Home Habari za michezo YANGA, SIMBA LIGI YA MABINGWA NUSU FEDHEA NUSU HESHIMA

YANGA, SIMBA LIGI YA MABINGWA NUSU FEDHEA NUSU HESHIMA

Yanga SC na Simba SC

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga bado wako kwenye hatihati ya kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya abingwa Afrika kutokana na matokeo waliyopata kwenye mechi tatu walizocheza kwenye mashindano hayo.

Mpaka sasa wote wanaburuza mkia kwenye makundi yao wakiwa na pointi mbili kila mmoja walizopata kutoka kwenye mechi tatu walizocheza. Kundi B lililopo Simba, timu inayoongoza ni Asec Mimosas yenye pointi saba ikifuatiwa na Jwaneng Galaxy yenye nne kisha Wydad AC inayomiliki pointi tatu.

Upande wa Kundi D ilipo Yanga, Al Ahly inaongoza ikikusanya pointi tano ikifuatiwa na CR Belouizdad yenye pointi nne sawa na Medeama inayoshika nafasi ya tatu ambayo imezidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kutokana na hayo, baadhi ya wadau wakubwa wa soka nchini wameeleza wanachokiona kuelekea mechi tatu zilizobaki kwa kila timu, kwamba nini kifanyike kwa ajili ya faida ya timu hizo katika michuano hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Tanzania, Ally Mayay ameeleza kuwa hali hiyo imetokea kutokana na ugumu wa michuano yenyewe msimu huu lakini pia ubora wa timu hizo mbili
msimu uliopita zimechagiza hali hiyo.

“Kwanza ifahamike hii ni hatua kubwa kwa maana ya wanakoanzia kwenye mechi za mtoano za mchujo mpaka kufikia makundi mnakutana na timu za hali nyingine hivyo hapo sasa lolote linaweza kutokea maana zinakuwa bado hatua chache kabla ya kucheza fainali.

“Lakini kingine ni Yanga ilichofanya msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika au Simba kuingia robo fainali mfululizo, inafanya kunakuwa na deni na matamanio ya kupata kikubwa zaidi kila msimu, sasa ikitokea kama hivi kunakuwa na shida kidogo
kukubaliana na hiyo hali.

“Ila kwa bahati nzuri timu zote mbili zimebakiza mechi mbili za nyumbani na ugenini moja, kwa hiyo hapa ndipo pa kuweka vizuri mpango wa kuhakikisha unachukua pointi zote za nyumbani ili kujisogeza juu kwenye msimamo na kusubiri kuona mwisho unakuwaje,” anasema Mayay.

Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars aliongeza kuwa ni muhimu pia timu hizo kufanya marekebisho kila siku kulingana na mazingira ya wapinzani na soka linavyobadilika kila baada ya mechi.

Anasisitiza kuwa kama maeneo hayo yakifanyiwa kazi anaamini kuna nafasi kubwa ya timu hizo kupata nafasi ya robo fainali na kuendelea kuliwakilisha vyema taifa katika michuano hiyo mikubwa ya klabu Afrika.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema viongozi na wachezaji wa timu hizo waelewe kwanza kilichopatikana mpaka sasa kwa taifa si sawa kisha wajue nini cha kufanya ili kuondoa haya masononeko kwa Watanzania.

“Kwanza watambue Tanzania inasononeka kwa haya matokeo, watu wanasema tutapita lakini mioyoni mwao wanasononeka hivyo viongozi na wachezaji watambue kilichopatikana mpaka sasa kwa upande wao si kitu sahihi.

“Wajipange vizuri zaidi kwenye mechi zilizobaki, makocha waone nini shida mpaka tunaruhusu mabao na tunashindwa kuwafunga wapinzani, waanzie hapo naamini mengine yatafuata, unajua kwa tulipofikia, kuna timu zinatuogopa Afrika hivyo lazima tuendelee kuogopwa, isiwe tunafungwa na kukosa matokeo kirahisi,” anasema Kibadeni.

Kocha wa zamani wa timu za Biashara United, Lipuli, Mbao na Mbeya City, Amri Said ‘Stam’ anasema: “Upande wangu naona Simba ina nafasi kubwa bado ya kwenda hatua inayofuata
kutokana na mabadiliko makubwa ya timu baada ya ujio wa kocha Benchika (Abdelhak).

“Na Simba kwa namna inavyocheza hata katika mechi tatu zilizopita inaweza kabisa kushinda nyumbani au ugenini hivyo ni suala la kujiweka sawa na matokeo yanaweza kupatikana katika mechi hizi tatu zilizobaki.”

Beki huyo wa zamani wa Simba, pia ameitaja Yanga kuwa na nafasi ingawa ni kama wana mtihani mkubwa wa kuiweka sawa timu hiyo kutokana na kuondokewa na wachezaji wao wengi waliochangia mafanikio makubwa kimataifa msimu uliopita.

“Yanga inapambana, inacheza vizuri, nayo ina nafasi japo kuna kuiunganisha timu kutokana na kuondoka kwa Bangala (Yanick), Mayele (Fiston), Djuma (Shaban) na
wengine ambao kwa sasa hawatumiki kama mwanzo kama kina Sureboy (Salum
Aboubakar), kwa hiyo unaona kuna kitu zaidi Yanga kinahitajika kuvuka hapa ilipo,” anahitimisha Stam.

Kipa wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa Singida Fountain Gate, Manyika Peter amezitaka timu hizo kuondoa taswira ya mechi za nyumbani na ugenini na badala yake wapambane kupata ushindi kokote ili wajinusuru kuishia makundi.

“Bado kuna nafasi kwa timu zote, hata hao wanaoongoza makundi kwa mechi zilizobaki, kama timu zetu zitashinda mechi zote basi kuna uwezekano mkubwa wa kupenya hapa tulipo.

“Kwa sasa hakuna tena cha nyumbani wala ugenini, zaidi ni kupambana kupata ushindi na wakati huo lazima wapinzani wao nao wanakutana wanapunguzana wenyewe
kwa wenyewe, hivyo kama watapambana watapata pointi zote tisa zilizobaki na wasikate tamaa kwenye soka lolote linatokea,” anasema Manyika.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ yeye ana maoni tofauti kuhusiana na hilo ambapo anaamini kinachowaangusha vigogo hao ni kutokuwa na wachezaji wakubwa kwenye vikosi hivyo ingawa anaamini makocha waliopo ni sahihi.

“Nafikiri kwa mechi zilizobaki hizi timu zisijipe presha ya kuhusu hatua ya robo fainali, waingie uwanjani wapambane kimbinu, kisoka na ikitokea imeshindikana basi uongozi na benchi wajipange kusuka kikosi cha msimu ujao cha kupambana na timu nzito.

“Nasema hivyo kwa maana ya ukitazama wachezaji waliopo sasa ni tofauti kiushindani na walio kwenye timu nyingine, kila kukicha wao (wapinzani) wanasajili wachezaji wakubwa, ghali na bora zaidi.

fano mtazame yule Percy Tau wa Al Ahly, pesa anayolipwa halafu unakutana naye robo fainali hawezi kuwa kama kwenye makundi, kwa hiyo hivi ni vitu vya kujifunza na kuchukua ili tufike mbali wakati mwingine.

“Angalia hata Benchika, ni kocha mkubwa lakini naamini wachezaji walio pale Simba hawaendani na anachowaza kichwani, hivyo lazima msimu ujao aunde kikosi kikubwa zaidi ili kuendana na anachotaka, ndio maana nasema msimu huu kusiwe na presha, tuchukulie
kama funzo kwa ajili ya mapambano kamili msimu ujao,” anasema Jembe Ulaya.

Winga wa zamani wa Simba na Yanga, Edibily Lunyamila anaeleza: “Nafasi bado ipo japo si nyepesi na zaidi wasitoe sana macho katika mipango ya mechi zote tatu, waanze na hizi zinazofuata sasa ili wapate ushindi na kuwapa nguvu katika mechi zilizosalia.

“Mfano Simba mechi yake inayofuata na Wydad haitakuwa nyepesi sababu wameshaamka walipopata ushindi dhidi ya Simba mechi ya mwisho na Simba inahitaji kupata ushindi hapa ili wapate matumaini, kwa hiyo haitakuwa mechi rahisi lakini inawezekana.

SOMA NA HII  BENCHIKHA AREJESHA MATUMAINI MAPYA SIMBA