao.

“Hata wao walipokuja hapa walipopata bao la kwanza lilituchanganya sana na kutupunguza nguvu, nafasi kama hiyo nasisi tunataka kuitumia tunaendelea na maandalizi hayo kujaribu kufanya kitu tofauti.”

Mbinu hizo za Nabieh ni kama mtego kwa Gamondi ambaye amekuwa akitaka kuona anacheza na timu inayoshambulia kuliko zile zinazopaki basi.

Gamondi akiwa mazoezini tayari ameshaanza kukiandaa kikosi chake kukabiliana na mazingira yote magumu akiandaa mfumo wa kusaka mabao mengi kama kawaida yao, lakini akianza hesabu za kuongeza mbinu mbadala wa kusaka mabao wakikutana na timu inayokaa nyuma.

Gamondi amekuwa akianza kujaribu mifumo inayotumia mawinga kutoka pembeni ili kuweza kuufungua uwanja kutokea pembeni ikiwa ni njia ambayo iliwapa matokeo katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Namungo ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuifanya timu hiyo ifikishe mabao 21 katika mechi nane za mashindano, huku Maxi na Aziz KI wakiongoza kwa kufunga mabao manne kila mmoja.

Wachezaji wengine walioifungia Yanga mabao ni Kennedy Musonda na Clement Mzize wenye mabao matatu kila mmoja, Pacome, Hafiz Konkon na Mudathir Yahya wenye mabao mawili kila mmoja, huku mabeki Yao Kouassi na Dickson Job kila mmoja amefunga bao moja moja kwenye mechi hizo nane za mashindano zikiwamo za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, kuonyesha safu ya mbele ya Yanga haitabiriki kujua ni mchezaji gani atatupia kambani, kwani haimtegemei mchezaji mmoja.

SOMA NA HII  BAADA YA MAYELE KUANZA KUTETEMA TENA....GEORGE MPOLE LEO 'KUMTIMULIA VUMBI' KWENYE UFUNGAJI BORA..?