SIMBA jana ilizindua jezi mpya za michuano mipya ya African Football League (Super League) ikijiandaa kuvaana na Al Ahly ya Misri, lakini kocha wa timu hiyo Roberto Oliveira ‘Robertinho aking’aka kutokana mastaa wa kikosi cha kwanza akiwamo Kibu Denis, Henock Inonga na Clatous Chama kuitwa timu za taifa.
Wachezaji hao wameitwa kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa za nchi zao kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na kumtibulia programu kocha huyo ambaye mapema aliuomba uongozi wa klabu hiyo kutuma maombi kwa mashirikisho husika ili wabaki klabuni kwao.
Hata hivyo, jambo hilo limeonekana kuwa gumu na kumfanya kocha huyo ang’ake wakati akikuna kichwa jinsi ya kuikabili Al Ahly ambao wenyewe wamezuia wachezaji kujiunga na Timu ya Taifa ya Misri kuonyesha ilivyo siriazi na michuano hiyo mipya itakayozinduliwa Oktoba 20 jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa wachezaji watano wa Simba wa kikosi cha kwanza, hawapo kambini akiwamo beki Inonga aliyepo New Zealand na Timu ya Taifa ya DR Congo, Chama aliyepo Misri na kikosi cha Chipolopolo ya Zambia pamoja na Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Ally Salim walio Taifa Stars inayoenda Saudi Arabia.
Inonga atakuwa sehemu ya DR Congo kitakachocheza mechi ya kirafiki dhidi ya New Zealand, pia wakiwa na mechi nyingine na Angola Oktoba 17, ikiwa ni siku tatu kabla ya Simba kuvaana na Ahly.
Hali iko hivyo pia kwa Chama ambaye jana alitarajiwa kuwa sehemue ya timu ya Zambia kwenye mechi ya kirafiki na wenyeji kisha itacheza tena Zambia dhidi ya Uganda siku ya Oktoba 17, ilihali kina Kibu wao watacheza mechi ya kirafiki kesho dhidi ya Sudan inayochezwa Arabia kisha timu itarejea.
Kocha Robertinho alishtukia mapema mechi hizo kumtibulia programu zake wakati akiwa na pambano gumu na kuuomba uongozi kuyaomba masharikisho ya nchi husika kuwaruhusu wachezaji wa Simba kusalia, jambo ambalo mabosi wa klabu hiyo wamekiri walikuwa wakiendelea kuomba japo ni kama wamechelewa.
“Tuna mazungumzo na mashirikisho ambayo wachezaji wetu wameitwa kwenye timu za taifa. Tumeomba wawape muda warudi kambini mapema lakini hadi sasa (jana), tulikuwa hatujapata jibu la jumla,” alisema Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally. Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Al Ahly kwani iliomba na kuruhusiwa kubaki na wachezaji muhimu walioitwa timu za taifa, ikiwemo kiungo Mmali, Aliou Dieng na mshambuliaji kutoka Afrika Kusini Percy Tau ambao wote kwa sasa wapo kambini wajiweka tayari kuivaa Simba.
Kocha Robertinho alisema alitamani kuwa na wachezaji wote kwenye maandalizi ya mechi hiyo, lakini hana jinsi zaidi ya kuendelea kuwafua waliosalia kujiandaa vilivyo.
“Nilitaka tuwe wote tufanye maandalizi ya pamoja, lakini ndivyo hivyo tena, ila bado naamini katika kikosi chetu, tutaendelea kujiandaa kupitia wachezaji tulionoa kambini,” alisema Robertinho ambaye msimu huu ameiongoza Simba kwenye mechi tisa za mashindano, akishinda saba na kutoa sare mbili.