Home Habari za michezo BAADA YA YANGA KUANZISHA SAFARI….SIMBA KAZI KWENU SASA…MKISHINDWA NI AIBU YENU…

BAADA YA YANGA KUANZISHA SAFARI….SIMBA KAZI KWENU SASA…MKISHINDWA NI AIBU YENU…

Habari za Michezo leo

Mara ya mwisho Yanga kufanya walichokifanya, Benjamin William Mkapa alikuwa katika awamu yake ya uongozi wa nchi hii. Clement Mzize alikuwa hajazaliwa. Ndio, Waingereza walikuwa bado wanakishikilia kisiwa cha Hong-Kong.

Na wamefanya hivyo kwa mbwembwe nyingi. Mbwembwe kubwa za kuiita siku yenyewe ‘Pacome Day (Kitaalamu Zaidi)’. Mashabiki na wachezaji wao wakapaka nywele zao rangi kama anavyofanya staa wao na mhimili mkubwa wa timu, Pacome Zouzoua. Fundi wa mpira.

Wakati wakitinga robo fainali ya michuano hii mfumo ulikuwa tofauti na ulikuwa rahisi kidogo. Ukitinga tu makundi unakuwa umetinga robo fainali. Safari hii wametinga kwa staili ya aina yake huku wakimsaga Mwarabu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kiasi cha kocha kugombana wao na mchezaji wake katika benchi.

Kiasi cha wachezaji kuondolewa uwanjani kupitia njia ya waandishi wa habari wakihofia kupigwa na mashabiki wao wenyewe wenye hasira.

Yanga wametinga kwa staili ya aina yake. Mechi tatu za kwanza ziliwaacha na pointi mbili tu, lakini wametinga robo fainali wakiwa na pambano moja mkononi. Dhidi ya Al Ahly ugenini.

Haikutazamiwa hasa iwe hivi kwa namna Yanga walivyolianza kundi lenyewe. Wamemaliza kundi kwa staili ya aina yake. Mudathir Yahya alianza kwa kupiga simu kama kawaida yake.

Baadaye Aziz Ki, Kennedy Musonda na Joseph Guide wakapokea na kuendeleza maongezi. Yalihitajika mabao manne katika Pacome Day ili kuweza kurudisha zile tatu walizopigwa Algiers na kisha kupata bao la mwisho la kuweka deni lisilolipika kwa Belouizdad.

Kufikia hapo kuna mechi mbili za mwisho za kundi zitachezwa Afrika Kaskazini siku chache zijazo kufunga kundi. Hata kama Yanga wakifungwa na Al Ahly pale Cairo kisha Medeama akachapwa na Belouizdad pale Algiers bado Yanga atasonga mbele kwa sababu kinachoangaliwa endapo wakilingana pointi ni nani alimfunga mwenzake mabao mengi walipokutana. Belouizdad alishinda tatu, Yanga ameshinda nne.

Shukrani ziende kwa Ghalib Said Mohamed. GSM. Ametia pesa. Shukrani nyingine ziende kwa kijana anayeitwa Hersi Said. Rais wao. Hapo kuna mchanganyiko wa pesa na akili. Ndio mchanganyiko uliowaokoa Yanga kutoka katika lile shimo la michango ambayo kocha wao wa zamani, Mwinyi Zahera na nahodha Ibrahim Ajibu walikuwa wakichangisha michango ili walau timu iende Mwanza.

Na sasa wanaweza kuiota nusu fainali. Msimu uliopita walienda fainali ya Shirikisho Afrika kama masihara. Msimu huu walitudanganya kwamba lengo lao lilikuwa kutinga hatua ya makundi. Sidhani kama walikuwa wanasema kweli, bali walikuwa wanashusha kisirisiri matazamio ya mashabiki ili wasijiweke katika presha kubwa.

Wanajua kwamba kama wangeishia katika makundi ni jambo ambalo lisingewafurahisha mashabiki na wao wenyewe. Wanajua kwamba walau hatua ya robo fainali ingewaacha mashabiki katika furaha kwa sababu ndivyo viwango ambavyo mtani wao anavifikia kila uchao. Walitudanganya tu kwamba wanataka kuishia makundi. Sio kweli.

Deni la Yanga limekwisha na sasa bado deni la nchi. Saa 24 kabla Yanga haijafanya walichofanya Simba walikuwa wakihaha katika jiji la Abidjan kukabiliana na ASEC Mimosas. Pambano lilimalizika kwa suluhu, huku Sadio Kanoute alikosa nafasi ya wazi. Pengine leo tungekuwa tunazungumza lugha nyingine.

Suluhu hii inamuacha mnyama akiwa na kazi ndogo tu. Apate ushindi wa nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy katika pambano la mwisho. Hata kama Waydad akishinda pambano la mwisho dhidi ya ASEC bado Simba atapita katika mfumo ule ule ambao umempitisha Yanga. Kwamba Mnyama atapita kwa sababu alimtwanga Wydad mabao mengi kuliko lile moja alilofungwa yeye kule Casablanca.

Sidhani kama Simba watafanya masikhara katika mechi hii. Wana sababu mbili za kutofanya masikhara. Kwanza ni kwamba watani tayari wamepita kwenda robo. Nchi itakuwa na matusi ya namna gani kwao kama wakishindwa kwenda robo fainali halafu kama hivi mtani wao kapita. Matusi yasiyomithilika.

Kila mtu atasahau kwamba katika miaka ya hivi karibuni Simba amecheza sana robo fainali huku Yanga wakiwa hawanusi hata makundi. Kila kitu kitasahaulika na aibu itakuwa kwao. Mlaji ni mla leo mla jana kala nini? Sidhani kama Mnyama atakubali aibu hii kutoka kwa mtani.

Lakini hapo hapo sidhani kama Simba watarudia ile aibu ambayo waliipata wakati ule walipotolewa na Jwaneng kwa masikhara tu kwenye Uwanja wa Taifa. Walikwenda Gaborone wakashinda 2-0 halafu wakarudi Temeke wakafungwa 3-0. Aibu iliyoje.

Mnyama hatakubali ujinga huu. Nadhani ana sababu zote mbili za kutokubali jambo jingine zaidi ya ushindi dhidi ya Jwaneng ambao hawagombei chochote katika mechi za mwisho. Labda atakuja kujaribu kuharibu hali ya hewa kufuatia ahadi za nyuma ya pazia atakazopewa na Wydad.

Hata hivyo, pambano halichezwi mdomoni kwa sababu mpira hautabiriki. Simba wanahitaji kupambana ili tupate timu mbili hatua ya robo fainali. Itakuwa heshima kubwa kwa nchi. Itakuwa heshima pia kwa rafiki zetu wa CAF ambao siku hizi wanapata sababu nyingi za ‘kutupendelea’ katika mambo ya soka. Huenda hata Yanga wakashiriki Super League kama Hersi alivyowahi kutuambia wakati fulani.

Lakini hapo hapo, ukiwa na timu mbili katika hatua ya robo fainali basi uwezekano wa kupeleka moja nusu fainali unakuwa mkubwa. Kwenye wengi ni rahisi mmoja kupenya kuliko kwenye mmoja. Ni suala la kusubiri na kuona pambano la Mnyama na Jwaneng. Huu upande wa Pacome Day umeisha salama.

Ni kama vile unasubiri penzi zito kutoka kwa aliyekukataa siku nyingi lakini siku aliyokubali ukamalizia kwa busu zito.

SOMA NA HII  MWAMBUSI: KOCHA WA MAKIPA AMEPATIKANA