KIUNGO wa Yanga, Jonas Mkude amejikuta mtegoni baada ya nafasi yake kikosini kuendelea kuwa finyu huku baadhi ya vigogo wakitaka aondoke kutokana na mwenendo wake wa kinidhamu.
Nyota huyo aliyejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Simba alikocheza kwa zaidi ya miaka 11, hajaonyesha kile Yanga ilichotarajia kutoka kwake kwa maana ya ubora.
Mkude ameichezea Yanga mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya JKT kwa dakika saba na Simba dakika saba jumla ya dakika 14 kati ya 810 ilizocheza kwenye ligi, ilhali katika Ligi ya Mabingwa Afrika akicheza dakika 15 katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Asas ya Djibouti.
Ukiachana na kukosa nafasi mbele ya viungo Khalid Aucho, Zawadi Mauya na Mudathir Yahya wanaocheza eneo hilo, Mkude pia amekuwa na tuhuma za utovu wa nidhamu.
“Hadi sasa kocha ndiye anamfanya aendelee kuwepo lakini kiuhalisia viongozi hawaoni haja ya kuendelea naye. Tunasubiri ripoti ya mwalimu kama atapendekeza abaki basi atabaki kumalizia mkataba na mwishoni mwa msimu ataondoka,” alisema mmoja ya viongozi.
Huenda nyota huyo wa zamani wa Simba akawa kwenye kikosi cha Yanga kitakachocheza mechi ya ligi leo dhidi ya Mtibwa Sugar.