Home Habari za michezo MCHAWI WA SIMBA APATIKANA

MCHAWI WA SIMBA APATIKANA

Tetesi za Usajili Simba

Mashabiki wa Simba na viongozi wakati huu kila mmoja anatafuta mchawi katika kikosi kutokana na kuruhusu mabao manne katika mechi tano ilizocheza.

Simba imecheza mechi mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate uliomalizika kwa suluhu na ikashinda kwa mikwaju ya penalti 4-2 kisha mchezo wa fainali nao ilitoka suluhu na kushinda kwa penalti 3-1 dhidi ya Yanga.

Baada ya hapo Simba ikacheza mechi za Ligi Kuu na kushinda 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar na 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji, huku kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya pili imetoka sare 2-2.

Wadau wengi ni kama vile hawafurahishwi na namna ambavyo mabao hayo yamefungwa katika kikosi cha Simba wakionyesha wazi ni makosa ya mabeki wa pembeni na ukabaji wa macho katika viungo wao.

Kumekuwa na pangua pangua katika eneo la kiungo, muda mwingine anacheza Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma au Ngoma na Sadio Kanoute hali inayoonyesha ni wazi bado Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ hajapata pacha kamili katika eneo hilo.

Kanoute wa sasa sio kama yule wa msimu uliopita na inawezekana ndio sehemu au sababu kubwa ya kuwa na ingia toka katika kikosi hicho na kuleta ugumu kwa Simba.

Ngoma ni mkabaji mzuri lakini anazidiwa ujanja anapokutana na viungo wepesi na kushidndwa kuachia mpira mguuni jambo hilo linamfanya Mzamiru ahahe kwenye kukabana na wapinzani.

Bao la kwanza Simba kuruhusu kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, beki wa kushoto Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alipiga pasi kwa Ngoma ambaye alishindwa kuutuliza mpira vizuri na alipokonywa na Kelvin Nashon ambaye alipiga pasi kwa Matheo Anthony na kufunga.

Tshabalala wakati anatoa pasi hiyo aliendelea kusimama eneo la pembeni ya boksi huku Matheo akipita pembeni yake na aliishia kumkaba kwa macho.

Bao la pili katika mchezo huo huo ilipigwa pasi ndefu na beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Mohamed Kassim na beki wa kushoto Simba, Tshabalala alishindwa kuufikia mpira huo kwa kichwa na alijikuta akiunga tela kumkimbiza Matheo wa Mtibwa Sugar aliyeingia na mpira ndani ya boksi na kufunga.

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Simba iliruhusu bao la kwanza kupitia upande wa kulia baada ya Joshua Mutale kumchambua Shomari Kapombe na kupiga shuti

Bao la pili lililofungwa na Cleofas Mulombwa huku wachezaji wa Simba wakiwa watano halafu wachezaji wa Dyanamos wakiwa wawili tu. Wachezaji watano waliokuwa eneo hilo ni Ngoma na Mzamiru ambao ni viungo wakabaji, mabeki Shomari Kapombe, Che Malone, Tshabalala na Henock Inonga.

Katika bao hilo Kapombe na Mzamiru walikuwa na uwezo wa kumzuia Mulombwa kutofyatua shuti nje ya boksi lakini waliishia kukaba kwa macho.

WASIKIE WADAU

Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema mabeki wa pembeni, Kapombe na Tshabalala wanatakiwa wapumzike kwa sababu wametumika sana. Kigodeko alisema mchezaji hata awe mzuri kiasi gani kuna muda anajikuta anakabia macho kwa sababu anakuwa anashindwa kuendana na kasi inayotokana na kucheza mara kwa mara.

“Sio kwamba wameshuka viwango hilo hapana, bado ni wachezaji wazuri na muhimu kwenye kikosi cha Simba lakini wanahitaji kupumzika ili levo yao iendelee kuwa juu,”alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Zamoyoni Mogela ambaye alisema kuna muda inabidi benchi la ufundi liwapunguzie idadi ya mechi.

“Ifike muda wacheze hata mechi chache kwanza ili warejee kwenye kasi yao, wapewe nafasi wachezaji wengine;

“Sina shida kabisa na kocha kwenye mbinu zake bali ni upande mambo ambayo nimesema hapa wapewe muda wa kutosha kupumzika ili waweze kujipanga upya.” Baadhi ya wadau wanasema Simba inahitaji kiungo wa chini mwenye kiwango bora zaidi.

SOMA NA HII  TUKUTANE KWAMKAPA NDIO KAULI ILIYOBAKIA SIMBA.... HUKU BENCHIKHA AKIBAKIA NA DADIKA 360 PEKEE