KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amefurahia ushindi wa mabao 2-1 tuliopata dhidi ya Ihefu kutokana na mchezo kuwa mgumu na sasa anaenda kuandaa siraha zake kwa ajili ya Darby.
Robertinho alisema ratiba imekuwa ngumu sababu tunapata muda mfupi wa kujiandaa kabla ya mechi kutokana na ratiba kubana lakini kikubwa pointi tatu zimepatikana.
Alisema mchezo wa leo (jana) ilibidi kuwapumzisha baadhi ya nyota akiwemo Kibu Denis na Jean Baleke katika dakika 45 ili kuwandaa kwa ajili ya mchezo unaofuata wa Derby.
“Ratiba ni ngumu, tumetoka kushiriki michuano mikubwa ya African Football League (AFL) na tumefanya mazoezi siku mbili kabla ya leo kushuka uwanjani.
Ndio maana nawapongeza wachezaji wangu, haikuwa kazi rahisi lakini kikubwa tumepata pointi tatu muhimu nyumbani,” alisema Robertinho.
Aliongeza kuwa anahitaji kuona timu yake inacheza vizuri pamoja na kushinda ili kuendelea kwenye nafasi nzuri ya mbio za kuwania ubingwa wa Ligi hiyo.
Robertinho alisema baada ya kukamilika kwa dakika 90 na Ihefu FC, sasa wanajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Yanga, kihakikisha wanapata matokeo mazuri ambayo yatawasaidia kufikia malengo yao mwisho wa msimu.
Naye kocha wa Ihefu FC, Mosses Basena alisema mechi ilikuwa ngumu na wameadhibiwa kulingana na makosa waliyoyafanya kwa Simba kuibuka na ushindi.
“Tumefanya makosa na Simba wakayatumia kupata ushundi, narudi uwanja wa mazoezi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi hiyo na kujuandaa na mechi iliyopo mbele yetu,” alisema Basena.