Home Habari za michezo HATARI YANUKIA LIGI KUU….MMILIKI MPYA WA IHEFU HAJULIKANI TFF….ISHU NZIMA IMEKAA HIVI…

HATARI YANUKIA LIGI KUU….MMILIKI MPYA WA IHEFU HAJULIKANI TFF….ISHU NZIMA IMEKAA HIVI…

Habari za Michezo leo

Kwa wiki takribani nne kumekuwa na mjadala kuhusu udhamini wa jezi wa Kampuni ya GSM na kampuni zake nyingine kwa klabu tofauti za Ligi Kuu Bara, baadhi ya watu wakihusisha na matokeo baina ya timu zilizo kwenye udhamini mmoja.

Ingawa mjadala huo umejibiwa kwa majibu mazuri na mengine ya kebehi, kama yale ya kuhoji matokeo mabaya ya timu ambazo hazimo chini ya udhamini wa GSM na kampuni zake, lakini ungefaa ufikirishe wenye mamlaka na wadau wengine wa mchezo huu pendwa.

Hii inazidishwa na majibu ambayo kiongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyotoa kwa waandishi waliotaka kujua chombo hicho kinachukua hatua gani kwa madai hayo, hasa yale ya mabadilishano ya umiliki wa klabu za Ihefu na Singida United baada ya mmoja wa watu wanaosadikiwa ni wamiliki wa Ihefu, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni mmoja wa wadhamini wa klabu ya Young Africans Sports Club, maarufu kwa jina la Yanga.

Ni kwamba siku moja kabla ya kucheza na Yanga, Nchemba alienda kambi ya Ihefu kwa kile alichokieleza ni kuongeza nguvu kwa timu hiyo ambayo hadi wakati huo ndiyo pekee ilikuwa ishaishinda Yanga msimu huu. Lakini matokeo yakawa mabaya kwa Ihefu, ambayo sasa inahamia mkoani Singida, ambako Mwigulu ni mbunge wa moja ya majimbo.

Ihefu ilikubali kipigo cha mabao 5-0 na kukoleza mjadala huo wa udhamini wa kampuni moja kwa klabu tofauti na ambao sasa ulichukua sura ya mtu mmoja kumiliki klabu tofauti, huku ukihoji sababu za mdhamini wa Yanga kuitembelea kambi ya timu pinzani kabla ya mechi ya Ligi Kuu.

Majibu ya TFF yalikuwa; “Tatizo ni vigumu sana kuwajua wamiliki wa hizi klabu”, akijaribu kuonyesha imewawia vigumu kutekeleza kanuni za Leseni za Klabu inayokataza mtu mmoja, kampuni au taasisi kumiliki zaidi ya klabu moja zilizo katika ligi moja.

Majibu hayo yanafikirisha. Kwamba TFF haijui hata wamiliki wa klabu zinazoshiriki mashindano yake? Kama haijui itawezaje kudhibiti au kuratibu ushiriki wake katika dunia ya leo ambayo mchezo wa soka unaangaliwa kwa macho mawili kuhakikisha klabu zinazoshiriki haziyumbi kiuchumi na kuvuruga mashindano, dunia ambayo inataka uwepo na udhibiti mkubwa wa fedha zinazoingizwa kwenye soka ili zisitokane na vyanzo vichafu au mchezo huu usitumike kusafisha fedha chafu, dunia ya leo inayotaka kuwepo na uwazi katika uendeshaji wa klabu na hasa katika masuala ya fedha.

Kwa TFF kutojua wamiliki wa klabu zinazoshiriki mashindano yake ni kitu cha hatari na kinakaribisha zaidi vitendo vinavyoendelea vya klabu kubadilisha umiliki wake kiholela bila ya kuwepo na taarifa rasmi zinazoonyesha uuzwaji huo umegharimu kiasi gani na kilichosababisha mmiliki mmoja auze klabu kwa mwingine kana kwamba ni ile biashara ya zamani ya ‘mali kwa mali’.

Ukiliangalia hilo na lile lililokwamisha mchakato wa klabu ya Simba kuuza sehemu ya hisa zake kwa mwekezaji, utaona ni kwa nini Kamisheni ya Ushindani wa Haki (FCC) iliagiza Simba isubiri mwongozo utakaotolewa na TFF kuhusu umiliki wa klabu za Ligi Kuu kabla ya kukamilisha mchakato wake wa kuuza hisa kwa wawekezaji.

Ni sahihi kabisa kwamba sasa TFF haina budi kukaa chini na kutunga kanuni ambazo zitaongoza umiliki wa klabu zilizokuwa za wanachama, za watu binafsi na zile zinazomilikiwa na kampuni au taasisi ili pia kuwepo na uitaratibu ambao una uwazi katika kubadilisha wamiliki, kama ilivyofanyika kwa Singida Fountain Gate, ambayo awali ilikuwa Singida Big Stars, na Ihefu, ambayo muda si mrefu inaweza kubadilishwa jina.

Kama wanaoamini Mwigulu ameinunua Ihefu kuilainishia Yanga mechi dhidi ya timu hiyo ambayo hata msimu uliopita ilikuwa moja ya timu mbili zilizoishinda Yanga, wataachaje kuendelea kuamini iwapo Mwigulu ataachana na Ihefu na kuinunua klabu nyingine inayoonekana kuwa tatizo kwa Yanga na matokeo yakawa kama ya Ihefu? Kwa sababu hakuna kanuni zozote zinazoongoza uuzwaji wa klabu wala umiliki kulingana na kanuni za Leseni za Klabu.

Kama imani hiyo itasambaa na hakuna ilani yoyote, nani atamzuia mtu mwingine kununua klabu kwa lengo la kuilainishia klabu yake pendwa matokeo?

Kwa haraka haraka huoni hilo likitokea katika kipindi kifupi kijacho, lakini haitakiwi lisubiriwe hadi litokee. Wakati huu mzuri kuanza kudhibiti umiliki wa klabu kwa angalau TFF kuanza kuhakikisha kuwa kila klabu inawasilisha kwake vielelezo vya wamiliki wa klabu vilivyothibitishwa na serikali kabla ya kuanza kwa msimu au wakati mtu binafsi, taasisi au kampuni anataka kuinunua klabu.

Kwa wenzetu wa barani Ulaya, ambako watu hawataki tujilinganishe nao, ni rahisi kujua wamiliki kwa sababu klabu nyingi ni mashirika yaliyosajiliwa rasmi na hivyo yanawajibika kwa mamlaka za serikali kama zilivyo kampuni nyingine. Kwa sasa ili kulinda mpira, nchi kama Uingereza inaelekea kuwasilisha muswada ambao utazidisha udhibiti wa klabu kutokana na kuanzisha ofisi ya Msajili wa Klabu licha ya Chama cha Soka cha England kuwa na msajili wake.

Si kitu kizuri kwa klabu kumilikiwa na mtu aliye nyuma ya pazia na ambaye hajulikani kabisa, na ambaye hata akiamua kuondoka huwezi kumlazimisha abakie kwa sababu hukujua kama yupo. Matokeo yake yatakuwa kama ambavyo Singida United, ambayo pia iliaminika ilikuwa inamilikiwa na Mwigulu, ilisambaratika kwa mara ya pili baada ya ile Singida ya kwanza iliyokuwa ikimilikiwa na Mohamed Dewji.

Hii itasaidia kudhibiti hata maamuzi kama ya Alwxander Mnyeti ambaye aliamua kuiondoa klabu yake ya Gwambina kwenye ligi, akisema ni heri atumie uwanja wake kulisha mifugo kuliko kutumika kwa soka.

Hali kadhalika itadhibiti tabia ya klabu kuinunua klabu nyingine iliyo daraja la juu ili irejee kwenye ligi ya juu kirahisi kama ambavyo Pan African, Pamba, Moro United, African Lyon na nyingine zimejaribu kufanya na baadhi kufanikiwa.

Kwa kiasi fulani tumeshafanikiwa sana katika uendeshaji mashindano yetu kwa hiyo tunatakiwa tupige hatua nyingine kubwa ya kuanza kudhibiti umiliki wa klabu na kutaka uwazi katika mapato na matumizi ya fedha ili kuwa na uhakika zaidi katika uendeshaji na upangaji mipango mikubwa zaidi inayotaka uhakika wa uchumi wa klabu.

Kwa hiyo, kusema ni vigumu kujua wamiliki wa klabu kwa sababu wanafanya siri sana, hakutoi mwanga wa kumalizika kwa matatizo mengi yanayoonekana kuunyemelea mpira wa miguu, huku kukiwa na maswali mengi na yasiyo na majibu kuhusu uwezekano wa mechi kuchezwa nje ya uwanja kutokana na usiri huo.

SOMA NA HII  SIMBA NA MZIMU WA SARE ULIOKITA MIZIZI MSIMBAZI