Home Habari za michezo MASTAA TAIFA STARS KULAMBA BIL 1.3 WAKIMFUNGA DR CONGO LEO….

MASTAA TAIFA STARS KULAMBA BIL 1.3 WAKIMFUNGA DR CONGO LEO….

Taifa Stars

Wachezaji na benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wameahidiwa Dola 500,000 za Marekani (takriban Sh1.3 bilioni) endapo itafuzu hatua ya 16 bora ya fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Taifa Stars leo itapambana na DR Congo kuanzia saa 5.00 usiku kwenye Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Karhogo katika mchezo wa mwisho wa kundi F.
Mchezo mwingine wa kundi hilo utaikutanisha Morocco dhidi ya Zambia ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro.

Mpaka sasa, hakuna timu katika kundi hilo ambayo imefuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora ambapo mechi za usiku huu zitatoa picha halisi ya timu zipi zitaingia hatua hiyo ya mtoano.

Morocco inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne ambapo inahitaji sare na Zambia ili ifuzu hatua inayofuata.

Taifa Stars inahitaji ushindi dhidi ya DR Congo huku ikiomba Morocco ipate ushindi dhidi ya Zambia au zitoke sare ili ipate nafasi hiyo. Kwa sasa Stars ina pointi moja ambapo DR Congo na Zambia zimekusanya pointi mbili kila moja.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwanaspoti, leo, Januari 24, 2024, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema ahadi hiyo ya fedha imetolewa ili kuongeza hamasa kwa wachezaji.

Dk Ndumbaro amesema kuwa ahadi hiyo imetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na anaamini kuwa wachezaji watapambana mpaka tone la mwisho ili kushinda na kuiweka Tanzania katika ramani mpya ya soka.

SOMA NA HII  KUHUSU UVUMI WA KUMKATAA FEI TOTO...NABI AIBUKA NA KUANIKA KILA KITU WAZI...