Home Habari za michezo UJIO WA KOCHA MPYA SIMBA,ULIVYOWASAHAULISHA WANAMSIMBAZI MIAKA 30 YA SIMANZI

UJIO WA KOCHA MPYA SIMBA,ULIVYOWASAHAULISHA WANAMSIMBAZI MIAKA 30 YA SIMANZI

Habari za Simba

Inawezekana wengi wenu hii imewapita. Sio kwa sababu hamjui, ila ni kutokana na kuwa bize na ujio wa Kocha Mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha na wasaidizi wake wawili, sambamba na uwepo wa maandalizi ya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu.

Ndio jana Simba ilikuwa ugenini kuvaana na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye mchezo wa Kundi B, ilihali watani wao, Yanga walikuwa nyumbani Kwa Mkapa kuikaribisha Al Ahly katika mechi ya Kundi D.

Mechi hizo zimepigwa wakati timu hizo zikitoka kupata matokeo yasiyovutia ya raundi ya kwanza, Yanga ikilala mabao 3-0 ugenini huko Algeria mbele ya CR Belouizdad, huku Simba ikilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Sasa kama hamjui ni Novemba 27, yaani juzi kati tu ilikuwa ni mwaka wa 30 kamili kwa tukio la Simba kucheza fainali ya kwanza ya CAF mwaka 1993.

Simba ilicheza fainali ya Kombe la CAF lililoanzishwa mwaka 1992 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast na kuipoteza kwa jumla ya mabao 2-0. Ilianza kwa suluhu ugenini Novemba 14, 1993 na kurudiana Novemba 27 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na Simba kulala 2-0.

Ukihesabu, tangu kipindi hicho hadi hivyo Novemba 27 ya mwaka huu ilikuwa ni miaka 30 imepita tangu Wekundu kuandika historia iliyokuja kufikiwa na Yanga msimu uliopita kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (michuano iliyounganishwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi, mwaka 2004).

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Simba iliingia kwenye michuano hiyo mwaka huo wa 1993 ikitoka kupoteza taji la michuano ya Kombe la Kagame 1993 iliyofanyikia Kampala, Uganda.

Simba ndio iliyokuwa watetezi wa taji hilo, ikitwaa mwaka 1992 lakini ikaenda kulitema kwa watani wao, Yanga iliyotwaa kwa kuifunga SC Villa ya Uganda.

Kwenye mechi hizo za Kombe la CAF, Simba ilianza kichovu kwa kuvaana na Ferreviario de Maputo ya Msumbiji kwa kutoka suluhu nyumbani.

Mashabiki wengi waliikatia tamaa kwa kuamini inaenda kutolewa ugenini, lakini kama zali Simba ilipata sare ya 1-1 mjini Machava na kuvuka raundi ya pili kwa faida ya bao la ugenini na kupangwa kukutana na Manzini Wanderers ya Swaziland (sasa Eswatini).

Kwenye mchezo wa kwazna Simba ilishinda nyumbani na ugenini kwa bao 1-0 kila mechi na kuvuka robo fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0. Bao la mechi ya nyumbani liliwekwa kimiani na Malota Soma ‘Ball Juggler’ sekunde chache kabla ya mapumziko.

YAKUTANA NA WAALGERIA

Kutinga kwao robo fainali kuliifanya Simba kukutana uso kwa uso na Al Harrach ya Algeria na kuwatia hofu mashabiki wa klabu hiyo wakiamini huenda mambo yakaishia hapo, lakini Mnyama akapeta.

Simba iliing’oa, Al Harrach kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2, kwani ilishinda nyumbani 3-0 kupitia Edward Chumila ‘Edo’ aliyefunga mawili na jingine Abdul Ramadhan ‘Mashine’, lakin i ilipoenda ugenini kurudiana na Waalgeria hao, Mnyama alichezea 2-0 na kufanikiwa kuvuka salama kwenda nusu fainali.

WAANGOLA HAWAKUAMINI

Simba kwenye hatua ya nusu fainali ilipangiwa Atletico Sportive Aviacao ambao waliizuia Gor Mahia kwenye hatua ya robo fainali kwa kuifumua mabao 4-2 na kuwafanya Wanamsimbazi kuwa na presha kubwa hasa kutokana na kipa wa timu Kanka Vemba aliyekuwa mahiri enzi zake.

Hata hivyo, Simba ikiwa uwanja wa nyumbani iliishindilia Aviacao kwa mabao 3-1 na kuifuata Angola ikiwa na matumaini makubwa, japo Waangola waliwachimba mkwara kule wasingetoka salama kama walivyowang’oa Wakenya kwa penalti 4-2 Kanka Vemba akiwa ndiye nyota kwa kudaka penalti za Gor.

Hata hivyo, Simba ilimaliza kazi mapema dhidi ya ASA na kipa wao huyo kwa kupata ushindi huo wa 3-1 nyumbani yaliyofungwa na Chumila tena aliyetupia mawili, huku jingine lililokuwa la pili Waangola wakijifunga, huku bao lao la kufutia machozi likifungwa na Nello.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida na iliyoleta utata ni kwamba Simba ilipoenda Angola baada ya miaka mingi sana mvua ilinyesha.

Na mchezo huo, uliisha kwa sare tasa 0-0, huku Waangola wakishindwa kuamini kilichoikuta timu yao na kuamua kufanya fujo za kumrushia chupa na vitu vingine kipa Mohammed Mwameja ili kumzingua kwani ndiye waliyemuona kikwazo kwao tangu Dar.

FAINALI SASA

Baada ya Simba kufanikiwa kuingia hatua ya fainali kwa kuwatoa Waangola hao moja kwa moja ilivyorudi Tanzania wakaingia kambini visiwani Zanzibar

Mfanyabiashara, Naushad Mohammed alihusika kwa kiasi kikubwa kuipa Simba msaada wa hali na mali.

Kuelekea mchezo huo wa ugenini, Simba ilikumbwa na majeruhi, mshambuliaji wake Edward Chumila ‘Smile Killer’ alikuwa na tatizo la nyama pamoja na beki wake wa kushoto Deo Mkuki waliukosa mchezo huo muhimu mno kwao.

Kocha Abdallah Kibadeni akisaidiana na Etenne Eshette alilazimika kumtumia mshambuliaji David Mihambo kuchukua nafasi ya Chumila, huku Twaha Hamidu alicheza beki wa kushoto kuziba pengo la Deo Mkuki.

Simba ilicheza vizuri sana na kuibana Stella Abidjan kama sio kukosa umakini kwa Mihambo na Feruz Teru ingeshinda mchezo huo ugenini na kujitengenezea mazingira mazuri katika mchezo wa nyumbani, lakini hadi dakika 90 zilipomalizika matokeo ya timu hizo ilikuwa ni suluhu.

VURUGU ZA VIONGOZI

Hapo sasa ndipo mambo yalipoonza kwani baada ya Simba kurudi tu, viongozi, wanachama na baadhi ya viongozi wa serikali wakaona kama vile kazi ilikuwa imekwisha akili zote zikaelekezwa kwenye maandalizi ya jinsi ya kulitembeza kombe.

Kambi ya Simba pale Zanzibar ilikuwa bize kila siku viongozi wa serikali walitembelea huku kila mmoja akitoa ahadi lengo ni kuwahamasisha wachezaji wafanye vizuri.

Movemba 27, siku ya mchezo uwanja ulifurika watu na viingilio vilikuwa Tsh 50,000 sehemu maalumu, Tsh10, 000 jukwaa kuu, Tsh5,000 jukwaa la kijani, Tsh1,500 mzunguko

Baada ya mchezo kuanza huku Watanzania wakiwa na matumaini makubwa ya kuona Simba kushinda mchezo huo ilishtushwa na bao la mapema lililofungwa na mchezaji Koume Disire katika dakika ya 17 tu ya mchezo huo.

Uwanja ulikuwa kimyaa (hapa hata wale mashabiki wa Yanga nao walificha makucha yao kwanza ) bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili, Simba ilitafuta bao la kusawazisha bila mafanikio, huku mara kadhaa mshambuliaji wake Damian Kimti akikosa nafasi za kufunga, majonzi yalikuja dakika ya 77 pale mshambuliaji hatari wa Stella Abdijan Jean Zozo ‘Boli Zozo’ alipopokea pasi safi kutoka kwa N’guessan Serge na kumpindua beki wa kushoto wa Simba, Rashid Abdallah kisha kupachika bao safi la pili bao ambalo lilishangiliwa mno na mashabiki wa Yanga huku wakiimba; ‘Uzalendo umetushinda…Uzalendo umetushinda…!”

Benchi la Simba lilijaa simanzi baadhi ya wachezaji walitokwa na machozi.

Stella Abidjan ilibadilika tofauti na ile ilivyocheza mechi ya kwanza wiki mbili nyuma jijini Abidjan.

Wachezaji Amani Celestine, Solo Jean, Austine Koune, N’guessan Serge waling’ara na kuwafunika vibaya wachezaji wa Simba ambao walikata tamaa.

Hadi dakika 90 zinakamilika Simba ilishindwa kutwaa ubingwa na kuambulia nafasi ya pili iliyowawezesha kupata medali za fedha na kumpa wakati mgumu Rais wa Awamu ya Pili wakati akiwa madarakani na kuwa mgeni rasmi kulikabidhi Kombe la wageni.

Leo unaposoma ni imetimia miaka 30 ya majonzi kwa klabu ya Simba kwa kushindwa kuandika historia ya kubeba taji la kwanza la CAF, kama ilivyowakuta tu watani zao msimu uliopita mbele ya USM Alger ya Algeria waliobeba taji kwa faida ya bao la ugenini kwani Yanga ilifungwa nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0 kwa bao la penalti ya Djuma Shaban aliyepo Azam FC kwa sasa akisubiria kuanza kukikunisha.

Kukosa taji kwa Simba kuliponza mastaa wa timu hiyo kukosa zawadi ya magari aina ya KIA waliyoahidiwa na aliyekuwa mfadhili mkuu enzi hizo, Azim Dewji na kuishia baadhi yao kupewa Toyota Corolla na fedha tu, lakini taji na medali za fedha zikaenda Ivory Coast.

SOMA NA HII  GALLAS: NITASEPA BONGO WAKATI UKIFIKA