Simba imewasili jijini Cairo nchini Misri tayari kwa mchezo wa kesho wa marudiano ya African Football League dhidi ya Al Ahly lakini kuna mambo mawili ambayo kocha wa timu hiyo, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amewashushia wachezaji wake.
Simba ugenini kesho kusaka ushindi au sare yoyote ya mabao kuanzia 3-3 kusaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na mabingwa hao wa Afrika katika mchezo wa kwanza.
Robertinho alisema kama kuna mabadiliko anayataka kwa wachezaji wake ni kujiandaa kucheza kwa ubora wakati hawana mpira.
Robertinho alisema katika mchezo uliopita walifanya makosa makubwa ya kuruhusu mabao mawili kutokana na changamoto za wachezaji wake wengi kutokuwa bora wakati Ahly wanamiliki mpira wakiwapa nafasi ya kufanya maamuzi.
“Nikweli tulikuwa na hiyo shida na nimeongea nao hii ni mechi ngumu ya ugenini lazima tubadilike eneo hili, tunatakiwa kuwa na ubora mkubwa wa kufanya kazi kubwa wakati hatuna mpira,”alisema Robertinho.
“Tulikuwa tunapoteza mipira kirahisi lakini shida ilikuwa tuna hesabu gani za kuhakikisha tunauirudisha kwa haraka, hili lilitufanya kufanya mabadiliko ya kipindi cha pili.
“Ahly ni timu kubwa tukirudia makosa kama yale yatatuweka kwenye wakati mgumu, tutaendelea kukumbushana kwenye mazoezi ya hapa Misri kabla ya mchezo.
Kocha huyo raia wa Brazil ameongea kuwa mbali na changamoto hiyo pia anahitaji wachezaji wake kuwa na kasi ya kukamilisha mashambulizi yao kwenda lango la wapinzani.
“Tunahitaji kufunga mabao lakini lazima tuwe na kasi ya kuharakisha mashambulizi kwenye lango lao, tunahitajika kuwa na ubora wa kuwafanya wafanye makosa, kama tutakuwa taratibu itakuwa ngumu.”
Wakati Robertinho akiyasema hayo naye beki wake wa kulia Shomari Kapombe amesisitiza akisema wanahitajika kuipa presha safu ya ulinzi ya waarabu hao ambayo inafanya makosa.
Kapombe alisema kama Ahly iliruhusu mabao mawili kwenye mechi zao sita zilizopita kabla ya kukutana nao wao huku pia sare ya mechi yao ikiwa ya kwanza wanaweza kufanya kitu kwa kupata mabao.
-
“Mabao mawili ambayo wameyaruhusu kwenye mchezo mmoja dhidi ya yetu ndio mabao ambayo waliyaruhusu ndani ya mechi zao tisa zilizopita hapa maana yake tunatakiwa kuwa sawa kwenye ushambuliaji kwa kuwa safu yao ya ulinzi inafanya makosa,”alisema Kapombe.