Home Habari za michezo MASHABIKI SIMBA MMEMSIKIA FREDDY HUKO!!!…., HAO JWANENG WAJIPANGE LEO AISEE…

MASHABIKI SIMBA MMEMSIKIA FREDDY HUKO!!!…., HAO JWANENG WAJIPANGE LEO AISEE…

Habari za Simba leo

Mashabiki wa Simba bado hawamuelewi vyema, mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Michael Freddy Koublan aliyesajiliwa katika dirisha dogo kutokana na kushindwa kutupia mipira kambani tofauti na walivyomtumainia kulingana na rekodi alizoandika Zambia alipokuwa anakipiga Green Eagles.

Freddy pamoja na Pa Omar Jobe walisajiliwa dirisha dogo ili kuziba nafasi za Jean Baleke na Moses Phiri ambao waliifungia Simba jumla ya mabao 11, Baleke akitupia manane na Phiri matatu, lakini bado hawajawa na moto mkali jambo linalofanya baadhi ya mashabiki kuwajadili mtaani na mtandaoni.

Hata hivyo, ni kama vile Freddy amezisikia kelele za mashabiki na wapenzi hao wa soka wa Simba kwa kufichua kwa sasa amelishwa mbinu mpya na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha ili aweze kutupia mabao zaidi na kuwaahidi wanasimba kwamba wakae kwa kutulia na uhondo unakuja.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast aliyetua Simba akitoka kuitumikia Green Eagles kwenye mechi 17 na kuifungia mabao 14 na asisti nne hadi sasa ameifungia timu hiyo mpya mabao mawili tu, likiwamo moja la Ligi Kuu na jingine la michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Freddy amesema baada ya mechi ya ASFC dhidi ya TRA ambapo Simba ilishinda mabao 6-0, alikaa na Kocha Benchika kikao cha muda mfupi na kumwambia mambo yatakayomfanya kuwa bora zaidi ya alipo sasa ili kuwapa furaha mashabiki wa klabu hiyo.

Freddy amesema kwanza Benchikha alimwambia aachane kabisa na kelele za mashabiki, kwani kupoteza nafasi ya mabao uwanjani ni kitu cha kawaida kwa mchezaji, japo yapo mambo ya kuzingatia kwa upande wake ili awe bora na kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kocha aliniambia nina uwezo na akili ya kufunga ila shida ni moja tu ya kukosa utulivu ninapopata nafasi, jambo ambalo linasababisha kukosa mabao kizembe, kitu kizuri ni kwamba kocha ameonyesha kuniamini na kusema huu ni mwanzo wangu wa kufunga na ananiona mbali zaidi,” amesema Freddy mwenye umri wa miaka 25 na kuongeza;

“Kwangu naiona nafasi ya kushinda mechi ijayo ya Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ni kubwa, kwani sitarudia makosa ya kupoteza nafasi yoyote itakayotokea mbele yangu. Najua ni mechi muhimu na tunataka matokeo mazuri ya kutuvusha robo fainali.”

Freddy aliyewahi kuwika na timu kadhaa zikiwamo za AS Port Louis ya Shelisheli, Ferroviario de Nacala ya Msumbiji na Desportivo da HuĂ­la ya Angola ameongeza kwa kusema; ‘Kwa mazoezi ninayoendelea nayo, naamini Simba tunaenda kuwasapraizi mashabiki kwa kutinga robo fainali tukiwa nyumbani kwa ushindi mzuri na kulipa kisasi cha misimu miwili iliyopita.”

Ushindi wa Simba kwenye mechi ya leo ya kufungia Kundi B itaiwezesha kufikisha pointi tisa na kumaliza ya pili nyuma ya Asecv Mimosas ya Ivory Coast iliyotangulia, lakini matokeo hayo yanaweza kumfanya mshambuliaji huyo kujenga kujiamini zaidi kikosini.

Licha ya rekodi mbaya iliyonayo Simba kwa kufungwa mabao 3-1 nyumbani na Jwaneng katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2021/2022 na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini licha ya kushinda ugenini 2-0 kwa mabao Joh Bocco, nyota huyo na wenzake kikosini wametamba wamejiandaa kufanya kweli na kulipa kisasi.

Mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku sambamba na ile ya Asec dhidi ya Wydad itakayopigwa mjini Casablanca inapaswa Simba kutoingia uwanjani kwa kujiamini na badala ya kupambana mwanzo ili ipate ushindi na kuwafuata watani wao Yanga.

SOMA NA HII  RUSHA KETE NA UJIPATIE MSHIKO WA KUTOSHA KUTOKA KASINO YA MTANDAONI YA MERIDIANBET....