Home Habari za michezo MHHHH….KWA HILI LA MANULA HAPANA AISEEE….KUNA JAMBO HALIKO SAWA TOKA 5G YA...

MHHHH….KWA HILI LA MANULA HAPANA AISEEE….KUNA JAMBO HALIKO SAWA TOKA 5G YA YANGA…

Habari za Michezo

NI ngumu kuamini, ukweli ndio huu, mapito anayopitia kipa Aishi Manula yameshtua mashabiki wa soka kwani hawajamzoea kumuona hivyo alivyo.

Manula alirejea tena akitokea kuwa majeruhi wa muda mrefu tangu alipoumia katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) la msimu uliopita wakati Simba ikiizamisha Ihefu kwa mabao 5-0. Mechi hii ilipigwa Aprili 7, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Tangu amerejea, rekodi zinaonyesha, Manula amecheza mechi tatu za kiushindani na kufungwa mabao 10!

Bila ya kuangalia mazingira au aina ya mabao aliyofungwa, hii sio rekodi nzuri kwa mchezaji wa kiwango chake akiwa kipa namba moja wa Tanzania na klabu ya Simba anayoitumikia kwa msimu wa saba sasa.

Kipa huyo alianza kucheza baada ya kutoka kuwa majeruhi katikati ya Oktoba kwa kupewa mechi za kirafiki ikiwamo dhidi ya Dar City ambapo Simba ilishinda mabao 5-1 kwenye uwanja wa mazoezi, kabla ya kupewa pambano la Kariakoo Derby, lililopigwa Novemba 5 mwaka jana na kukutana na dhahama la Yanga.

TANO ZA KWANZA

Manula aliyeanza kupata jina akiwa na Azam FC zaidi ya miaka 10 iliyopita kabla ya kujitengenezea ufalme langoni akichukua nafasi ya makipa waliowahi kutamba nchini kama Juma Kaseja, Ivo Mapunda na wengine, alikuwa hajawahi kukutana na kipigo cha mabao mengi katika Ligi Kuu Bara.

Lakini katika mechi hiyo ya watani, iliyokuwa ya kwanza kwake tangu alipotoka majeruhi, alikubali nyavu zake kuguswa mara tano. Ndio, Simba ilikufa kwa mabao 5-1, mbele ya Yanga na kuvunja mwiko wa Simba wa kutowahi kupigwa mabao mengi na watani wao, tangu ilipofanya hivyo mwaka 1968 wakati Wekundu wa Msimbazi walipopigwa 5-0.

Sio kama Manula hajawahi kupigwa idadi hiyo ya mabao matano akiwa na Simba, la! Alishakumbana na vipigo hivyo kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilipochakazwa 5-0 na AS Vita jijini Kinshasa kisha kwenda kupokea tena idadi kama hiyo mbele ya Al Ahly ya Misri, lakini katika Ligi Yanga ilimtibulia.

Katika mechi hiyo, Manula alicheza kwenye kiwango cha chini mno kulinganisha na yule aliyezoeleka lakini mashabiki wa soka walimuelewa kwamba ni vile alitokea kuwa majeruhi na kumlaumu kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwa uamuzi wa kumuanzisha, ilihali hakuwa hajapata muda mrefu kujiweka fiti kwa ushindani.

Ndio maana haikushangaza sasa waliposikia viongozi wakimfurusha Robertinho, kwa kuamini huenda kipigo hicho kilichangiwa na uamuzi wake wa kumchezesha Manula kwenye mechi ngumu na muhimu kama hiyo, wakati alikuwa na makipa Ally Salim na Ayoub Lakred aliyeonyesha kiwango kwenye mechi chache katika kipindi hicho.

TANO ZA STARS

Kama haitoshi, kipa huyo akarejeshwa timu ya taifa na akacheza mechi ya kirafiki wakati wa maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazofanyika Ivory Coast na kutunguliwa mabao mawili na Misri katika mechi iliyopigwa jijini Cairo.

Lakini wakati mashabiki wakiendelea kujiuliza, kulikoni Manula aliyezoeleka kuokoa michomo mikali, kuokoa penalti na kuzibeba timu anazozidakia, fainali za Afcon zikafika na juzi usiku mwamba alikuwa langoni kuikabili Morocco katika mchezo wa Kundi F.

Katika mechi hiyo, Manula alitunguliwa mabao matatu na hivyo kuwa ameruhusu mabao matano kwenye timu ya taifa kama ilivyo kwenye klabu ya Simba na hivyo kuonekana amerejea katika kipindi kibaya cha kuruhusu mabao mengi na vipigo mfululizo kwa timu zake akitunguliwa jumla ya mabao 10 katika mechi tatu tu.

GARI HALIJAWAKA

Kwenye mitandao ya kijamii walipokuwa wakimjadili Manula wanaeleza ni kama ameharakishwa kubebeshwa majukumu langoni kabla hajakaa vizuri, yaani gari lake halijawaka sawasawa, ila analazimishwa kuvishwa mabomu.

Wapo wanaosema ni vyema kama angepewa muda wa kupona kabisa na kupewa mechi laini kuliko hivi sasa ambavyo sio tu vinamshushia hadhi, lakini inachafua rekodi tamu alizokuwa nazo kipa huyo tangu akiwa Azam, Simba na hata timu ya taifa.

Kuna wengine wanabashiri kama ataendelea kupewa nafasi ya kusimama kwenye mechi mbili zijazo za Stars katika fainali hizo za Afcon, huenda akavuka idadi ya mabao aliyowahi kufungwa kwenye fainali za 2019 ambapo mechi tatu, alitunguliwa jumla ya mabao manane.

Stars ilianza kufungwa 2-0 na Senegal, kisha ikalala 3-2 mbele ya Harambee Stars ya Kenya na kuchapwa 3-0 na walioibuka mabingwa wa Afcon wa msimu huo, Algeria.

Stars itashuka uwanjani Jumapili hii kuvaana na Zambia kabla ya Januari 24 kumalizana na DR Congo, huku mashabiki wakiwa na wasiwasi kama mambo hayawekwa vizuri, huenda Stars inaendeleza rekodi ya kutowahi kupata ushindi kwenye fainali za Afcon tangu 1980, ilipoishia kuambulia sare moja pekee.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa makipa wa Simba, raia wa Hispania, Dani Cadena anayemnoa Manula amesema kila kipa anafungwa na jukumu la kuzuia kufungwa ni la timu nzima kwa ujumla hivyo Manula hastahili kulaumiwa peke yake kwa kushuhudiwa akiruhusu mabao mengi kwenye mechi hizo tatu zilizopita.

“Manula ni kipa bora na anatimiza vyema majukumu yake. Hadi mpira umfikie kipa maana yake kuna makosa yamefanywa na wachezaji wa ndani hivyo akishindwa kuuzuia basi hapaswi kulaumiwa peke yake bali wote waliohusika kwenye makosa kuanzia mwanzo,” alisema Cadena mwenye Leseni ya FIFA Pro.

Kocha wa soka, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alimkingia kifua Manula akisema amekuwa akifanya kazi kubwa mara nyingi uwanjani kuibeba timu, ila dosari zake chache ndizo huzungumziwa zaidi.

“Ukimlaumu Manula kwenye mechi ya jana (juzi, dhidi ya Morocco) utakuwa unamvunjia heshima na kumkatisha tamaa. Mabao karibu yote Tanzania iliyofungwa ni makosa ya mabeki na sio Manula,” amesema Mwaisabula na kuongeza;

“Pia hata kwenye mechi na Misri ambayo Tanzania ilifungwa 2-0, Manula hauwezi kumlaumu kwa bao lolote. Manula ni kipa mzuri, amekuwa akiokoa mabao mengi kuliko anayofungwa binafsi katika mechi hizo mbili sioni kama kuna mahali pa kumlaumu labda ingekuwa kwenye mechi ile dhidi ya Yanga aliyofungwa mabao matano kwani alicheza akiwa hajawa fiti na hapo huenda alilazimishwa kucheza.”

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Pondamali ‘Mensah’ amesema anatambua Manula hana muda mrefu tangu amerejea uwanjani kutoka kwenye majeraha, lakini hawezi kuzungumzia kupewa kwake mechi au kutompa nafasi kwani hajui anafanya nini anapokuwa kwenye uwanja wa mazoezi.

“Kufungwa kwa kipa ni kawaida na kipa yeyote anaweza kufungwa, hivyo tusiwalaumu sana makipa wetu bali tuwajenge kuwa bora zaidi. Ninachoweza kusema kuhusu Manula kupewa nafasi au kutopewa hilo tuwaachie makocha wanaomfundisha na wanaokuwa naye zaidi mazoezini kwani hao ndio wanajua ubora wake tofauti na mtu yeyote. Unaweza kumlaumu lakini kumbe mazoezini ni bora kuliko makipa wengine waliopo,” amesema Pondamali.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  MAYELE: TULICHOTAKA KUKIFANYA SUDAN ...TUTAKIFANYA JUMAPILI KWA SIMBA....