Meneja wa Simba SC, Ahmed Ally amesema anawashukuru Ihefu FC kwa kuwafunga Yanga SC kwani wamewarahishia kazi na wao wanakwenda kuimaliza Jumapili katika dabi ya Kariakoo.
Ahmed ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2023 kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo mkubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati.
“Ni mechi ambayo tunakwenda kuendeleza ubabe kwa watani zetu. Ili tujiridhishe kwamba msimu huu tutafanya vizuri ni kupata ushindi katika mchezo huo. Tunataka tuchukue ubingwa mapema sana, katika hili tunawashukuru Ihefu kwa kutusaidia kazi na sisi tunataka kuendeleza kuweka tofauti ya alama na Yanga SC.”- Ahmed Ally.
Wakati huohuo,Kelele za kwamba timu haichezi vizuri huwenda zikawa hazina maana kama tu, mashabiki wataingalia timu yao kwa jicho la takwimu kwani mpaka sasa, Simba ina un beaten 29 katika mechi za Ligi Kuu ya NBC.
Hii inatokana, tangu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ atue Msimbazi katika dirisha dogo la usajili mapema mwaka huu, hajapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu.
Juzi alipocheza mchezo wake wa raundi ya saba dhidi ya Ihefu, ndipo alipofikisha un beaten hiyo na Jumapili hii anakwenda kucheza dabi yake na Yanga SC mchezo wa raundi ya nane akiwa na alama zake 18 sawa na Yanga anayeongoza Ligi.
Hata hivyo, Simba anacho kiporo kimoja mkononi cha mchezo wa raundi ya sita dhidi ya Mashujaa.