Home Habari za michezo BAADA YA GAMONDI KUMALIZANA NA YANGA….NI ZAMU YA BENCHIKHA KUONYESHA UMWAMBA …

BAADA YA GAMONDI KUMALIZANA NA YANGA….NI ZAMU YA BENCHIKHA KUONYESHA UMWAMBA …

Habari za Simba leo

Yanga juzi Jumamosi usiku ilitisha sana. Ilitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe sana baada ya kuwachakaza mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu ya Algeria, CR Belouizdad kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kilikuwa ni kisasi kitamu baada ya Yanga kulala 3-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Waarabu hao kule Algeria.

Mechi hiyo iliyopewa jina la ‘Pacome Day’ ikipambwa na wachezaji kadhaa wa Yanga na mashabiki wao kutia rangi kichwani kumuunga mkono staa wao Pacome Zouzoua ambaye ni maarufu kwa kupaka ‘bleach’ nywele zake, ilifanana na kauli mbiu ya siku ya ‘Kitaalamu Zaidi’ baada Wananchi kutembeza boli la kiwango cha juu, na ilikuwa ni bahati kwamba Belouizdad haikufungwa zaidi ya mabao hayo.

Mabao kutoka kwa Mudathir Yahya, aliyefunga bao lake la tano katika mechi zake tano zilizopita alizocheza katika michuano yote, na mengine kutoka kwa Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Joseph Guede yaliifanya Yanga ifuzu hatua ya robo fainali kwa kufikisha pointi 8 katika kundi D ikiungana na vinara Al Ahly ya Misri yenye pointi 9, zote zikiwa zimebaki na mechi moja mkononi.

Yanga na Al Ahly zitavaana Machi 2 nchini Misri katika kuwania timu itakayomaliza kileleni mwa kundi hilo. Belouizdad yenye pointi 5 ndiyo pekee yenye uwezo wa kuzifikia pointi 8 za Yanga endapo itaifunga Medeama katika mechi yao ya mwisho, lakini haiwezi kuwang’oa Wananchi katika nafasi ya pili kwani timu hizo zilipokutana, Yanga imepata matokeo ya jumla ya mabao 4-3.

SIMBA INASAKA 1-0 TU

Simba iliyotoka suluhu ugenini dhidi ya Asec Mimosas juzi usiku jijini Abidjan, Ivory Coast imeendelea kubaki katika nafasi ya pili katika Kundi B ikiwa na pointi 6, sawa na Wydad Casablanca iliyo katika nafasi ya tatu, huku Jwaneng Galaxy ikishika mkia kwa pointi 4.

Wekundu wa Msimbazi wanahitaji ushindi wa japo bao moja tu dhidi ya Jwaneng kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam Machi 2 ili kufuzu katika robo fainali yao ya tano ya CAF katika miaka sita. Simba imecheza robo fainali nne, tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika katika miaka mitano iliyopita.

Ushindi wowote hata wa bao 1-0 utaifanya Simba kuwa na matokeo bora zaidi ya wapinzani wao wa karibu Wydad, endapo wababe hao wa Morocco watashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya vinara Asec Mimosas, ambao walifuzu mapema kabla ya kucheza mechi zao mbili za mwisho, ambao wana pointi 11 na wamejihakikishia kumaliza kileleni. Simba ilifungwa 1-0 na Wydad siku ya Desemba 9, 2023 kule Morocco kabla ya kuja kuifunga 2-0 Kwa Mkapa Desemba 19, 2023. Hii ina maana Simba na Wydad zikimaliza na pointi sawa, Simba itaenda robo fainali.

Wakati Simba ikisubiri mechi ya mwisho ili kujua hatima yake ya kwenda robo fainali, Yanga imeungana na Al Ahly, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe na Asec Mimosas kwenda robo huku zikisubiriwa timu tatu za mwisho kukamilisha idadi ya timu 8 za hatua hiyo.

Hatua ya robo fainali itaanza rasmi mwisho mwa Machi kwa mechi za mkondo wa kwanza na zile za marudiano zikitarajiwa kupigwa kati ya Aprili 5 na 6 mwaka huu.

Droo ya mechi hizo za mtoano za robo fainali na zile nyingine za nusu fainali hadi fainali yenyewe itakayopigwa Mei 26 inatarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao. Hapa chini ni uchambuzi namna makocha wa Simba na Yanga, Abdelhak Benchikha na Miguel Gamondi kila mmoja akiwa na kazi ya kutimiza matarajio ya timu hizo na ndoto zao binafsi Afrika.

BENCHIKHA HESHIMA

Kocha mkuu huyu wa Simba, anachokitafuta kwa sasa akiwa na klabu hiyo ni heshima tu, kwani tayari alishaandika rekodi mbalimbali kwenye michuano ya CAF kwa ngazi ya klabu.

Msimu uliopita tu, kocha huyo akiwa na USM Alger ya Algeria, alifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutwaa ubingwa kwa kuzidi ujanja Yanga, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2.

Benchikha na USMA ilifaidika na kanuni ya faida ya bao la ugenini baada ya kushinda jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-1, licha ya kukubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani mjini Algiers na kutwaa taji hilo kabla ya kwenda kutwaa taji jingine msimu huu la CAF Super Cup kwa kuifunga Al Ahly, ikiwa ni mara ya pili mfululizo kwake, kwani kabla ya hapo alitwaa 2022-2023 akiwa na RS Berkane ya Morocco.

Hivyo, kwa Simba kutinga robo fainali kwake itakuwa heshima na kuendeleza mafanikio katika soka la Afrika, kwani ameshawahi kucheza hatua hiyo mara kadhaa akiwa na timu nyingine alizowahi kuzinoa nyuma.

Kocha huyo aliyewahi kunyakua tuzo ya Kocha Bora wa Afrika, anatafuta heshima kwa kuipekeka Simba robo fainali kabla ya kuivusha kwenda nusu fainali na itakuwa rekodi kwake na klabu hiyo kwa ujumla, kwani hatua hiyo iliwahi kucheza mwaka 1974 enzi za Klabu Bingwa Afrika, iliyokuja kubadilishwa kimfumo na jina mwaka 1997 kuwa Ligi ya Mabingwa ya sasa.

Rekodi zinaonyesha tangu ajiunge na Simba Novemba mwaka jana, ameiongoza timu hiyo kwenye mechi nne za Ligi ya Mabingwa msimu huu, ikiwamo ile ya 0-0 ugenini dhidi ya Jwaneng, kisha mbili dhidi ya Wydad ya Morocco, ikilala ugenini 1-0 na kushinda nyumbani 2-0 na suluhu ya juzi dhidi ya Asec na sasa anaisubiri Jwaneng wikiendi ijayo.

Katika mechi hizo nne za awali za CAF akiwa na Simba, kocha huyo raia wa Algeria, amevuna jumla ya pointi tano na mabao mawili ya kufunga, huku ikiruhusu bao moja tu, hadi sasa kuonyesha anavyojua kujilinda vyema.

GAMONDI REKODI TU

Tofauti na Benchikha wa Simba, kocha Miguel Gamondi anayeinoa Yanga ameweka rekodi nyingine akiwa na kikosi hicho kwa kuifikisha robo fainali yao ya kwanza tangu mfumo mpya huu wa Ligi ya Mabingwa uanze kutumika mwaka 1998 baada ya awali kuiingiza hatua ya makundi.

Gamondi ambaye aliomba radhi kwa waajiri wake wa zamani CR Belouizdad baada ya kuwatoa kwa kipigo cha aibu juzi cha mabao 4-0, awali aliivusha Yanga kwa kuandika historia mpya kwa kuifunga Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0. Kabla ya hapo Yanga ilikuwa haijawahi kuishinda Al Merrikh katika mechi za CAF ama zile za Cecafa, lakini chini ya Gamondi, Wasudan walikufa 2-0 wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, jijini Kigali, Rwanda kwa mabao ya Kennedy Musonda na Clement Mzize, aliyefunga pia bao pekee pale timu hizo ziliporudiana jijini Dar na Yanga kutinga makundi baada ya miaka 25 tangu ilipocheza mwaka 1998.

Ushindi wa jana wa 4-0 dhidi ya klabu yake ya zamani ya CR Belouizdad ulioipeleka Yanga hatua ya robo fainali ni rekodi nyingine mpya kwa Yanga na kwa kocha huyo kutoka Argentina.

Gamondi alianza na timu mwanzoni mwa msimu na kuiongoza timu hiyo kuvuka raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 7-1 mbele ya Asas ya Djibouti waliyoifumua 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza kisha kushinda 5-1 ziliporudiana, ndipo akaifumua Al Merrikh na kutinga makundi kibabe.

Katika mechi tano za kwanza za makundi, Gamondi ameiongoza Yanga kushinda mechi mbili; 4-0 dhidi ya CR Belouizdad jana na 3-0 dhidi ya Medeama ya Ghana iliyotoka nayo pia sare ya 1-1 ya ugenini kama iliyoipata nyumbani ilipoialika Al Ahly, huku ikipoteza moja kwa mabao 3-0 mbele ya CR Belouizdad.

Kocha huyo amevuna jumla ya pointi nane na mabao tisa ya kufunga na kufungwa matano, lakini akiiwezesha Yanga kufunga jumla ya mabao 19 na kuruhusu sita tu nyavuni mwa timu hiyo kwa msimu huu katika mechi za michuano ya CAF ikiwa ni rekodi kwao kwa Ligi ya Mabingwa.

Tayari Yanga ina hazina kubwa kulinganisha na hali iliyokuwa nayo iliposhiriki makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 1998, kwani msimu huo katika mechi 10 ilizocheza kwenye hatua zote, iliishia kufunga jumla ya mabao 16 na kufungwa 25.

Katika hatua ya makundi kwa mwaka huo, Yanga ilivuna pointi mbili tu zilizotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Manning Rangers ya Afrika Kusini kisha kufungana 3-3 na Raja Casablanca ya Morocco, wakati kwa msimu huu Gamondi alishapata pointi tano (kabla ya matokeo ya mechi ya jana), japo ni mara ya kwanza kufundisha barani Afrika.

Katika mechi za hatua ya mtoano za msimu huo, Yanga ilikusanya mabao 11 ya kufunga na kufungwa sita na kwenye makundi ilifunga mabao matano tu na kufungwa 19 kupitia mechi sita ilizocheza ikiwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo na kupangwa Kundi B pamoja na Asec iliyobeba taji, Manning Rangers na Raja Casabalnca.

KAZI IPO

Makocha hao wote pamoja na kazi nzuri walizofanya hadi sasa, bado wana kazi kubwa kuthibitisha ubora wao wa kuzingiza na kuzifikisha timu hizo mbali kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Tangu Yanga ilipowahi kucheza hatua ya robo fainali enzi za Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 haijawahi kuwa na maajabu kwenye michuano hiyo, japo msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya awali 2016 na 2018 kucheza makundi, pia kuwahi kufika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.

Kwa Simba iliyopo mkononi mwa Benchikha, tangu ilipocheza nusu fainali enzi za Klabu Bingwa mwaka 1974, haijawahi kuifikia tena hatua hiyo, kwani mara nne tofauti, imeishia robo fainali, ikiwamo ya 1994 kabla ya mfumo kubadilishwa na 2018-2019, 2020-2021 na 2022-2023.

Pia imewahi kucheza makundi 2003, mbali na kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 2021-2022 na fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.

Hivyo, Benchikha na kibarua cha kuifikisha Simba mbali ikiwezekana kuifikia rekodi ya mwaka 1974 na hata ile ya 1993 Simba ilipocheza fainali ya CAF, michuano iliyokuja kuunganishwa na ile ya Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika ya sasa.

Kwa aina ya wachezaji ilizonazo timu hizo, inawapa nafasi nzuri Gamondi na Benchikha kufanya kweli, hata hivyo wasitarajie kazi iwe rahisi, kwani wanatakiwa kukaza msuli ili kufika mbali katika michuano hiyo ya Afrika yenye donge nono la zawadi.

MECHI ZIJAZO

Machi 01, 2024

Al Ahly v Yanga (Saa 1:00 usiku)

Belouidad v Medeama (Saa 1:00 usiku)

Machi 02, 2024

Simba v Jwaneng (Saa 1:00 usiku)

Wydad CA v Asec Mimosas (Saa 1:00 usiku)

DONDOO MUHIMU

1974 – Mwaka ambao Simba ilicheza hatua ya nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

1998 – Mwaka ambao Yanga iliandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kucheza makundi Afrika.

2023 – Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho na kulikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria

1993 – Simba ilicheza fainali ya Kombe la CAF (sasa halipo) ikifa mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.

SOMA NA HII  USAJILI WA NABI YANGA SC WAVUJA...WANAOSAJILIWA NA KUACHWA WATAJWA...PABLO AWEWESEKA HUKO..