Home Habari za michezo HIZI HAPA DAKIKA ZA KUFA KUPONA KWA SIMBA NA YANGA CAF….WAKISHINDWA NDIO...

HIZI HAPA DAKIKA ZA KUFA KUPONA KWA SIMBA NA YANGA CAF….WAKISHINDWA NDIO BASI TENA…

Habari za Michezo

Mechi mbili zijazo ambazo zitachezwa ndani ya muda usiozidi siku saba kwa Yanga na Simba zimeshikilia hatima ya ndoto ya timu hizo kumaliza katika nafasi mbili za juu katika makundi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambazo zitafanya zifuzu kusonga mbele katika hatua ya robo fainali.

Matokeo ya mechi za kwanza kwa kila moja kwenye kundi lake, yanazilazimisha Simba na Yanga kuchanga vyema karata zao katika mechi hizo mbili zinazofuata ili ziweke hai matumaini ya kufuzu robo fainali vinginevyo zitaweka rehani uwezekano huo.

Kwa Yanga ambayo ilianza kwa kupoteza ugenini kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, ndani ya siku saba zijazo itakabiliana na Al Ahly nyumbani, Jumamosi, Desemba 2 na baada ya hapo siku sita baadaye itakuwa na mechi ya ugenini dhidi ya Medeama ya Ghana, Desemba 8.

Ushindi katika mechi hizo mbili hasa dhidi ya Al Ahly utakuwa na umuhimu mkubwa kwa Yanga kwani kinyume na hapo italazimika kupata ushindi katika mechi zote tatu za mwisho kwenye kundi lake mojawapo ikiwa ya ugenini ili iweze kusonga mbele.

Kupoteza dhidi ya Al Ahly kutaifanya Yanga icheze mechi mbili mfululizo dhidi ya Medeama ambazo zitafuata ikiwa imetanguliwa kwa pointi sita na ugumu wa mechi hizo utaongezeka kwa matokeo ya aina yoyote ambayo Medeama itayapata dhidi ya CR Belouizdad katika mechi inayofuata.

Kama Medeama itapata ushindi mbele ya CR Belouizdad maana yake itaikabili Yanga ikiwa inafahamu kwamba ushindi katika mechi mbili dhidi yao utaifanya iwe na pointi tisa na kukaribia kufuzu lakini ikiwa itapoteza, michezo dhidi ya timu hiyo inayoiwakilisha Tanzania ndio itakuwa ya kujiokoa au kuaga mashindano hayo kutegemeana na matokeo yatakayopatikana.

Ni kama ilivyo kwa Simba ambayo katika mechi yake ya kwanza nyumbani ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani ambayo mazingira yanailazimisha kutopoteza mechi mbili zinazofuata za kundi C dhidi ya Jwaneng Galaxy na Wydad.

Mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy ambao utachezwa Desemba 2 huko Gaborone, Botswana, ni wa muhimu kwa Simba kupata ushindi ili kwanza iisimamishe timu hiyo ambayo ilianza vyema hatua ya makundi kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca lakini pia unaweza kuifanya Simba iongoze kundi kutegemeana na matokeo ya mchezo baina ya Asec Mimosas na Wydad Casablanca.

Kutakuwa na ugumu zaidi kwa Simba ikiwa itapoteza au kutoka sare katika mechi hiyo dhidi ya Jwaneng kwani baada ya hapo itakabiliana na Wydad Casablanca, Desemba 9 ambayo kama itaifunga Asec Mimosas katika mechi inayofuata maana yake dhidi ya Simba itakuwa inasaka pointi sita za kulainisha safari yao ya kusaka robo fainali lakini kama ikipoteza, itakabili mwakilishi huyo wa Tanzania kwa hesabu za kujifufua.

Hii sio mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kuanza vibaya hatua ya makundi lakini baadaye zikapindua meza na kufika hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika.

Msimu uliopita, Simba ilipoteza mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya na Raja Casablanca lakini ikapata ushindi katika mechi tatu mfululizo zilizofuata dhidi ya Vipers na Horoya na kukata tiketi ya kutinga robo fainali, hatua ambayo ilitolewa na Wydad.

Yanga katika msimu huo uliopita, ilianza kwa kupoteza mechi ya kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Monastir ugenini lakina ikaja kupata ushindi katika mechi nne nne kati ya tano zilizofuata na kufika hadi hatua ya fainali.

Aliyekuwa anakaimu nafasi ya Kocha wa Simba, Daniel Cadena alisema kuwa watapambana kuhakikisha wanapata ushindi ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy.

“Tunaenda kucheza dhidi ya timu ambayo imepata ushindi kwenye mechi ya kwanza tena ugenini hivyo tunafahamu tunakabiliwa na mechi ngumu lakini huu ni wakati wa kuonyesha kwamba Simba ni timu kubwa Afrika. Tunawaandaa vyema wachezaji wetu kwa ajili ya mechi hiyo na tunaamini tutafanya vyema alisema Cadena.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema mechi dhidi ya Al Ahly umeshikilia hatima yao.

“Huu ndio mchezo muhimu zaidi na tunaotakiwa kupata ushindi ili kuweka vizuri hesabu zetu za kusonga mbele. Tunahitajika kupata ushindi hapa dhidi ya l Ahly na wachezaji wangu nina imani watapambana kuhakikisha tunapata ushindi. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutusapoti,” alisema Gamondi

SOMA NA HII  ALIYEHUSIKA SIMBA KUFA 5-0 ARUDI KIVINGINE.....SAFARI HII KASOGEA KABISA MLANGONI...