Home Habari za michezo PAMOJA NA KUFUNGIWA….KOCHA TAIFA STARS AIBUKA NA HILI TENA KUHUSU MOROCCO

PAMOJA NA KUFUNGIWA….KOCHA TAIFA STARS AIBUKA NA HILI TENA KUHUSU MOROCCO

Habari za Michezo leo

Aliyekuwa KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania kabla hajafungiwa jana , Adel Amrouche amekiri kwamba mbinu zake za kiufundi zilifeli wakati Taifa Stars ilipokumbana na kipigo kikubwa zaidi cha Afcon ya mwaka huu nchini Ivory Coast kwa kulala 3-0 mikononi mwa Morocco katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi F juzi.

Kabla ya mechi hiyo, Amrouche aliituhumu Morocco kuwa na nguvu kubwa kiasi cha kujichagulia waamuzi wa kuchezesha mechi zao na kuwapendelea, kauli ambayo ililifanya Shirikisho la Soka (TFF), kujiweka kando nayo likisema ni maoni binafsi ya kocha huyo mwenye uraia pacha wa Algeria na Ubelgiji.

Mbinu ya kujilinda ya Amrouche ilisambaratika haraka baada ya kuruhusu bao la nahodha Romain Saiss aliyemalizia mpira wa friikiki ya Hakim Ziyech iliyotemwa na kipa Aishi Manula, kabla ya Azzedine Ounahi aliyeibuka nyota wa mchezo kutupia la pili baada ya kugongeana ‘one-two’ na mwenzake na straika Youssef En-Nesyri kumalizia la tatu ambalo lilihitaji kuangaliwa katika VAR na kutolewa uamuzi wakati staa huyo akiwa ameshafanyiwa ‘sub’ na hivyo kushangilia akikumbatiwa na wenzake akiwa ameshakaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba.

“Mbinu yetu ya mchezo ilifeli. Hatukutarajia matukio haya lakini nawapongeza Morocco kwa kiwango walichoonyesha na matokeo waliyopata,” alisema Amrouche baada ya mechi.

Kocha huyo alisema ubora wa Morocco ulileta tofauti kubwa katika mechi yao juzi.

“Ubora wa wachezaji wa Morocco ulileta tofauti kubwa na walistahili kushinda,” alikiri Amrouche.

Majeraha kabla ya mechi pia yaliathiri matumaini ya Tanzania kwa mujibu wa kocha huyo.

“Tulitaka matokeo mazuri lakini pia nilikuwa na majeruhi wengi sana jambo ambalo lilituathiri. Kisha tukafanya na makosa binafsi,” alifafanua Amrouche.

Lakini kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya alisema Tanzania bado ina nafasi ya kufuzu hatua ya 16-Bora.

“Najaribu kuendelea kuwa na matumaini. Tutarekebisha makosa yetu tuliyoyafanya katika mechi mechi hii na kuwa makini na mechi zijazo,” alisema Amrouche.

“Haitakuwa kazi rahisi lakini bado nafasi tunayo.”

Tanzania mechi ijayo itawakabili mabingwa wa Afcon wa 2012, Zambia Jumapili hii ya Januari 21 katika mechi muhimu ya kundi.

SOMA NA HII  JINSI GUU LA PACOME LILIVYOZUA BALAA KWA CR BELZOUIDAD....MAKOCHA WOTE KICHWA CHINI...