Home Habari za michezo ENG HERSI CHUKUA STRAIKA LA MAGOLI HILI…PIGA CHINI KONKON

ENG HERSI CHUKUA STRAIKA LA MAGOLI HILI…PIGA CHINI KONKON

Habari za Yanga

GOR Mahia ya Kenya inatamba na kijana mdogo mwenye umri wa miaka 21, Benson Omalla ambaye yupo katika kiwango cha juu cha uchezaji huku akiwa kinara katika kutupia mabao nyavuni kwenye mashjindano hayo.

Bwa’mdogo huyo hadi sasa ameshafunga mabao 23 kwenye mechi 26 za Ligi Kuu ya Kenya maarufu kama FKF-PL huku timu yake ikiongoza msimamo na pointi 56, ikifunga mabao 40 na kwa hesabu za haraka haraka ni kama amefunga zaidi ya nusu ya mabao ya timu hiyo ambayo ni maarufu kama KOgalo.

Omalla ni zao la mashindano ya shule yanayofahamika nchini humo kama Chapa Dimba na Safaricom kama ilivyo Umiseta hapa Tanzania, na wakati akichipuki alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu 2019 alipokuwa akisoma Kisumu Day High School, kisha alisajiliwa na timu ya Ligi Kuu ya Western Stima.

Akiwa hapo, alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu, Desemba 2019. Mwaka 2020 alitakiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, lakini serikali ikafuta mitihani hiyo kwa sababu ya mlipuko wa Uviko-19.

Nyota huyo alimaliza msimu akiwa na mabao sita katika Ligi Kuu ya Kenya katika umri wa miaka 16. Mwaka 2020 alisajiliwa na miamba ya Nairobi, Gor Mahia akiwa na miaka 17.

Katika msimu wake wa kwanza na Gor 2020/21, hakupata nafasi ya kuonyesha makali yake na alianza kucheza 2021/22, akafunga mabao 10 kwenye mechi 15 alizobahatika kukipiga.

Omalla alienda Sweden kucheza soka la kulipwa, lakini alikaa miezi miwili tu akarudi Kenya na huu ukiwa ni msimu wa nne kwake ndiyo anaofanya mabalaa katika ligi ya Kenya.

KAMA LUNYAMILA

Mwaka 1991 kwenye Umiseta iliyofanyika Zanzibar, kulikuwa na mtoto mmoja fulani kutoka Kanda ya Ziwa aliyeitwa Edibily Lunyamila. Kumbuka enzi hizo hazikuwa zama za TV na hazikuwa za mitandao ya kijamii wala hazikuwa simu za mikononi.

Kipindi cha michezo kilikuwa kimoja tu redioni saa mbili kasorobo usiku kupitia redio moja pekee – RTD na kilikuwa cha robo saa.

Pata picha habari za michezo za kutwa nzima ziliripotiwa na redio moja tu nchi nzima, halafu kwa robo saa. Hapo unategemea stori gani zitatawala?

Lakini kwa mwaka huo ilikuwa tofauti. Habari za Umiseta ziliripotiwa kutoka Zanzibar na mtangazaji akiwa Yusuf Omary Chunda na jina la Lunyamila ndilo lililotawala sana enzi hizo akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Buhangija, mjini Shinyanga.

Lunyamila alienda Zanzibar kwenye Umiseta akiwa na timu ya Kanda ya Ziwa na baada ya mashindano hayo alisajiliwa na Biashara Shinyanga, timu iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza ambalo ndilo sawa na Ligi Kuu kwa sasa.

Akiwa na Biashara Shinyanga, Lunyamila aling’ara sana kiasi cha kuitwa kuichezea timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na siku anamalizia mtihani wa mwisho wa kidato cha nne 1992, gari aina ya SHANGINGI lilikuwa nje ya darasa linamsubiri kumpeleka Dar es Salaam akaungane na timu ya taifa.

Mechi yake ya kwanza kuichezea Taifa Stars ilikuwa dhidi ya Liberia mjini Monrovia, Agosti 30, 1992, nahodha wa Liberia alikuwa George Weah ambaye wakati huo alikuwa akiitumikia PSG.

Lunyamila aliibukia kwenye mashindano ya shule na Omalla ni vivyo hivyo. Lunyamila alisajiliwa na timu ya Ligi Kuu akiwa kidato cha tatu na Omalla ni vivyo hivyo. Lunymamila alienda Ulaya na hakukaa sana akarudi nyumbani na Omalla ni hivyo.

Tofauti pekee ya Lunyamila na Omalla ni yeye alikuwa winga na Omalla ni mshambuliaji wa kati. Ukitaka kumpata Benson Omalla hili hapa ni dau lake.

Fedha ya kusaini mkataba ni Dola 100,000 za Marekani sawa na shilingi milioni 230 na anataka mkataba usiopungua miaka miwili.
Gor Mahia inataka Dola 200,000 sawa na shilingi milioni 460, kama ada ya uhamisho na mshahara anaoutaka Dola 6,000 sawa na milioni 13 kwa mwezi na wakala wake anataka ada ya uwakala ya Dola 20,000 shilingi milioni 46,000.

Jumla, Omalla ana gharama ya Dola 564,000 za Marekani sawa na shilingi bilioni 1.3. Timu yoyote Tanzania inayomtaka hilo ndilo dau lake.

Benson Omalla msimu huu (23/24):
◉ Mechi ligi kuu — 7
◉ Mabao scored — 7
◉ Assists — 2

Benson Omalla msimu uliopita (22/23) :

◉ Mechi ligi kuu — 27
◉ Mabao scored — 26
◉ Assists — 4

SOMA NA HII  FT:- KMC 0-3 YANGA SC...MUDATHIR KAMA KAWA...'MAJINI' YAMKUMBA GUEDE....