Home Habari za michezo SIMBA YANGA VICHEKO TU

SIMBA YANGA VICHEKO TU

Yanga SC na Simba SC

Saa kumi juu ya alama Simba itakuwa kwenye kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume, Botswana kuikabili Jwaneng Galaxy mechi ya Kundi B. Awali ilikuwa kipigwe kwenye Uwanja wa Taifa ambao uko Gaborone lakini zikatokea figisu wakasogezwa kwenye mji mwingine ulioko kilomita kadhaa nje.

Lakini viongozi wa Simba walishtukia hali hiyo mapema na kujipanga ambapo wamesisitiza kwamba hawana presha yoyote watatumia uzoefu wao kushinda mchezo huo. Wamewaahidi mashabiki kwamba furaha ipo leo. Yanga wao wataingia kwenye Uwanja wa Mkapa saa 1 usiku kuwakabili Al Ahly wakiwa tayari na matokeo ya Simba.

Utakumbuka mechi zilizopita Yanga alichapwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria na Simba akadroo Dar es Salaam dhidi ya Asec Mimosas yenye pumzi na pasi nyingi.

Makocha na wachezaji wa Simba na Yanga wanajua matokeo ya ushindi ndio pekee yatakayowapa faraja na furaha mashabiki wao, vinginevyo wikiendi itakuwa ngumu kwa vijembe vya wao kwa wao.

HESABU ZA YANGA

Lugha nyingine tofauti na ushindi leo watakuwa wamejiweka rehani. Hata sare pia tatizo. Hivyo kwa namna yoyote ile inatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inapata ushindi dhidi ya Ahly bila kujali kuwa ni mabingwa watetezi wala ukubwa wao wa namna yoyote ile.

Ile kauli ya kila mtu ashinde zake inaanza na hii kwa mujibu wa Bakary Mwamnyeto. Pale kati atachezeshwa na mwamuzi Abdel Aziz Mohamed Bouh kutoka Mauritania na wenyeji wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali juu dhidi ya Wamisri ambao mwezi uliopita walikuwepo nchini kucheza na Simba kwenye mechi ya African Football League na kutoka sare nje ndani.

Nidhamu kubwa hasa dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza inahitajika kuwepo kwa safu ya ulinzi ya Yanga ili kutoruhusu kujirudia kwa makosa kama yale ambayo yaliwaponza katika mechi ya kwanza dhidi ya CR Belouizdad ambapo licha ya timu hiyo kutandaza soka tamu, lakini ilipoteza mchezo mbele ya Waalgeria.

Urejeo wa kipa Djigui Diarra una umuhimu mkubwa kwa Yanga kutokana na uwezo wa kipa huyo raia wa Mali wa kudaka na ujenzi wa mashambulizi kuanzia nyuma, kuipanga na kuituliza safu ya ulinzi lakini pia kuokoa hatari zinazoelekezwa langoni mwake.

Kocha Miguel Gamondi ataendelea na soka lake la kushambulia kama alivyokuwa akifanya dhidi ya timu nyingine lakini akichukua tahadhari ya kujilinda kwa haraka pindi timu inapopoteza mpira.

SIYO KINYONGE

Yanga haina historia nzuri mbele ya Al Ahly iwe katika mechi za nyumbani au ugenini na pengine leo ni muda sahihi wa kuthibitisha kuwa nyakati za unyonge dhidi yao zimeshaisha kwa kupata ushindi nyumbani.

Historia inaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 10 katika mashindano tofauti ya klabu Afrika ambapo katika idadi hiyo ya michezo, Al Ahly imeshinda mara sita, sare tatu na imepoteza moja tu kwa Yanga.

Katika mechi hizo 10, tano, Yanga ilikuwa mwenyeji ambapo iliibuka na ushindi mara moja, sare tatu na ikapoteza mechi moja.

Lakini kwa sasa mambo yamebadilika sana na hapana shaka Al Ahly itakutana na mechi ngumu zaidi pengine kuliko zote walizowahi kucheza na Yanga kutokana kuimarika vilivyo kwa wawakilishi hao wa Tanzania kunakobebwa na hali ya kujiamini hasa inapokuwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kuthibitisha hilo, katika mechi tano zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ilizocheza nyumbani,Yanga imeibuka na ushindi mara nne na kupoteza mechi moja tu.

TABULELE NA VIKOI

Mechi ya leo imepewa jina maalumu la ‘Bacca Day’ ikinasibishwa na beki wa kati wa Yanga kutoka Zanzibar, Ibrahim Abdallah Ahmad, huku mashabiki wakihamasishwa kumuunga mkono kwa kutinga Kwa Mkapa na misuli, vikoi, Kanzu na baraghashia kwa wanaume na wenzao wa kike kuvaa baibui na majuba. Ni mtoko wa Wananchi.

Mavazi hayo ni maarufu kwa wakazi wa Zanzibar anakotokea beki huyo, lakini uwanjani hapo kutakuwa na burudani nyingine kutoka kwa msanii Mkongoman wa Kundi la KKL Bomoko linalotamba na wimbo wa Tabulele Laah, aliyeletwa nchini maalumu kwa mchezo huo.

Tayari msanii huyo amefanya remix ya ngoma hiyo ya Tabulele Laah akimshirikisha Harmonize na leo wataliamsha kuwapa raha mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo ambao wamepata mzuka kutokana na kauli za mastaa wa timu hiyo kuwahakikishia leo wanafanya kweli mbele ya Wamisri.

KIKOSI CHA USHINDI

Dalili zinaonyesha hakutokuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi cha Yanga leo kulinganisha na kile kilichoanza dhidi ya CR Belouizdad. Diarra hapana shaka atarudi langoni kuchukua nafasi ya Metacha Mnata na nafasi nyingine ambayo inaweza kuwa na mabadiliko ni ile ya Kennedy Musonda ambayo inaweza kuanzwa na Clement Mzize.

Kikosi; Diarra, Yao Attohoula, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahaya, Mzize, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.

GAMONDI MATUMAINI KIBAO

Kocha Gamondi alisema; “Ni mchezo muhimu kwetu kupata ushindi. Hatukufanya vizuri katika mechi ya kwanza hivyo ni lazima kupata ushindi ili tuweke sawa hesabu zetu kwenye kundi,” alisema Gamondi, huku nahodha Bakar Mwamnyeto amesema kwa namna walivyojiandaa anaamini wataikabili Al Ahly kwa lengo la kupata ushindi nyumbani baada ya kupoteza ugenini mchezo uliopita. Ushauri wa Kocha wa zamani wa Simba, Robertinho kwa Yanga; “Kama Yanga watatumia mfumo wa 4-3-3 wakati wa kushambulia utawafanya kuwa na idadi nzuri kule mbele katika mashambulizi yao ambayo itawapa wakati mgumu mabeki wa Al Ahly ambao hawana utulivu sana.

“Ahly hawana kasi sana ya kukimbia kurudi nyuma kujilinda hili lazima Yanga ilitumia kwa kucheza mpira wa kasi ili wafike langoni kwao kuwapa presha mabeki wao.”

SIMBA MZUKA BOTSWANA

Ujio wa kocha mkuu mpya, Abdelhak Benchikha kutoka Algeria, umeongeza mzuka kwenye kambi ya Simba iliyotua Gaborone kabla kusafiri hadi mji wa Francistown utakaotumika kwa mechi hiyo ikiwa na wachezaji 25 na wote wameahidi kupambana ili kupata ushindi kujiweka pazuri katika Kundi B.

Sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Asec Mimosas imewamsha wachezaji wa Simba kwa kutambua mechi ya leo ni ngumu kutokana na wenyeji wao, Jwaneng Galaxy kuongoza kundi hilo baada ya kuifumua Wydad Casablanca kwa bao 1-0 ikiwa kwao Morocco.

Kupoteza mechi ya leo kutaiweka Simba katika uwezekano finyu wa kuingia robo fainali hasa ikizingatiwa mechi mbili zinazofuata ni ngumu dhidi ya Wydad ambayo msimu uliopita iliwatoa hatua kama hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 180 kumalizika kwa sare ya 1-1 kila timu ikishinda mechi ya nyumbani.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Mohamed Adel kutoka Misri na Simba haina kitu kingine inachokihitaji zaidi ya ushindi tu na Benchikha amesisitiza kwamba bado ataendelea kutumia mbinu za kina Cadena wakati akiendelea kusoma picha linavyoenda.

NI KISASI KIZITO

Kwa Simba hiyo ni fursa nzuri ya kulipa kisasi kwa Jwaneng Gaaxy ambayo msimu wa 2021/2022 iliwatupa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kanuni ya faida ya mabao ya ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Kumbukumbu ya mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika inaonyesha Simba haina ubabe ugenini ambapo imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare mbili na kupoteza tano.

Lakini hilo halipaswi kuipa hofu Simba kwani Jwaneng nao wamekuwa hawana historia ya utemi nyumbani ambapo katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika, wameshinda nne tu, sare moja na wamepoteza mechi tano. Wachezaji wa Simba akiwamo nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wamewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutokuwa na hofu, kwani wamepania kutoka na ushindi kwenye mchezo huo licha ya kuwa ugenini.

AYOUB AMEIVA

Kikosi cha Simba leo; Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Enock Inonga, Fondoh Malone, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Fabrice Ngoma, Jean Baleke, Clatous Chama na Kibu Denis.

Morena Ramorebodi, kocha mkuu wa Jwaneng Galaxy, alisisitiza jana kwamba; “Tunacheza dhidi ya timu ngumu sana na mechi si rahisi kujiandaa nayo. Tuko nyumbani, tutacheza kwa ujasiri, kiburi na mashambulizi makali lakini tukiwapa heshima yote Simba kwa sababu wana wachezaji wenye uwezo wa kiufundi.”

FIGISU UWANJA

Mratibu wa Simba, Abbas Ally amesema; “Suala la kubadilisha uwanja sisi tulishaanza kulipata toka awali hivyo tumejipanga kukabiliana na hilo, ingekuwa mchezo unachezwa nje ya mji wa Botswana tungesema mengine hivyo hatuwezi kutoka mchezoni kwa sababu ya aina hiyo.”

CADENA

Kocha Daniel Cadena alisema wapo tayari; “Morali ya timu iko juu sana na wachezaji wanatamani kupata ushindi katika huu mchezo ili tuweze kupata pointi tatu ambazo zitatuweka katika nafasi nzuri kwenye kundi.”

Cadena ambaye amekuwa na timu hiyo tangu kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutimuliwa na yeye ndiye atakayeliamsha licha ya Benchikha kuwepo kikosini. Simba itasafiri kuifuata Wydad ambayo leo saa 4 usiku itakuwa ugenini kuvaana na Asec Mimosas, huku Yanga yenyewe itasafiri kwenda Ghana kuikabili Medeama ambayo jana usiku ilikuwa nyumbani kuikaribisha CR Belouizdad katika mechi ya Kundi D.

Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kupata kila kitu kuhusiana na mechi za leo. Tutakupa kila kinachoendelea. Weka bando tu mengine tuachie sisi na kesho nunua Mwanaspoti.

SOMA NA HII  FEI TOTO AFUNGUKA HAYA KWA MARA YA KWANZA TANGU ALIPOTIMKA YANGA