Home Habari za michezo SAIDO ATANGAZA VITA, AKILI YOTE KWENYE KIATU SASA

SAIDO ATANGAZA VITA, AKILI YOTE KWENYE KIATU SASA

Habari za Simba leo

Baada ya kufunga mabao mawili katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara mfululizo, straika wa Simba, Saido Ntibazonkiza amenogewa kufunga na sasa ameanza kuwaza kiatu cha mfungaji bora mwisho wa msimu.

Staa huyo aliyetambulishwa kwenye Ligi Kuu na klabu ya Yanga, baadaye Geita Gold na sasa Simba, ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita alipopachika mabao 17 akifungana na Fiston Mayele aliyekuwa akiichezea Yanga.

Saido ameliambia Mwanaspoti kwamba mabao mawili aliyofunga dhidi ya Tanzania Prisons timu yake ikishinda 3-1 na Singida Big Stars katika ushindi wa 2-1 yamempa morali ya kupambana zaidi na sasa ameanza kuuwaza ufungaji bora.

“Lengo la kwanza ni kuisaidia timu kufikia malengo na najivunia kufunga. Bado mapema kuzungumzia ufungaji bora, lakini napenda kutetea kiatu changu kwani ni fahari ya kila mshambuliaji kufanya hivyo,” alisema Saido anayeichezea timu ya taifa ya Burundi.

Kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema kikosini kwake kuna idadi ya kutosha ya washambuliaji na anaamini mfungaji bora wa msimu huu atatoka Simba.

“Sio Saido tu, Simba ina washambuliaji wengi na wote wanafanya vizuri. Naamini mfungaji bora msimu huu ana nafasi kubwa ya kutoka kwetu,” alisema Robertinho.

Kwa sasa Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kupisha kalenda ya Fifa baada ya duru ya tano, mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke, ndiye anaongoza kwa kupachika mabao akiwa nayo matano akifuatiwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC mwenye manne kisha Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli wa Yanga na Matheo Antony wa Mtibwa Sugar kila mmoja akiwa na mabao matatu.

SOMA NA HII  KISA MECHI IJAYO NA SIMBA....YANGA WAINGIA MCHECHETO...YALIA WACHEZAJI WAKE KUUMIZWA MAKUSUDI...