Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kutoka East Africa radio, Samwel Rashid mwenyewe anajiita Wakanda Republic amesema kuwa hakubaliani na maamuzi ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo kati ya Simba Sc dhidi ya Mtibwa Sugar uliokuwa umepangwa kupigwa jana Februari 18, 2024.
Simba iliomba kusogezwa mbele kwa mchezo huo kutokana na sababu kuwa itakuwa na safari ya kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wao wa marejeano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya ASEC mimosas, utakaopigwa Februari 23.
“Mimi sikubaliani na hii kitu (Simba kuahirisha mechi), ni kitu ambacho bodi ya ligi wanatakiwa kuachana nayo, mchezo wa CAFCL ni tarehe 23 na Simba walitakiwa kucheza (mchezo wa ligi) tarehe 18, kuna gape ya zaidi ya siku 3 hapo.
“Ahmed Ally amesema safari ni masaa 7, hivyo sisi tufanye ni masaa 24, kwa hiyo wangemaliza mchezo Jumapili na wangeweza kuondoka Jumatatu asubuhi ama jioni.
“Mimi ni Mwalimu najua siku 3 zinatosha kujiandaa na mchezo, mimi naamini masaa 72 yanatosha kujiandaa na mchezo ndani ya nchi husika, maana yake watasafiri tarehe 19 hivyo watakuwa na terehe 20, 21 na 22 watakuwa na siku 3 za kujiandaa na mchezo.
“Masaa 72 ndani ya nchi ya Ivory Coast kwa nini yasitoshe kujiandaa na mchezo, hizo siku 3 kwa nini zisitoshe, kwa hiyo bodi ya ligi waache kuzibeba hizi timu kubwa,” amesema Wakanda Republic.