Home Habari za michezo TATIZO LA YANGA KWENYE LIGI YA CAFCL LIPO HAPA

TATIZO LA YANGA KWENYE LIGI YA CAFCL LIPO HAPA

Habari za Yanga

Yanga ndio mabingwa wa Ligi Kuu Bara, mabingwa wa kihistoria na ndiyo timu iliyofanikiwa zaidi katika historia ya soka la Bongo.

Kwa sasa ndiyo timu yenye kikosi bora zaidi na msimu uliopita walifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na ikatwaa mataji yote ya ndani pia.

Kwa kifupi Yanga wapo kwenye kilele cha ubora wao. Ni majuzi tu hapa wametoka kumfunga mtani wao Simba mabao 5-1. Ni ushindi mkubwa mno kwenye mechi za watani.

Kwa ubora wa kikosi cha Yanga wamefuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25. Ni hatua kubwa. Timu bora huweka rekodi bora.

Hata hivyo, nina tatizo moja na namna Yanga wameingia katika mechi za hatua ya makundi. Wamecheza mechi tatu za awali bila kupata ushindi.

Wameruhusu mabao kwenye kila mchezo. Walianza kwa kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa mabingwa wa Algeria, CR Belouizdad. Wakapata sare na Al Ahly na kisha Medeama ya Ghana.

Ubaya ni katika mechi zote tatu Yanga ndio ilitawala mpira kuliko wapinzani wao. Wanamiliki mchezo, wanapiga pasi nyingi lakini ushindi umekuwa mgumu.

Mfano mchezo wa kwanza pale Algeria, Yanga ilitawala karibu kila kitu lakini bado ilipoteza. Kwa nini? Subiri nitakueleza. Katika mechi hizi za CAF kucheza vizuri siyo kipaumbele, muhimu ni ushindi. Unapaswa kucheza kimkakati sana. Unapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa.

Hizi ni mechi ambazo unakutana na timu zilizofanya vizuri zaidi katika nchi zao. Ukifanya kosa moja tu, wanatumia hilo hilo kukuadhibu. Ndicho ambacho kinawapa Yanga wakati mgumu.

Makosa ambayo ukifanya kwenye mechi ya Mtibwa Sugar ama Geita Gold na usiadhibiwe, ukiyafanya mbele ya Belouizdad ama Al Ahly lazima watakuadhibu.

Tazama mfano penalti aliyosababisha Dickson Job pale Ghana, ingekuwa kwenye Ligi Kuu pengine wapinzani wasingeweza kulazimisha vile. Refa asingeweza kuamua vile. Lakini hii ni Ligi ya Mabingwa, watu wanacheza kimkakati.

Kwa ubora wa kikosi cha Yanga, kama wanatuliza akili na kucheza mpira wa malengo katika mechi tatu zilizosalia, bado wanaweza kwenda Robo Fainali.

Kupunguza makosa katika ulinzi. Kuheshimu uwezo wa wapinzani na kutumia vizuri nafasi chache wanazotengeneza. Hapa wanaweza kubadili upepo.

Ila kama watacheza michezo yote wakiamini wao ni wakubwa, wataendelea kupata wakati mgumu kwenye matokeo. Watahesabu pasi nyingi lakini mechi itamalizika wakiwa hawana cha maana.

Ila yote kwa yote, Pacome Zouzoua ameonyesha utofauti mkubwa na wachezaji wenzake kwenye michezo hii ya CAF. Mechi zote tatu amecheza vizuri sana.

Anaanzisha mashambulizi. Anakaa kwenye nafasi. Ana utulivu ndani ya eneo la hatari. Haishangazi kuona amefunga mabao yote mawili ya Yanga. Tazama alivyotulia na kufunga bao kali dhidi ya Al Ahly dakika ambazo watu walishaamini Yanga imepoteza mchezo. Mchezaji mahiri sana huyu. Ananikumbusha yule Clatous Chama wa msimu wa kwanza. Alikiwasha kweli kweli kwenye mechi za CAF. Alicheza vyema Kwa Mkapa na ugenini.

Ndivyo ambavyo wachezaji wakubwa hufanya. Anatulia wakati wenzake wamepagawa. Anafunga kwenye mazingira yoyote. Huyo ndio Pacome. Profesa wa soka.

SOMA NA HII  YANGA SIMBA HAKUNA KUZUBAA KIMATAIFA