Kiungo wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Feisal Salum Fei Toto amesema wapo tayari kuiheshimisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya ‘AFCON 2023’ yanayotarajia kuanza keshokutwa Jumamosi (Januari 13) nchini Ivory Coast.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars imepangwa Kundi F pamoja na timu za Morocco, DR Congo na Zambia, ambapo itaanza kampeni ya kusaka taji hilo kwa kucheza na vinara wa soka Afrika, Morocco.
Akizungumza akiwa nchini Ivory Coast, kiungo huyo amesema maandalizi wanayofanya chini ya Kocha Mkuu Adel Amrouche yamewaongezea ari ya kupambana na kulipa heshima taifa lao, licha ya kwamba watu wengi hawawapi nafasi.
“Ukweli kila mchezaji amepania kuipa heshima Tanzania kwa kufanya vizuri kwenye mashindano haya, najua tupo kundi gumu lakini hakuna kinachoshindikana, hata hao waliokuwa juu walianza kama sisi kwa hiyo Watanzania waondoe hofu tupo kwa ajili yao,” amesema Fei Toto.
Akijizungumzia yeye binafsi amesema tofauti na ilivyokuwa fainali za mwaka 2019, ambapo alikuwa kijana mdogo kwa sasa yupo fiti na yupo tayari kwa mapambano kuipigania nchi yake.
Amesema ana uzoefu wa kutosha kutokana na kucheza mashindano mengi kwenye ngazi ya klabu hivyo matarajio yake mbali na kuiheshimisha Tanzania, lakini pia anataka kuitumia michuano hiyo kuonesha kipaji alichokuwa nacho.
SOMA NA HII WAKATI SIMBA WAKIPANGA KUSHUSHA 'FULL' KIKOSI LEO...KOCHA WA SALLEM VIEW 'ALIA MAPEMA'..