Home Habari za michezo SIMBA WAKIINGIA NA ‘PLAN’ HIZI MBELE YA AL AHLY…..MECHI INAISHIA HAPA HAPA...

SIMBA WAKIINGIA NA ‘PLAN’ HIZI MBELE YA AL AHLY…..MECHI INAISHIA HAPA HAPA BONGO…

Habari za Simba SC

MECHI inayosubiriwa kwa hamu kubwa kwa sasa hapa nchini na Afrika kwa ujumla ni kati ya Simba na Al Ahly inayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Ijumaa.

Huo ni mchezo wa ufunguzi wa African Super League yakiwa ni mashindano mapya.

Maneno yamekuwa mengi kuhusu mchezo huo kutokana na ubora wa Al Ahly, lakini inaonekana kuwa kama Simba wakiweza kutegua mitego vizuri wanawapasua mabingwa hao wa Afrika kwenye mchezo huo.

Kipa

Al Ahly kwenye michezo yao yote mikubwa wamekuwa wakimtumia kipa Mohamed El Shenawy, ambaye amekuwa na ubora mkubwa, lakini akiwa na udhaifu kwenye mipira ya mbali.

Kipa huyo amekuwa akifungwa mabao mengi kwenye mashuti ya nje ya 18 hasa yakiwa yanapigwa juu.

Kumbuka bao ambalo Al Ahly walifungwa na Simba ambalo alifunga Luis Misquissone Februari 2023 lilikuwa shuti la nje ya 18.

Mchezo huo Simba walionekana kuwa na mpango wa kupiga mashuti, ingawa hawakuyapangilia vizuri na kupoteza nafasi nyingi.

Udhaifu huo pia ulionyesha kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ambao timu yake ililala kwa mabao 5-2, mawili yote yalikuwa ya nje ya 18, moja lilipigwa juu na lingine chini lakini kumbuka amefungwa mabao ya namna hiyo mara nyingi. Kama Simba wakitumia udhaifu huo kwa kupiga kutoka mbali wakiwatumia wapigaji wazuri kama Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama na Kibu Denis wanaweza kufunga mabao.

Spidi

Aina ya kucheza ya Al Ahly siyo ya kasi na wamekuwa wakikutana na wakati ngumu wanapocheza na timu zenye kasi mfano mchezo dhidi ya Wydad Casablanca na ule wa Mamelodi na hata mchezo wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Wachezaji wake wengi wamekuwa wakicheza taratibu, lakini kwa uhakika zaidi, hivyo mara nyingi hawapendi kukutana na timu ambayo ina mawinga wanaokimbia sana.

Mchezo huo unaweza kuwa muhimu kwa washambuliaji kama Kibu ambaye ana uwezo mkubwa wa kukimbia na kutumia nguvu.

Upande wake atakuwa akipambana na beki wa kushoto wa Ahly, Ali Maâloul ambaye ana uzoefu mkubwa kwenye soka, lakini amekuwa akishindwa kupambana na wachezaji wenye kasi na nguvu kama alivyo Kibu, labda kutokana na kutumika muda mrefu pamoja na umri wake wa miaka 33 kwa sasa.

Mabeki wa pembeni

Ahly wana mabeki bora wa pembeni, aina yao ya kucheza haina tofauti sana na hawa wa Simba kwa sasa, Mohammed Hussein na Shomary Kapombe kwa kuwa wote wana uwezo mkubwa wa kushambulia zaidi kuliko kukaba. Sehemu hizi Simba wanatakiwa kuwa na mkakati maalumu zaidi upande anaocheza Tshabalala kwa kuwa mabao mengi ya Ahly yametengenezwa kupitia huko anakocheza Mohammed Hanny anayeshirikiana vyema na Pecy Tau ambaye ndiye staa wa Ahly.

Katika upande huo Simba wanatakiwa kuwa na jambo moja, Tshabalala asipande sana au winga anayecheza juu yake awe na uwezo mkubwa wa kurudi kusaidia kwenye eneo la ulinzi kama ambavyo amekuwa akifanya Kibu upande wake.

Faulo, kona

Moja ya jambo ambalo Simba wanatakiwa kuliepuka ni kuwapa nafasi Ahly ya kupiga mipira mingi ya adhabu kwenye eneo la nje ya 18 au kuwapa nafasi ya kupiga kona nyingi, mara nyingi wamekuwa bora kwenye mipira hiyo jambo ambalo wanatakiwa kufanya ni kuwa na wachezaji wengi warefu wanaoweza kupambana na wale wa Ahly ambao wengi wao ni warefu na hivyo wamekuwa wakifanikiwa kuwa wa kwanza kugusa mipira.

Mechi hiyo inawafaa wachezaji kama John Bocco ambao wanaweza kusaidia kuokoa mipira ya juu na pia kusaidia Simba kufunga kwenye mipira hiyo kwa kuwa Al Ahly nao wameonekana kusumbuka zaidi kuzuia mipira ya juu langoni kwao.

Aishi Manula

Kama Manula atakuwa fiti angalau kwa asilimia 80, huu ni mchezo ambao anahitajika zaidi kuliko mingine ijayo. Uzoefu wake wa kukutana na mikimiki ya mechi kubwa kama hizi unatosha kuisaidia Simba kuliko kumuweka kipa mwingine yeyote ambaye yupo kwenye kikosi cha Simba.

Viungo

Mara nyingi kocha wa Simba, Robert Olivier ‘Robertinho’ amekuwa akitumia viungo wawili wa kukaba anacheza mfumo wa 4.2.3.1. Mfumo huu ndiyo umekuwa ukitumiwa na Ahly kwenye michezo ya msimu huu. Kutokana na viwango tofauti vya timu hizo, ni sahihi kama Robertinho atabadili mfumo wake na kuongeza kiungo mwingine wa kukaba ili kuwanyima uhuru viungo wa Ahly.

Mashabiki

Nguzo kubwa ya Al Ahly ikiwa kwao ni uwepo wa wingi wa mashabiki wanaoshangilia. Hii wamekuwa wakiitumia kama silaha kubwa, hivyo hata michezo ambayo Simba walifanikiwa kushinda hapa nchini walikuwa na nguzo kubwa ya mashabiki. Katika mchezo huu wanaweza kuwa na faida kubwa kama watajaa uwanjani na kushangilia kwa nguvu kubwa kwa Mkapa.

Wadau

Akizungumzia mchezo huo, George Masatu, mchezaji wa zamani wa Simba anasema ili ipate matokeo mazuri katika mchezo huo wachezaji wote watakaoaminiwa kucheza akili zao ziwe ndani ya dakika 90.

Alisema wanatakiwa kuwa na utimamu na kufuata maelekezo ya kocha ambayo atawapa kabla na ndani ya mchezo.

“Wachezaji wachukue plan A ya mwalimu ikishindikana watumie plan B ambayo ni yao wenyewe kila mchezaji ili wajitoe waweze kushinda mechi,”alisema mchezaji huyo.

Masatu alisema kila mchezaji ajitahidi kumdhibiti yule mwenye mpira na waache mambo ya kuambiana mkabe yule itawafanya washindwe kufurukuta.

Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Juma Pondamali alisema jambo kubwa ambalo Simba inatakiwa kuwa nalo makini ni upande wa safu ya ulinzi huku akiwataka pia kuhakikisha hawaruhusu bao lolote.

“Kwanza lazima waiheshimu Al Ahly kuwa ni timu kubwa licha ya kwamba hata wao Simba ni wakubwa. Pia lazima waingie uwanjani kwa heshima na kuhakikisha kuwa hawaruhusu goli lolote ili wasipate presha kubwa katika mechi ya marudiano,” alisema Pondamali.

“Jambo muhimu ni safu yao ya ulinzi kupunguza makosa ya mara kwa mara kama wanavyofanya kwenye ligi. Mabeki wa Simba wanaruhusu sana wapinzani kupita kati na wanashindwa kujua kuwa ukimruhusu mpinzani kupita katikati analiona goli lote hivyo akipiga shuti ni rahisi kukufunga, ni afadhali wapitie pembeni inakuwa rahisi kuwadhibiti.

“Kocha Robertinho anatakiwa kuanzisha wachezaji wote mahiri katika kikosi cha kwanza ili wampe matokeo na sio kuanza na wachezaji wa majaribio kwani hiyo sio mechi ya kujaribu, wale kina Baleke (Jean) wote wanatakiwa kuanza,

Kocha wa zamani wa Alliance, Kessy Mziray alisema ili Simba iweze kutoboa siku hiyo wachezaji wake wanatakiwa kuongeza uwajibika zaidi ya walivyofanya katika michezo iliyopita.

Alisema kwamba ana imani kubwa na kocha mkuu kuwa ni mzuri katika michezo ya mashindano, lakini shida ni kwa wachezaji wake kushindwa kukitumia walichonacho.

“Simba ina timu nzuri sana. Naamini wakijiamini na kuwaheshimu wapinzani watawashangaza wengi, japokuwa kwa sasa ile falsafa yao ya nyuma na mpira waliokuwa wakiucheza imebadilika ni jambo la kawaida kutokana na mabadiliko ya kikosi hicho,” alisema Mziray.

CREDIT- MWANASPOTI

SOMA NA HII  JINSI 'PAPARA' ZA KIBU DENIS ZILIVYOINYIMA SIMBA MAGOLI TISA KILAINI...MATOLA ASHINDWA KUJIZUIA....