Home Habari za michezo MUSEVEN, SAMIA WATUNISHA MSULI MICHUANO YA CECAFA…

MUSEVEN, SAMIA WATUNISHA MSULI MICHUANO YA CECAFA…

Habari za Michezo

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda wamejitokeza kudhamini Michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’.

Museveni ametoa Dola za Marekani laki tatu kudhamini mashindano ya Chalenji upande wa wanaume huku Rais Samia akitoa Dola 100,000 kudhamini Michuano ya timu za soka za taifa za wanawake kwenye ukanda wa ‘CECAFA’.

Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ Wallace Karia jijini Dar es salaam.

Amesema awali Rais Samia alitoa kiasi hicho cha fedha kudhamini Ligi ya Mabingwa ukanda wa ‘CECAFA’ lakini kuepusha mgongano wa kimaslahi na wadhamini wa Shirikisho la Soka la Afrika ‘CAF’ kampuni ya Total Energy wameamua kupeleka fedha hizo kudhamini timu za soka za taifa za Wanawake ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mkutano Mkuu umeamua kuhamisha zawadi ya Rais Samia ya Dola 100,000 kwenda kudhamini mashindano ya timu za taifa za wanawake kuepusha mgongano wa kimaslahi na Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ na kampuni ya Total Energy inayodhamini Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Karia

Aidha, Karia amesema Rais Museveni ameweka Dola 300,000 kudhamini Michuano ya Kombe la Chalenji kwa Wanaume ambazo zitatumika kununua medali na kutoa zawadi kwa washindi kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Zanzibar baadae mwaka huu.

Kuhusu Kombe la Kagame, amesema kalenda inasumbua kufanyika kwa mashindano hayo kutokana na kufika mbali kwa klabu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na zaidi wataomba kukutana na Rais Kagame kuona namna ya kuboresha udhamini wake wa Dola 60,000 uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kwenye michuano hiyo.

SOMA NA HII  KMC WATIBULIWA MIPANGO YAO,NGOMA INAPIGWA KARATU