Kuelekea mchezo wa Michuano mipya ya Africa Football League, Kocha Msaidizi wa AS Vita ya DR Congo, Roul Shungu amwambia Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira Robertinho’ kuwa kama kweli wanahitaji kuwaondoa wapinzani wao Al Ahly ya Misri katika michuano basi wanapaswa kuhakikisha wana uwezo wa kuzuia kufungwa nyumbani na ugenini.
Shungu ametoa kauli hiyo kuelekea katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa michuano hiyo ambao utakuwa ni wa ufunguzi unaotarajia kupigwa kesho Ijumaa (Oktoba 20) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Shungu ambaye aliwahi kufanya kazi katika klabu ya Young Africans amesema kuwa, kama Simba SC imedhamiria kweli kufanya vizuri katika michuano hiyo basi Kocha Robertinho anapaswa kuwaanda wachezaji wake katika mipango ya kupata ushindi mkubwa nyumbani pamoja na njia za kuweza kuzuia wakiwa ugenini kwani wapinzani wao kawaida hawatabiriki.
“Hii ni hatua kubwa kwa Simba SC kuwa katika timu za kwanza katika michuano hii mipya na bahati ambayo wamepata ni kufungua michuano wakiwa kwenye ardhi ya nyumbani niwapongeze katika hilo japo kuwa wana kazi kubwa mbele ya Al Ahly, nafahamu Simba SC siyo wageni kwenye michuano mikubwa lakini hawatokuwa na mchezo rahisi.
“Ni mkweli kwa sababu ukiangalia kiubora bado Ahly ni bora na wamekuwa na uzoefu mkubwa kushinda Simba SC, nadhani kocha wao hapaswi kuangalia rekodi zitamwambia kitu gani kuweza kupata matokeo anachotakiwa kufanya ni kuwa na mkakati wa kuweza kupata ushindi nyumbani na kisha ugenini maana wapinzani wao kawaida huwa hawatabiriki,” amesema Shungu.
Katika hatua nyingine hizi hapa faida za mchezo huo kupigwa Tanzania.
Leo acha tuangazie faida ya African Football League (AFL) kwenye kulitangaza soka la nchi na club ya Simba SC Tanzania uko ulimwenguni ambako ndio ndoto za kila mmoja wetu.
Faida ya ufunguzi wa AFL nchini Tanzania, je, Soka la Tanzania linanufaika vipi?
Tanzania inaenda kujitangaza ulimwenguni kuwa wao wanamiundo mbinu rafiki na wezeshi ya kumudu kuanzisha na kusimamia matukio makubwa ya michezo.
Miundo mbinu hiyo ni viwanja, Hoteli, Usafiri na hali ya usalama wa Afya na Amani na utulivu nchini hivi ni miongoni mwa vitu muhimu katika kuanda matukio makubwa ya michezo Duniani.
Faida kubwa ni kuwa baada ya hapa Tanzania itakuwa imejiweka salama katika uwekezaji na makampuni mengi na tasisi zinaenda kuvutika kuja kuwekeza Tanzania.
Kama mpango wa serikali na Tanzania Football Federation (TFF) utakwenda kwa haraka basi miaka 5-10 ijayo Tanzania inaenda kuwa sehemu ya matukio makubwa ya michezo.
Manufaa kwa Simba SC Wazo na lengo la Simba sc linaenda kukamilika kwa kuwa klabu kubwa Afrika kwa kushiriki mashindano makubwa na vilabu vikubwa Afrika.
Soka la Afrika bado haijaifahamu Simba ila kucheza mashindano makubwa na kupewa nafasi ya ufunguzi na timu kubwa inaenda kuifanya Simba ionekane na kusikika kwa bara la Afrika na Dunia inaenda kuiona Simba.
Kujulikana na kuonekana kwa Simba siku moja tu mchezo wa AFL unaenda kuongeza thamani ya nembo yao kibiashara hivyo kwa miaka ya hivi karibuni Simba inaenda kuwa nembo kati ya nembo 10 zenye thamani kubwa Afrika.
Kama kitengo cha Biashara na masoko cha Simba kitakuwa makini kwenye kuuza Chapa (Brand) ya Simba basi Simba kuanzia Jezi zao,Tv rights and Radio Rights na Social platform zao zinawanufaisha sana.
AFL kwa Tanzania inaenda kuondoa giza kwa wachezaji wetu wa Kitanzania kuuzwa nje ya nchi kwa sababu tayari Dunia ya mpira itakuwa imejua Taifa la Tanzania.
Wachezaji wa Simba wanaenda kuongezeka thamani kwenye soko la micheza (Marketing Value) Simba itakuwa rahisi kununua na kuuza wachezaji katika Soko la mpira kama Simba itakuwa makini na project zake za timu za vijana.