Home Habari za michezo IHEFU KUITIBULIA TENA YANGA…MIPANGO YAO LAZIMA KINA SKUDU ‘WAOMBE POO’…

IHEFU KUITIBULIA TENA YANGA…MIPANGO YAO LAZIMA KINA SKUDU ‘WAOMBE POO’…

Habari za Michezo

Ihefu imeangalia kwa umakini kasi ya ushambuliaji ya Yanga na uimara wa beki wao na kutikisa kichwa ikisema wanajua pakuwabana kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa Ligi Kuu, huku vigogo wa Yanga Mbeya wakishtukia kitu.

Timu hizo zinatarajia kukutana katika mchezo huo Oktoba 4, ambapo rekodi inaonesha mara ya mwisho kuvaana katika Uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali, Ihefu walishinda 2-1 na kumaliza ubabe wa Yanga wa kutofungwa michezo 49.

Hata hivyo, katika mechi tano ikiwamo ya kombe la shirikisho (ASFC) walizokutana timu hizo, Yanga wameshinda nne wakifunga mabao 11, wakifungwa moja na kupoteza moja.

Hadi sasa Yanga ndio wanaongoza msimamo kwa pointi tisa, huku wakiwa wametupia mabao 11 wavuni wakiwa hawajafungwa bao lolote, huku Ihefu wakiwa nafasi ya tisa kwa pointi tatu, wakifungwa mabao matatu na kufunga moja. Kocha mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila alisema wameiona Yanga katika mechi zake, akikiri kuwa mchezo wao utakuwa mgumu lakini akieleza kuwa wamejipanga kuwabana kubaki na pointi tatu.

Alisema maandalizi waliyofanya tangu walipomaliza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mashujaa Septemba 16 na kupoteza kwa 2-0, wamefanyia marekebisho makosa yao na sasa kazi imebaki kuwamaliza Yanga.

“Tumekuwa na maandalizi mazuri na tumewaona Yanga, kimsingi ni kudhibiti mashambulizi kucheza mtu na mtu, makosa yaliyoonekana katika mechi iliyopita tumeyarekebisha”

“Lazima tutumie madhaifu yao tuliyoyaona kuweza kushinda mchezo huo na kujiweka pazuri, sisi tunahitaji kujinasua nafasi za chini na kupanda juu, vijana wana ari na morali kufikia malengo,” alisema Katwila.

Kwa upande wake katibu wa Yanga mkoani Mbeya, Rajabu Mrisho alisema msimu uliopita walifanya makosa ambayo msimu huu hawatarajii kuyarudia tena na kwamba lazima Ihefu apigwe.

Alisema wakati wa mapokezi ya timu hiyo mkoani Mbeya hawatakuwa na shamrashamra zozote isipokuwa watafanya zoezi hilo kimkakati sana ili kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

“Tulikosea msimu uliopita ila hatutarajii kurudia makosa, tutaipokea timu kimkakati bila matarumbeta na njia iliyotumika tutabadili na kuona wapi tupite ili tushinde mchezo huo muhimu na kulipa kisasi,” alisema Mrisho.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA MBRAZILI KUSEPA...MGUNDA ASHUSHA PRESHA SIMBA...