Wakati tetesi zikieleza Simba inaisaka saini ya kiungo mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Edwine Balua, uongozi wa Maafande hao umesema unawasubiri wekundu hao mezani, huku nyota huyo akiweka wazi yupo tayari kwenda popote.
Balua amekuwa na kiwango bora tangu ajiunge na ‘Wajelajela’ hao wa jijini hapa misimu miwili sasa akitokea Coastal Union huku akiwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza. Hivi karibuni tetesi zimekuwa zikisambaa Wekundu hao tayari wametuma ofa kwa nyota huyo ambaye mkataba wake na Prisons unaisha mwisho wa msimu huu na wanahitaji huduma yake.
Balua ambaye aliwahi kuwatungua Wekundu hao msimu uliopita kwenye kipondo cha 3-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, alisema bado hajapokea simu yoyote na kinachoendelea anasikia tu mitandaoni.
“Nipo tayari kucheza popote kwa sababu mchezaji yeyote ndoto zake ni kucheza kwa mafanikio kwenye timu kubwa, hivyo kama ofa itafika tukakubaliana hamna shida,” alisema Balua mtaalamu wa mipira adhabu.
Meneja wa timu hiyo, Raulian Mpalile alisema, “Waje tu tuzungumze kwa sababu mchezaji bado ana mkataba na timu, tunasikia taarifa hizo ila uongozi bado haujazungumzA na hao wanaomtaka, hatuwezi kuzuia chochote mpira ni maisha.”
SOMA NA HII KUELEKEA MECHI YA CAF NA WASAUZI...TFF WAIPA MBELEKO YANGA KOMBE LA SHIRIKISHO BONGO....