Home Habari za michezo KWA TAKWIMU HIZI TU….HUYU MUDATHIRI ATAFUNGA SANA MSIMU HUU….

KWA TAKWIMU HIZI TU….HUYU MUDATHIRI ATAFUNGA SANA MSIMU HUU….

Habari za Yanga leo

Kwa sasa anajiita ‘mtambo wa mabao’. Hii ni kwa sasabu amekuwa akifunga karibu kila mechi na licha ya kwamba haimbwi sana kama ilivyo kwa Pacome Zouzoua, hakuna ubishi namba zinambeba.

Si mwingine, ni Mudathir Yahya Abbas. Kiungo fundi mwenye sifa ya kubadilika kila mchezo. Amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Jangwani na amewapa furaha kwa kiasi kikubwa na huwaambii kitu kwa sasa wakiamini kila anapocheza lazima atupie hasa kwenye uwanja wa nyumbani wa Azam Complex, Chamazi na wakampa jina la ‘King of Chamazi’.

Mudathir aliyejiunga na Yanga dirisha dogo la msimu uliopita akitokea KMKM ya Zanzibar alikokuwa akifanya mazoezi baada ya kuachana na Azam FC, amefichua siri ya mabao yake na kazi yake nzito anayofanya uwanjani na licha ya namba zake kuonyesha balaa lake amesema atafunga sana kama ataendelea kupata nafasi kikosini.

Kabla ya kujiunga na Yanga kiungo huyo alikuwa anatajwa na Simba na Singida Big Stars lakini wanajangwani ndio waliofanikiwa kuinasa saini yake kwa kumsainisha miaka miwili.

Chini ya Kocha Nasriddine Nabi alipata namba akicheza kama kingo mkabaji na mshambuliaji, hata hivyo, hakuwa na namba nzuri kwenye kupachika mabao na alifunga mawili tu ndani ya miezi sita kwenye mechi za ligi, Yanga wakiibuka mabingwa.

Mbali na ubingwa huo, pia Mudathir alivaa medali za Kombe la Shirikisho Afrika ilipocheza fainali dhidi ya USM Algers.

Kwenye michuano hiyo, Mudathir alifunga bao moja na lilichagulia ‘Bora la hatua ya makundi. ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bao hilo alilifunga dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye ushindi wa mabao 3-1, Februari 19, kwenye Uwanja wa Benjamín Mkapa, Dar es Salaam.

Mudathir aliwashinda wachezaji wengine waliofunga dhidi ya timu za DRC, Aymen Mahious wa USM Alger kwa bao alilofunga dhidi ya St. Eloi Lupopo, Aubin Kramo Kouamé wa ASEC Mimosa ya Ivory Coast kwa bao alilofunga dhidi ya Diables Noirs na Paul Acquah wa Rivers United kwa bao alilowafunga DC Motema Pembe.

Kwenye ligi Muda alifunga mabao mawili pekee hii ni kutokana na kuchezeshwa zaidi nafasi ya kiungo mkabaji tofauti na msimu huu ambao amekuwa akitumika nafasi tatu tofauti, namba nane, 10 na sita na kote akipangwa anafanya vizuri.

MSIMU HUU Kiungo huyo hakuwa na namba nzuri mzunguko wa kwanza kutokana na kukosa nafasi kikosi cha kwanza licha ya kuanza kufunga kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya KMC wakiibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Katika mechi saba za Yanga za hivi karibuni, imeshinda sita na sare moja, huku Muda akifunga mabao matano na kuisaidia timu yake kushinda.

Mechi hizo ni dhidi ya Tabora United (1-0) akifunga Aziz Ki, Kagera Sugar (0-0), Dodoma Jiji (1-0) mfungaji Mudathir, dhidi ya Mashujaa (2-1) wafungaji Maxi Nzengeli na Mudathir, Tanzania Prisons (2-1) Clement Mzize na Pacome Zouzoua.

Wakati dhidi ya KMC (3-0) Mudathir alifunga mabao mawili huku moja likifungwa na Pacome na mechi dhidi ya Namungo wakishinda mabao 3-1 amefunga bao moja huku mengine yakifungwa na Aziz Ki na Mzize na jumla kwenye mechi 17 zilizochezwa na timu yake amefunga mabao saba akitumika kwa dakika 1242.

Kiraka huyo chini ya Gamondi ameifungia timu yake bao moja kimataifa kwenye mchezo dhidi ya CR Belouizdad, Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 na kutinga robo fainali.

GAMONDI, MUDATHIR WATIA NENO

Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema, “Mudathir licha ya kufunga pia ni kiungo ambaye anaweza kukaba, kutengeneza mashambulizi na kufunga, hivyo ni mzuri akicheza namba sita, nane, 10 na saba,” anasema na kuongeza;

“Nafurahishwa na namna anavyocheza na ni mchezaji msikivu, ukimwelekeza nini cha kufanya anafanya hivyo hivyo, suala la kuanza au kuanzia benchi hilo ni jukumu langu.”

Gamondi amesema amekuwa akimtumia katika nafasi tofauti kulingana na mchezo na anasaidia kumpatia matokeo hivyo ni mchezji muhimu kikosini kwake.

Mudathir amesema anafurahia kucheza katika nafasi yoyote anayopangwa kikubwa ni kuona anapata nafasi kikosi cha kwanza na kucheza kwa kutoa mchango.

“Watu hawafahamu, naomba kuwafahamisha nafunga sana kwa sababu nakaa nyuma ya mshambuliaji, muda mwingine nacheza kama winga namba saba, hiyo ndiyo siri ya mabao mfululizo,” anasema na kuongeza;

“Gamondi ananipa majukumu yote uwanjani, kukaba, kuchezesha timu na kushambulia kwa kufika ndani ya boksi, nitafunga sana, nimeambiwa nifanye yote kwa sababu ya uwezo wangu wa kucheza nafasi nyingi uwanjani.”

Mudathir amesema anavyoendelea kupata nafasi kunamwongezea nguvu ya kupambana huku akiamini ataendelea kufanya juhudi zote ili kumthibitishia kocha Gamondi hajakosea kumpa nafasi.

Amesema kwa Yanga ilivyo mchezaji yeyote akipata nafasi atapambana ili kumfanya kocha amwamini na kumpa nafasi ya kucheza kitu ambacho hata yeye kakifanya ili kujitengenezea nafasi ya kuaminiwa na kucheza.

DAKIKA

Kiungo huyo amecheza dakika 1062 kwenye mechi 15 kati ya 17 zilizochezwa na timu hiyo huku akihusika kwenye mabao nane kati ya 42 yaliyofungwa na Yanga.

Amefunga mabao nane dhidi ya KMC, Namungo, Dodoma Jiji, Mashujaa na mawili dhidi ya KMC huku akitoa asisti kwenye mechi dhidi ya Geita Gold, Namungo FC na jana jioni akifunga bao dhidi ya Ihefu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUPATA 'PANCHA' INGINE....KRAMO NNJE WIKI MBILI....