Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA CAF KESHO KUTWA…MAMELOD WAINGIA UBARIDI KWA YANGA…

KUELEKEA MECHI YA CAF KESHO KUTWA…MAMELOD WAINGIA UBARIDI KWA YANGA…

Habari za Michezo leo

Benchi la ufundi la Yanga linaendelea na maandalizi ya mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi itakayopigwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini jana limenasa taarifa za wapinzani wao wakipanga kuja fulu mziki kwa ajili ya mechi hiyo.

Yanga inafahamu miamba hiyo ya Afrika Kusini itawasili nchini, Machi 28, ikiwa ni siku mbili kabla ya mechi ikiwa na msafara usiopungua watu 70 na kati yao, 30 ni wachezaji wa timu hiyo.

Katika kundi hilo watu 40 ambao sio wachezaji, kuna makocha na maofisa wa benchi la ufundi, lakini Mamelodi pia itaingia ikiwa na walinzi maalumu kwa ajili ya kuwalinda mastaa wa kikosi hicho muda wote ambao watakuwa hapa nchini.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimefichua wamenasa taarifa, Mamelodi itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ndege ya kukodi itakayowasubiri ili mara baada ya mechi warejee fasta Sauzi bila presha.

“Tunafahamu ipo hoteli moja iliyo jirani na ufukwe wa Bahari ya Hindi ambayo ndio msafara wao utafikia na tayari wameshatuma taarifa za kuomba vibali kwa ajili ya ndege watakayokuja nayo ambayo itakuwa ya kukodi,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga na kuongeza;

“Inaonekana jamaa wamejipanga sana lakini na sisi kwa upande wetu tunaendelea kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo kwa vile tukipata ushindi mnono, utatuweka katika nafasi nzuri ya kuingia hatua ya nusu fainali.”

Mwanaspoi linafahamu Mamelodi imeamua kuja na walinzi maalumu ambao jukumu lao ni kuhakikisha hakuna mwingiliano wowote kati yao na wachezaji wa timu hiyo pindi watakapokuwa hoteli au uwanjani wakati wa mechi na mazoezi.

Timu hiyo pia imepanga kutotumia usafiri wa basi ambao Yanga imeuandaa kwa ajili yao katika kipindi chote itakachokuwepo hapa nchini na itajigharimia na kuandaa usafiri wake na tayari imeshatanguliza maofisa wa awali hapa nchini kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

MASHABIKI 400

Kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuandika barua kwenda kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuijulisha, mechi hiyo itachezwa kwa kufuata kanuni na taratibu za soka zilizowekwa, kimeonekana kuwapa mzuka Mamelodi wanaotarajia kusafirisha idadi kubwa ya mashabiki wao kuja nchini kuwaunga mkono katika mechi hiyo.

Timu hiyo inaripotiwa kuomba nafasi ya mashabiki wapatao 400 kwa ajili ya kuingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuishangilia.

Inadaiwa, Mamelodi ilionyesha wasiwasi wa kusafirisha mashabiki wake kuja nchini kushuhudia mechi hiyo, baada ya kauli iliyotolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk.

Damas Ndumbaro, ili shabiki wa timu pinzani ya Simba au Yanga aruhusiwe kuingia uwanjani katika mechi hizo za mwishoni mwa wili ijayo, anapaswa kuonyesha hati yake ya kusafiria ya nchi inazotoka timu hizo akilenga kuhamasisha uzalendo, japo alishaanza kupingwa na baadhi ya wadau mapema.

Hata hivyo, katiba barua iliyoandikwa na TFF, imeijulisha taratibu zote za mpira wa miguu zitafuatwa katika mchezo huo na hakutokuwa na zuio lolote kwa mashabiki.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linalihakikishia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mechi husika itachezwa kwa kanuni na taratibu zilizowekwa za soka na namna ya utaratibu wa kuingia uwanjani.

“Kwa hivyo, sio kwamba pasipoti (pasi za kusafiria) zitatumika kama kigezo cha kuingia uwanjani kwa mashabiki wa Mamelodi Sundowns na mtu yeyote kwa sababu mechi ipo kikanuni na taratibu za mpira wa miguu bali sio kwa Idara ya Uhamiaji.

“Timu ya Mamelodi Sundowns imehakikishiwa usalama wao kutoka kwa vyombo husika wakati wote ambao watakuwa nchini na kuheshimu taratibu za mechi yao dhidi ya Young Africans SC, na Dhamana hii pia inawahusu maafisa wa mechi, mashabiki wa Sundowns wanaosafiri pamoja na mashabiki wanaoishi Tanzania na anaetaka kuhudhuria mechi hiyo,” ilifafanua barua hiyo.

SOMA NA HII  YANGA IMERUDI KWA KAZE, YAMPA OFA HIZI HAPA MBILI SIO POA