Home Habari za michezo GAMONDI: TULIFANYA KOSA HILI IKAWA NI ZAWADI KWA WAPINZANI

GAMONDI: TULIFANYA KOSA HILI IKAWA NI ZAWADI KWA WAPINZANI

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amezungumzia kiufundi mchezo wa juzi waliopoteza kwa magoli 2-1 dhidi ya Ihefu katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023-2024 uliochezwa Uwanja wa Highland Estates, Mbarali, Mbeya.

Gamondi amesema katika soka lazima makosa yatokee ndiyo timu iruhusu kufungwa, hivyo timu ilifanya makosa ya kimchezo.

“Nadhani bao la kwanza tulilofungwa lilikuwa ni makosa yetu na tukawapa zawadi wapinzani.

“Tulijaribu kucheza kutokea nyuma, lakini kwa sababu tulisema uwanja sio mzuri kwa hivyo tuwe na tahadhari kwenye upigaji pasi wetu, halafu tukafanya kosa hilo. Lakini hii ndio soka, makosa yanatokea.

“Katika kipindi cha kwanza tulicheza vizuri sana. Nadhani tungemaliza kipindi cha kwanza kwa bao la kuongoza, ingekuwa mechi tofauti kabisa, lakini kipindi cha pili walicheza kwa kushambulia kwa kushtukiza, tukaruhusu goli la pili.

“Nimesikitishwa sana na matokeo, lakini inaeleweka. Ni mechi nne pekee tumeshacheza, hivyo tunahitaji kufikiria kwa mchezo unaofuata,” alisema Gamondi.

Katika hatua nyingine, Gamondi amezungumzia uchaguzi wa kikosi ambapo alifanya mabadiliko makubwa.

Kuhusu hilo, Gamondi alisema: “Kikosi hakikuwa kibaya, narudia, tuliruhusu goli kwa makosa yetu lakini sio mabadiliko.

“Unajua jinsi mpira wa miguu ulivyo, ikiwa ningeshinda mchezo wangeweza kusema “Yeye ni kocha mkubwa” wangesema hivi, kocha mkubwa kwa sababu kaweza kucheza na kikosi kingine.

“Pengine mashabiki wengi hapa watauliza kwa nini nilifanya mabadiliko, lakini unajua kamwe hatuwezi kumpa kila mtu furaha kwa asilimia mia moja.”

Baada ya mchezo wa juzi, Jumamosi kikosi cha Yanga kitakuwa Mwanza kucheza na Geita Gold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kesho Oktoba 7.

Kuhusu mchezo huo, Gamondi amesema: “Ni lazima tuiweke sawa. Tulikuja hapa tukijua msimu uliopita vilevile Yanga ilipoteza. Sikutaka kupoteza mchezo huu, lakini kwa bahati mbaya tulipoteza.

“Tunahitaji kupambana ili kuendelea kuwa bora na kwa hakika tutarejea Jumamosi ijayo.”

SOMA NA HII  MWISHO WA ENZI....NABI KUTUPIWA VIRAGO YANGA...HOFU YATANDA KUHUSU KUIBUKIA SIMBA...