BAADA ya kufanikiwa kwa viungo kufunga sasa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amehamia kuwafua mawinga kutengeneza nafasi ili kuwapa fursa na washambuliaji kufunga mabao ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Hatua hiyo ni baada ya jana Augustine Okrah kutengeneza nafasi za kufunga katika mchezo wa juzi wa kombe la Shirikisho FA, dhidi ya Polisi Tanzania ambapo mshambuliaji mpya, Joseph Guede kufunga mabao 2 ikiwa ni mechi yake ya kwanza kutikisa nyavu.
Gamondi amesema anajivunia sana wachezaji wake wenye uwezo mkubwa, lakini yote hayo ni jinsi gani inaonekana wanafuata yale anayowapa katika uwanja wa mazoezi.
Amesema anaanza kuona washambuliaji wake wakianza kufunguka na kufunga kama ilivyo kwa Guede, huku akimwambia asiwe na presha kwani atafunga mabao mengi, kutokana na mfumo ambao anataka kuutumia.
“Kuna muda tunahitaji kupata mabao kupitia pembeni na leo (juzi) Okrah ameonyesha uwezo huo, Spidi yake na uwezo wa kutengeneza nafasi umeongezeka kitu kwenye timu, naamini atatusaidia mbeleni , mchezaji mzuri na washambuliaji watatamani kucheza na winga huyo wakiamini pasi ya bao itakuja tu,” amesema Gamondi.
Ameongeza kuwa awali walipata mabo kupitia viungo hali imeanza kubadilika kwa kutumia winga wameweza kufunga kwa Guede kutupia mabao mawili katika mchezo huo wa FA.
Gamondi amesema mechu hiyo imekuwa sehemu ya kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji hawakuonekana sana uwanjani na kupewa nafasi kwa kucheza vizuri na kutengeneza maandalizi ya mechi ijayi.
“Kuhusu kutengeneza nafasi tunazipata nyingi, ukiangalia mechi ya Morogoro tulitengeneza nafasi zaidi ya 10 lakini tukakapata bao 3, ninaimani tutaendelea kutengeneza nafasi na kutumia katika mechi zijazo kuweza kufunga idadi ya mabao mengi,” amesema Kocha huyo.
Kuhusu maandaliz ya mechi yao ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya CR Belouizdad, Gamondi amesema wanataraji kufanya vizuri katika mchezo huo kwa sababu malengo yao ni kusonga mbele.
“Utaratibu wangu nafanya maandalizi hatua kwa hatua baada ya mechi hii tunarejea uwanjani kujiandaa na mchezo dhidi ya CR Belouizdad. Tulitaka kufuzu kucheza makundi tukafanikiwa baada ya miaka mingi na sasa tunataka kutafuta matokeo mazuri yenye ushindi mkubwa ili mwisho wa siku tukacheza robo, “ amesema Kocha huyo.
Wakati huo huo Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mechi ijayo kuhakikisha wanalipa kisasi dhidi ya CR Belouizdad.
“Wapinzani wetu wametua nchini leo (jana) wapo hapa nchini kwa ajili ya mechi ya Jumamosi, kwa upande wetu tuko vizuri, kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi, siku hiyo,” amesema Kamwe.