Home Habari za michezo HIKI HAPA KIKOSI CHA ‘MAPRO’ WA TZ WANAOWEZA KUTIKISA AFCON 2023 NA...

HIKI HAPA KIKOSI CHA ‘MAPRO’ WA TZ WANAOWEZA KUTIKISA AFCON 2023 NA TAIFA STARS…

Habari za Michezo leo

KOCHA wa Taifa Stars, Adel Amrouche anaweza kuwa na machaguo mengi ya kikosi cha kwanza kwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania, yote hiyo ni kulingana na idadi kubwa ya mastaa hao ambao wapo kwenye orodha ya wachezaji 27 waliopo Ivory Coast kwa ajili kuipeperusha Bendera ya Tanzania kwenye fainali za Afcon.

“Ni jambo zuri kuwa na wachezaji ambao wanacheza nje maana huongeza uzoefu wao kwenye timu kwa kushirikiana na wale ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye ligi ya ndani, nafurahishwa na maendeleo ya timu, bado tuna kazi ya kufanya,” anasema kocha huyo.

Kikosi hiki cha Taifa Stars ndicho chenye idadi kubwa zaidi ya wachezaji ambao wanacheza nje ya nchi 14 ukilinganisha na kile kilichopita ambacho kilishiriki Afcon ya Misri 2019 kikiwa na wachezaji tisa tu ambao walikuwa ni Hassan Ramadhan (Nkana, Zambia), Himid Mao (Petrojet, Misri), Thomas Ulimwengu (Js Saoura, Algeria).

Wengine walikuwa ni Adi Yussuf (Blackpool, England), Simon Msuva (Difaa El Jadida, Morocco), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Yahya Zayd (Ismaily, Misri), Mbwana Samatta (Krc Genk, Ubelgiji) na Farid Mussa aliyekuwa akiichezea CD Tenerife ya Hispania.

Kati ya wachezaji hao ni watatu tu ambao wamepenya na kuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars ya sasa ambayo inaenda Ivory Coast ambao ni Samatta, Msuva na Himid.

Hapa leo tunakuletea mtoko wa wachezaji wa Stars ambao wanacheza nje ya Tanzania.

KWESI KAWAWA

Amrouche alimpa nafasi kwa mara ya kwanza kipa huyo anayeichezea Karlslunds IF ya Sweden kwenye mchezo wa mwisho ambao Taifa Stars ilicheza kuwania nafasi ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco.

Licha kuruhusu mabao mawili kwenye mchezo huo, Kawawa alionyesha kuwa na kitu hivyo ana nafasi kutoa changamoto ya namba mbele ya Aishi Manula ambaye tangu atoke majeruhi bado hajawa kwenye kiwango chake bora kilichozoeleka.

MNOGA/ MIANO

Hivi karibuni Haji Mnoga ambaye anaichezea Aldershot Town kwa mkopo, amekuwa akitumika zaidi na kufanya vizuri upande wa beki ya kulia kiasi cha wadau kuacha kulalamika kuhusu kuachwa kwa Shomary Kapombe kwenye kikosi hicho.

Kwa sasa Mnoga atakumbana na changamoto ya namba kutoka kwa Miano ambaye anacheza soka la kulipwa Hispania, kabla ya kwenda Misri, mzaliwa huyo wa Uholanzi alikiwasha akiwa na Kilimanjaro Stars kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes kwenye ufunguzi wa Uwanja wa New Amaan Complex.

NOVATUS DISMAS

Akiwa Tanzania alizichezea Biashara United na Azam FC na alizoeleka akitumika katika nafasi ya kiungo lakini kwa sasa amebadilishwa na kuwa beki wa kushoto upande ambao kwenye kikosi cha Taifa Stars amekuwa akifanya vizuri Mohammed Hussein.

Novatus ambaye anaichezea FC Shakhtar Donetsk ya Ukraine amekuwa akifanya vizuri katika nafasi hiyo kiasi cha Hussein wa Simba kipindi fulani kupigwa chini kwenye kikosi hicho na Stars ilifanya vizuri bila ya kuwa na beki huyo wa Wekundu wa Msimbazi.

ABDI BANDA

Hii ingekuwa Afcon yake ya pili lakini utovu wa nidhamu ulimgharimu 2019 na kupigwa chini na kocha wa wakati huo wa Taifa Stars, Emmanuel Amuneke.

Pamoja na kupigwa kwake chini, beki huyo wa Richards Bay ya Afrika Kusini aliitakia kila la kheri Taifa Stars na kufanyia kazi kile kilichotokea na mwishowe akarejeshwa Stars na sasa yupo kwenye nafasi ya kucheza michuano hiyo mikubwa kabisa Afrika upande wa timu za taifa.

HIMID MAO

Ni nadra sana kumwona Himid akitumika eneo la beki wa kati lakini anamudu vizuri tu kucheza hapo kama atahitajika akiwa Misri ambako anacheza soka la kulipwa amewahi kucheza nafasi tofauti ikiwa pamoja na hiyo.

Uzoefu wake unaweza kuwa msaada kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kinaonekana kutawaliwa na idadi kubwa ya vijana. Hii ni Afcon yake ya pili.

MORICE ABRAHAM

Umri wake unaruhusu lakini ana kazi ya kufanya kutokana na ubora wa wachezaji ambao wanacheza kwenye nafasi ya kiungo mkabaji, ambao ni pamoja na Mudathir Yahya wa Yanga na hata Feisal Salum wa Azam naye anaweza kucheza nafasi hiyo.

Kinda huyo anayecheza soka la kulipwa Serbia akiwa na Novi Sad ni kati ya wachezaji wa kutazamwa kwenye mashindano hayo kwani ni mzuri wa kufanyia kazi maelekezo ya kocha na Amrouche amewahi kumsifia.

CHARLES M’MOMBWA

Ni miongoni mwa maingizo mapya kwenye kikosi cha Taifa Stars inaelezwa kwamba haikuwa kazi nyepesi kumshawishi winga huyo anayecheza soka la kulipwa Australia kuichezea Tanzania maana pia ana asili ya DR Congo.

M’mombwa ambaye anaichezea Macarthur FC ana furaha na uchaguzi wake maana anaenda Afcon kuweka historia, amekuwa akitumika mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Amrouche. Alifunga bao zuri la ushindi wa Stars wa 1-0 dhidi ya Niger katika mechi ya kundi E la kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Novemba 18, 2022 ikiwa ni mara yake ya kwanza kuitumikia Stars.

TARRYN ALLARAKHIA

Huyu anaweza kuwashangaza wengi, uwezo wake ni mkubwa. Anacheza vizuri eneo la kiungo mchezeshaji, pia anaweza kushambulia akitokea pembeni, amekomaa kiushindani.

Tarryn amezaliwa na kukulia Uingereza kama Mnoga vile, anaichezea Wealdstone. Alianza maisha yake ya soka akiwa na Leyton Orient kabla ya kujitafuta sehemu nyingine ambako kumemfanya kupiga hatua hadi kupata shavu Tanzania.

MBWANA SAMATTA

Ndiye nahodha wa Taifa Stars, anatajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi wa kutazamwa kwenye fainali hizi za mataifa ya Afrika huko Ivory Coast.

Ni mzoefu ambaye amefanya makubwa huko barani Ulaya akiwa na Krc Genk, Aston Villa ya Ligi Kuu England kabla ya kwenda Fenerbahce ya Uturuki lakini kwa sasa yupo zake Ugiriki ambako anaichezea PAOK.

MSUVA/ KACHWELE

Siku chache zilizopita Msuva alipewa ‘Thank You’ na JS Kabylie ambayo alikuwa akiichezea huko Algeria baada ya kushindwa kuonyesha makali yake akiwa na timu hiyo lakini pamoja na hilo nyota huyo amekuwa msaada kwenye kikosi cha Stars.

Msuva kwa sasa amekuwa akitumika zaidi kwenye eneo la kati la ushambuliaji na amekuwa na maelewano mazuri ya kiuchezaji na Samatta ambaye amekuwa akiongoza safu hiyo tofauti na zamani na alikuwa akitokea pembeni. Kachwele ambaye ametokea Canada ana nafasi ya kutoa changamoto ya namba.

BEN/OMAR

Muda mwingine Ben Starkie anayeichezea Basford United ya England amekuwa akicheza eneo la mwisho la ushambuliaji, pia ni mzuri akitokea pembeni.

Kama ilivyo kwa Ben, Mohammed Omar ambaye naye anacheza soka la kulipwa England akiwa na Boreham Wood ana uwezo wa kucheza nafasi hizo.

Credit:- Mwanaspoti

SOMA NA HII  LEO NDIO LEO.....BENCHIKHA AMALIZA KAZI MAPEMA...KOCHA AL AHLY AINGIA UBARIDI WA GHAFLA...