Home Habari za michezo KRAMO ALIVYOWACHOMEA ‘UTAMBI’ ASEC MIMOSAS KWA SIMBA…

KRAMO ALIVYOWACHOMEA ‘UTAMBI’ ASEC MIMOSAS KWA SIMBA…

Habari za Simba leo

Simba SC iko Ivory Coast kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya vigogo wa soka nchini hapo Asec Mimosas lakini Wekundu wa Msimbazi hao wamepewa faili zima la wapinzani wao na Aubin Kramo.

Kramo ni mchezaji wa Simba aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asec Mimosas lakini hakupata nafasi ya kucheza kikosini hapo kutokana na kuandamwa na majeraha, jambo lililowafanya vigogo wa Msimbazi kumwondoa kwenye orodha ya usajili hadi msimu ujao huku wakiendelea kumpa huduma na stahiki zote muhimu akiwa Dar es Salaam.

Simba imemwacha Kramo, hapa nchini lakini imeondoka na maoni yake namna ya kushinda mchezo huo kutokana na uzoefu wake na Asec Mimosas kwani alikulia kwenye akademi ya timu hiyo kabla ya kwenda kupata uzoefu klabu za FC San Pedro na African Sports na baadae kurejea kikosini hapo na kufanya makubwa yaliyowashawishi viongozi wa Simba na kumsajili.

Kramo amesema Asec ya sasa ina wahezaji wengi vijana na wenye ndoto za kusonga mbele zaidi kisoka hivyo watacheza mechi dhidi ya Simba kwa nguvu zote ili kuonekana na kuwataka Simba kuwa makini.

Aidha, Kramo amewaeleza Simba kutumia vyema pengo la mshambuliaji Sankara Karamoko aliyekuwa tegemeo kikosini hapo lakini mwezi Januari akauzwa kwenda Wolfsberger AC ya Austria.

“Asec ni timu nzuri na ina wachezaji wenye uchu wa kufanya vizuri zaidi. Hilo linawapa nguvu ya kupambana kwa dakika zote 90 ili waisaidie timu pia waonekane. Simba ina nafasi ya kushinda. Matumizi ya mapengo yaliyopo kwa Asec yanaweza kuisaidia Simba kushinda na kuongeza alama,” amesema Kramo.

Wakati Kramo akisema hayo, rekodi zinapigilia msumari, Karamoko alikuwa mchezaji hatari zaidi ndani ya kikosi cha Asec kwenye mechi za hatua ya makundi kwani katika mabao saba timu hiyo iliyofunga, amehusika na matano, akifunga manne na kuasisti moja ndani ya dakika 89 pekee alizotumika makundi msimu huu.

Karamoko aliasisti kwenye mechi dhidi ya Simba kwa bao la Serge Pokou lililowapa Asec sare ya ugenini, kisha kufunga bao pekee wakati Wydad ikizimwa ugenini kisha kufunga mabao mawili kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Jwaneng na kutupia moja nyumbani waliporudiana na Jwaneng iliyoifumua 3-0.

Mabao hayo yamemfanya nyota huyo hadi anaondoka Asec ndiye kinara wa mabao wa hatua ya makundi akiwa na mabao manne akifuatiwa na Pacome Zouzoua wa Yanga mwenye mabao matatu, hivyo kuondoka kwake huenda ikawa ni afadhari kwa Simba na sasa itawekeza nguvu nyingi kwenye kuwazuia Pokou na Mofosse Karidioula wasicheke na nyavu licha ya kwamba wamekuwa na kiwango kizuri pia.

Simba leo usiku itafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kesho saa 4:00 usiku kuingia uwanjani kucheza mchezo huo muhimu.

Simba na Asec zipo kundi B, sambamba na Wydad na Jwaneng na Asec inaongoza kundi ikiwa na alama 10, ikifuatiwa Simba yenye pointi tano, Jwaneng ikikaa nafasi ya nne na alama nne huku Wydad ikiburuza mkia na alama tatu.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE: NILISHANGAA SIMBA WALIPOMSAJILI KISUBI...AFUNGUKA ISHU YA NKANE NA YANGA...