Home Habari za michezo WAKATI DIARRA AKIRUDI TZ KESHO…UKIMYA WA AZIZ KI WAIBUA MASWALI YANGA….

WAKATI DIARRA AKIRUDI TZ KESHO…UKIMYA WA AZIZ KI WAIBUA MASWALI YANGA….

Habari za Yanga leo

Ikithibitishwa kuwa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diara anarudi leo tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara akianza na Tanzania Prisons, wingu limetanda juu ya ujio wa Stephane Aziz Ki.

Wakati ikithibitika kipa huyo kutua leo,  kutoka katika mapumziko mafupi baada ya kumaliza kibarua cha mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), Ivory Coast alikokuwa na timu ya taifa lake ya Mali, upande wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Aziz Ki bado haijajulikana atawasili lini nchini.

Aziz Ki aliyekuwa na kikosi cha Burkina Faso katika Afcon, waliondolewa katika hatua za makundi na baada ya kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mali ambayo iling’olewa katika hatua ya 16 bora.

AZIZ KI APANGUA KIKOSI

Wakati langoni kukiwa hakuna shida upande wa eneo la kiungo mshambuliaji kulikuwa na mabadiliko makubwa tofauti na ilivyozoeleka ambapo kocha Miguel Gamondi amekuwa akiwatumia Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua.

Na mabadiliko hayo yameonyesha upungufu mkubwa hasa kwa timu kukosa kiungo ambaye anaweza kuichezesha kama ilivyozoeleka kwa Aziz Ki.

Kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Hausung kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi cha Yanga, kocha akitumia zaidi wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Pia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambao waliambulia suluhu baada ya dakika 90 kumalizika, Gamondi alimtumia Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akicheza sambamba na Pacome na Maxi lakini pengo la Aziz Ki lilionekana hasa timu hiyo ilipopata mipira ya adhabu mitatu karibu eneo la 18 ambayo haikuzaa bao.

Ndani ya kikosi hicho Aziz Ki amejitengenezea ufalme katika upigaji mipira iliyokufa, ambapo mara nyingi imekuwa ikisababisha mabao upande wa Yanga au kuchangia kupatikana bao.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimesema  kuwa kipa namba moja, Diarra ataungana na timu Alhamisi huku kikiri kuwa hadi sasa hawafahamu Aziz Ki atarudi lini licha ya kuondolewa mapema.

“Kwa taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba Diarra Alhamisi ataungana na timu na atakuwa sehemu ya wachezaji watakaosafiri kwenda Mbeya kwa ajili ya mchezo wetu na Tanzania Prisons,” kilisema chanzo hicho.

“Kuhusu Aziz Ki bado sijafahamu kwani sina taarifa yoyote juu ya kurejea kwake ngoja tuone kama yeye pia atauwahi mchezo wa Mbeya.”

Mwanaspoti ilifanya jitihada za kumtafuta mchezaji huyo ambapo licha ya ahadi ya kutoa majibu jana juu ya kurejea kwake baada ya mawasiliano, lakini baadaye simu yake haikupokewa wala hakujibu ujumbe mfupi aliotumiwa.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu ya hiyo, Ally Kamwe amesema wachezaji hao wote watarudi siku mbili hizi kuanzia kesho.

“Tumewakosa kwenye mechi tatu Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na mechi za ligi mbili dhidi ya Kagera Sugar ugenini tukiambulia suluhu na mchezo dhidi ya Dodoma, nafikiri siku mbili hizi watarudi na kuungana na wenzao,” amesema.

Kukosekana kwa Diarra langoni kwenye mechi tatu wamecheza makipa wanaokuwa benchi akianza Aboutwaleeb Mshery dhidi ya Hausung kwenye ASFC akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja baada ya ushindi wa mabao 5-1, kisha Metacha Mnata aliyedaka kwenye mchezo na Kagera Sugar ambao waliambulia suluhu na Mshery tena alidaka dhidi ya Dodoma Jiji katika ushindi wa bao 1-0.

Diarra amejihakikishia namba ndani ya kikosi cha Yanga ambapo panga pangua, akiongoza jahazi la wababe hao wa Jangwani tangu alipotua nchini misimu miwili iliyopita.

SOMA NA HII  SIMBA MAJANGA MATUPU KWA UPANDE WA MASTAA WAZAWA...UKWELI MCHUNGU HUU HAPA..