Home Habari za michezo MIKATABA YA CHAMA, AZIZI KI PASUA KICHWA SIMBA NA YANGA….LOLOTE LINAWEZA KUTOKEA…

MIKATABA YA CHAMA, AZIZI KI PASUA KICHWA SIMBA NA YANGA….LOLOTE LINAWEZA KUTOKEA…

Habari za Simba na Yanga

Mabosi wa Simba na Yanga kwa sasa wanakuna vichwa juu ya nyota wa timu hizo ambao mikataba inaelekea ukingoni huku wakiwa hawajaanza mazungumzo ya kuwaongeza mipya, jambo linalotia hofu kwamba hadi mwishoni mwa msimu lolote linaweza kutokea kwao.

Hofu hiyo inaongezekana kutokana na wachezaji hao kuwa kwenye kiwango kikubwa, huku baadhi wakitajwa kunyemelewa na klabu pinzani na hapo ndipo mabosi wanapohaha kupambana ili kuwabakisha, lakini wakitakiwa kujiandaa kuvunja benki ili kuwazuia iwapo hawataki waondoke.

Inaelezwa kwamba kiungo mshambuliaji wa Yanga anayeongoza kwa mabao klabuni, Stephane Aziz KI mkataba wake upo ukingoni, wakati kule Msimbazi majina ni mengi, lakini anayeshtua zaidi ni Clatous Chama ambaye hivi karibuni alipotoka fainali za Afcon 2023 ameonekana kuwa na kiwango cha juu klabuni.

Wengine wanaomaliza mikataba Jangwani ni Bakari Mwamnyeto, Kennedy Musonda na Metacha Mnata anayetajwa kuwa huenda akatemwa, Jonas Mkude na Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ aliyesajiliwa kutoka Afrika Kusini.

Kwa upande wa wanaodaiwa mikataba inaisha upande wa Simba ni Aishi Manula, Saido Ntibazonkiza, Kennedy Juma, Shomary Kapombe na John Bocco ambaye inaelezwa umeshaisha na sasa anaendelea kusomea ukocha tayari kuanza kubeba majukumu mengine.

Kwa namna hiyo na presha zinazoendelea chinichini juu ya dirisha kubwa la usajili linalotarajiwa kufunguliwa baada ya kumalizika msimu wa 2023-2024, mashabiki wa klabu hizo na hata wale wa Azam wajiandae tu na sapraizi, kwani lolote linaweza kutokea kama ilivyotokea misimu iliyopita.

Hakuna anayebisha kwamba Aziz KI licha ya kuwepo Yanga, lakini Simba imekuwa ikimmezea mate tangu alipokuwa Asec Mimosas, sema dau lake liliwakimbiza ndipo Yanga na GSM wakambeba misimu miwili iliyopita, huku Yanga wakiota kumsajili kwa muda mrefu Chama tangu alipokuwa Zesco, lakini jamaa alitua Msimbazi.

Katika madirisha matatu ya usajili yaliyopita kulikuwa na tetesi nyingi za Chama kutakiwa na Yanga, lakini mara zote amekuwa akisalia Msimbazi, hivyo kwa namna mikataba waliyonayo nyota hao sio ajabu yakatokea yale ya Ibrahim Ajibu, Bernard Morrison au Haruna Niyonzima walivyopishana katika klabu hizo.

Kabla ya Yanga kuinasa saini ya Ki, Simba ilishindwa kumng’oa Asec Mimosas na mashabiki wake waliishia kuliimba jina lake mdomoni, huku macho yakiona huduma wanayoifaidi wana Jangwani.

Simba inaonekana haijakubali kushindwa baada ya kusikia mkataba wa Ki unatamatika mwisho wa msimu huu, wanafuatilia ishu yake kwa ukaribu ili kuhakikisha wanamsainisha msimu ujao (2024/25).

Vigogo wa Simba wakiwa na mtazamo huo juu ya Ki, Yanga haijapoa inahitaji kumuongezea mkataba mpya, ila staa huyo inaelezwa anawasubirisha.

Kiwango cha Ki kimewaka akiwa amefunga mabao 10 akishushwa hivi karibuni na Feisal Salum wa Azam aliyefunga 12 na ambaye usajili wake kutoka Yanga kwenda Azam ulikuwa na sapraizi na sasa inaelezwa si ajabu akiibukia Msimbazi kunakotajwa ndiko ilikokuwa shabaha yake ya awali kabla ya mambo kumbana.

Kama kawaida timu hizo zilivyo na ushindani kuanzia ndani hadi nje ya uwanja, Yanga imekuwa ikihusishwa kuhitaji huduma ya Chama na bado haijakata tamaa katika hilo.

Kila mkataba wake unapomalizika, Simba inakuwa inatumia nguvu kubwa kumbakiza, ikihofia Yanga kumchukua. Chama hadi sasa anamiliki mabao manne na asisti nne kwenye Ligi Kuu.

Lolote linaweza likatokea kwenye klabu hizo, miaka ya hivi karibuni Simba iliwasajili Morrison, Niyonzima, huku Yanga ikimchukua Ajibu na ilibaki kidogoimalizane na mabeki Shomari

Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, hilo lilishindikana baada ya wana Msimbazi kushitukia dili mapema. Hesabu kubwa zikiwa zimekaa kwa mastaa hao, usajili ujao kwa ujumla unaweza ukawa wa kishindo kikubwa.

Tetesi zinaeleza kwamba kipa wa Simba, Manula baada ya kuponea chupuchupu dirisha dogo, ila lijalo kama akiendelea na kiwango anachoonyesha njia ya kuondoka inaweza ikawa nyeupe kwake.

Tofauti na mwanzo ambapo kuligawanyika makundi mawili ya viongozi wengine wakimtaka aendelee kusalia, ila kwa sasa ni asilimia 75 wapo tayari aondoke, ikitajwa Azam FC ndiyo inayohitaji huduma yake.

Tayari limeanza sekeseke la Prince Dube, licha ya uwepo wa tofauti na mabosi wa Azam ambazo haziwekwi wazi, ila inatajwa Yanga inamnyemelea kutaka huduma yake na kuna asilimia kubwa mambo yakienda sawa akajiunga nayo.

Ukiachana na Dube, taarifa za ndani zinasema kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anapigiwa hesabu ya kuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao.

WASIKIE WADAU Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema mchezaji hana makazi ya kudumu kwenye timu, hivyo ikitokea yeyote kati ya wanaotajwa kuviziwa na timu nyingine wala haitashutua sana.

Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Amir Maftah alisema: “Ukiona mchezaji anatajwa huku na kule, ujue ameonyesha kazi nzuri na inakuwa ni sehemu yao ya kutengeneza pesa.”

SOMA NA HII  KISA RATIBA YA LIGI KUU...KOCHA MKUU SIMBA AIBUKA HILI JIPYA...AVUNJA UKIMYA KUHUSU MECHI NYINGI ZA 'HOME'....

1 COMMENT