Home Habari za michezo KUHUSU USHINDI WA SIMBA LEO DHIDI YA KAGERA….HAYA HAPA YA NYUMA YA...

KUHUSU USHINDI WA SIMBA LEO DHIDI YA KAGERA….HAYA HAPA YA NYUMA YA PAZIA YAKUYAJUA…

Habari za Simba

KOCHA mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha amepata ushindi wa kwanza leo tangu atue Msimbazi baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa kocha huyo Mualgeria aliyechukua mikoba ya kuinoa Simba kutoka kwa Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefungashiwa virago baada ya kukubali kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao wa jadi Yanga.

Benchikha alianza kuisimamia Simba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy uliomalizika kwa suluhu nchini Botswana, kisha akaiongoza mbele Ya Wydad Casablanca na kupoteza kwa bao 1-0, na leo ilikuwa mechi yake ya tatu lakini ya kwanza nyumbani.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha alama 22 na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi tisa huku juu yake ikiwepo Yanga yenye pointi 24 baada ya mechi tisa na kileleni ni Azam FC iliyo na alama 28 ilizovuna katika michezo 12.

Kagera imesalia katika nafasi ya 12 kwenye msimamo ikiwa na alama 13 baada ya michezo 12.

Huo umekuwa ni mwendelezo wa matokeo bora kwa Simba mbele ya Kagera kwani katika mechi 10 zilizopita (ukitoa ya leo), Simba imeshinda saba, Kagera ikishinda mbili na sare moja.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Timu zote mbili zilianza kucheza kwa utulivu huku zikishambuliana kwa kupokezana ambapo katika dakika 20 za mwanzo Simba iliongoza kucheza katika upande wa Kagera.

Mchezo uliendelea kuwa hivyo hadi dakika ya 42 ambapo Simba ilipata bao la kuongoza kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ baada ya staa huyo kuangushwa kwenye boksi la 18 la Kagera.

Tuta hilo lilipigwa mara mbili kwani mara ya kwanza Saido alipiga na mpira kupanguliwa na kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda, lakini mwamuzi wa mechi hiyo, Hance Maneno aliamuru tuta lirudiwe kwa kile kikichodaiwa Chalamanda alitoka kwenye msitari wa goli kabla ya mpira haujapigwa, ndipo Saido akafunga katika marudio.

Katika kikosi cha Simba kilichoanza, kocha Benchikha alifanya mabadiliko matatu kulinganisha na kile kilichoanza dhidi ya Wydad Casablanca ugenini Morocco.

Moses Phiri alianza katika eneo la Jean Baleke, huku Clatous Chama akianza eneo la Kibu Denis, ilhali Mzamiru Yassin akianza katika nafasi aliyocheza Willy Onana kwenye mechi na Wydad.

Hata hivyo mabadiliko hayo yaliinufaisha Simba kwani ndani ya dakika 45 za kwanza iliongoza kumiliki wa mpira, kutengeneza nafasi na kulishambulia lango la Kagera Sugar.

Kwa upande wa Kagera, kocha Mecky Maxime alifanya mabadiliko sita kwenye kikosi kulingana na kile kilichoanza mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union na kupoteza kwa kuchapwa bao 1-0.

Aliwaanzisha benchi Anuary Jabir, David Luhende, Datius Peter, Cleophace Mkandala, Abdallah Seseme na kipa Alain Ngeleka mwenye kadi nyekundu na nafasi zao kuchukuliwa na Dickson Mhilu, Chalamanda, Disan Ngaliwango, Shamte Hijja, Deogratius Mafie na Ally Mashaka.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kagera Sugar kufanya mabadiliko matatu wakiingia Datius, Anuary na Said Nushid waliochukua nafasi za Mhilu, Nicholaus Kasozi na Mafie.

Simba ilijibu mapigo dakika ya 63 kwa kuwaingiza Onana, Baleke na Kibu wakitoka Chama, Mzamiru na Phiri na dakika tatu baadaye Kagera ilimtoa Obrey Chirwa na kuingia Mkandala.

Baada ya kukosa mabao ya wazi zaidi ya matatu, kiungo Sadio Kanoute katika dakika ya 75 aliiandika Simba bao la pili kwa kichwa akiunganisha krosi ya kichwa iliyopigwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na dakika moja baadaye Kagera Sugar ilifanya mabadiliko mengine ikimuingiza Hamis Kiiza na kumtoa Ally Nassoro.

SOMA NA HII  ACHANA NA STORI ZA VIJIWENI...HUU HAPA UKWELI WA KWANINI KAMBOLE HATACHEZA MECHI YA LEO DHIDI YA SIMBA...