Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA MASHUJAA LEO….SIMBA WAANDALIWA MTEGO KAMA WA YANGA…

KUELEKEA MECHI NA MASHUJAA LEO….SIMBA WAANDALIWA MTEGO KAMA WA YANGA…

Habari za Michezo leo

Kikosi cha Simba tayari kimeshatua mjini Kigoma tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa leo dhidi ya Mashujaa, huku mastaa wa timu wenyeji wakichimba mkarwa na kuwahakikisha mashabiki wa mjini humo kwamba kesho ‘mnyama hatoki salama’.

Mashujaa inayocheza Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza itakuwa wenyeji wa Simba katika mechi ya kiporo cha ligi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, huku mashabiki wakilazimika kutoboka Sh3,000 -5,000 kulipa viingilio vya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu.

Katika kujiandaa na mchezo huo, maafande hao waliweka kambi ya wiki mbili jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza usajili wa dirisha dogo na kucheza michezo miwili ya kirafiki , ikianza kwa kuichapa KMC kwa mabao 2-1 kisha kutoka sare ya 1-1 na Namungo na leo watakuwa na kazi ya kuikabili Simba.

Kila timu imetamba kushinda mchezo huo, lakini wenyeji kupitia mastaa wao wamesema wanataka kuanza ngwe ya pili ya Ligi Kuu kwa kuinyoosha Simba ambayo imeingiza mashine sita mpya katika dirisha hilo walioanza kuonyesha makali yao kwenye mchezo wa kiporo cha michuano ya Shirikisho (ASFC).

Simba iliinyoa Tembo FC ya Tabora kwa mabao manne, huku mabao mawili kati yao yakifungwa na nyota wapya akiwamo Saleh Masoud Karabaka na Pa Omar Jobe, wakati mengine yalitupiwa nyavuni na Saido Ntibazonkiza na Luis Miquissone katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar.

Licha ya kukiri pambano hilo ni gumu kutokana na ukweli Simba ni timu kubwa na inayoundwa na mastaa wa kimataifa, lakini Mashujaa imesisitiza inataka kupata ushindi nyumbani ili kujiokoa kutoka eneo la mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu ikishika nafasi ya 15 kati ya timu 16.

Beki wa Mashujaa, Said Juma Makapu, amesema kuwa, kikosi chao kinahitaji ushindi kwenye mchezo huo ambao ni muhimu huku akitamba kuwa maboresho yaliyofanywa dirisha dogo na kambi ya wiki mbili jijini Dar es Salaam umewaimarisha.

β€œKwetu ni mchezo muhimu sana tumejianda vizuri ili kuweza kupata alama tatu, kwakweli kambi yetu ya jijini Dar es Salaam imesaidia kiasi kikubwa sana kwa sababu tumepata mechi nyingi za kirafiki na zimetujenga kuwa imara sana,” amesema beki huyo wa zamani wa Yanga na Ihefu, huku mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Emmanuel Mtumbuka aliyetua dirisha dogo akitokea Stand United ya Shinyanga, amesema anatarajia mchezo huo utakuwa wa kwanza kwake kwenye Ligi Kuu akiwa na uzi wa Mashujaa na endapo atapewa nafasi na benchi la ufundi hatawaangusha.

Mtumbuka tayari ameshaifungia timu hiyo mabao matatu kwenye mechi za kirafiki za maandalizi, ambapo alifunga mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC kisha akatupia bao moja kwenye ushindi wa mabao 7-0 mbele ya Twalipo Academy.

β€œNamuomba sana Mungu anijalie afya njema naamini kwa uwezo wake nitafanikiwa kucheza mchezo wangu wa kwanza, naamini kama nitapewa nafasi nitahakikisha napambana tu na kushirikiana na wenzangu kupata ushindi na nawaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kuisapoti timu yao,” amesema Mtumbuka.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara, lakini zote zikiwa na kumbukumbu kuwahi kukutana mara mbili, ikiwamo mechi ya raundi ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu wa 2018-2019 mechi iliyopigwa Desemba 2018 ambapo Simba iling’olewa kwa kufungwa mabao 3-2 kisha zikakutana tena kirafiki Oktoba, 2019 na Simba kushinda bao 1-0 kwa bao la Sharaf Shiboub.

SOMA NA HII  KOCHA TAIFA STARS AFUNGUKA SIRI NZITO...MECHI DHIDI YA UGANDA...ILIYOWAFANYA WASHINDE